VITABU VYA UINJILISTI KUTOKA LIFE CHALLENGE AFRICA NI MUHIMU SANA KWA WANAOPENDA KUISHUHUDIA KWELI KWAO WALI NJE.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Leo nakukaribisha wewe kununua vitabu kutoka kila duka la vitabu vya Kikristo kwa ajili ya kujifunza zaidi ushuhudiaji na kuongeza ufahamu kuhusu jamii inayokuzunguka. Vitabu hivi vimetolewa na Life Challenge Africa. hakika hivi ni vitabu bora sana, mimi binafsi vilinisaidia sana nilipokuwa naishi Zanzibar.
Bei yake ni sawa na bure, vitafute tu katika maduka maana viko kila sehemu. ubarikiwe sana na endelea kutumikwa kwa BWANA YESU maana uko uzima wa milele katika yeye.

AL KITAB - KITABU CHA VITABU
Kosi kwa njia ya posta yenye masomo 18 kuhusu Biblia. Mafundisho haya yametayarishwa na Wakristo kwa ajili ya Waislamu ambao wangependa kuielewa Biblia jinsi waielewavyo Wakristo. Baadhi ya maswala yanayoshugulikiwa ni maisha ya Yesu, ujumbe wa Injili, watu wa kitabu, yaani wafuasi wa Kristo, nk. Kila somo linaandamana na maswali ya kufanya ili mwanafunzi ajipime ufahamu wake ana-vyoendelea kukisoma kitabu hiki ambacho kimeandikiwa kwa lugha nyepesi inayoeleweka kwa urahisi sana.

ACHA BIBLIA IJISEME YENYEWE
Waislamu wameandika vitabu vingi vinavyoshambulia ukweli wa Biblia. Hata hivyo, Mwialmu yeyote anayedhamini ukweli sharti achunguze na aelewe jibu la Wakristo dhidi ya madai hayo. Ni jukumu la kila Mwislamu kufahamu kwa nini Wakristo hawaamini kwamba Biblia imegeuzwa.
Kuna ushahidi mwingi unaothibitisha kwamba haingewezekana kwa mtu yeyote kuigeuza Biblia. Ni vema Mwislamu aisome Biblia yeye mwenyewe bila upendeleo wowote na airuhusu Biblia ijisemee yenyewe kuhusu swala hili.
Tumeambatanisha utaratibu wa kusoma Biblia kwa miezi miwili ya kwanza.

UJUMBE WA NABII ISA
Ikiwa kweli Yesu ni nabii wa Mungu, je, ujumbe wake ulikuwa upi? Itawafaa Waislamu ikiwa watausoma ujumbe wa Masihi Yesu uliomo katika kitabu hiki ambacho kimenukuu sana kutoka kwenye vitabu vya Injili katika Biblia. Mwislamu yeyote anayekisoma kitabu hiki atagundua kwamba ni jambo la busara kufuata ukweli uliothibitishwa badala ya kufuata tu mambo anayoambiwa na watu wengine.

MPENDWA ABDALLAH
Bila shaka utafurahia kusoma "barua" hizi zilizoandikwa na Theofilo (mpendwa wa Mungu) kwa Abdalla (mtumishi wa Allah). Lengo la kitabu hiki ni kutufunza kwamba, inawezekana kumuelezea Mwislamu Injili bila kumkasirisha. Hata hivyo, jambo hili linawezekana tu ikiwa tunaielewa imani ya kiislamu ili tunapozungumza na Mwislamu tunaheshimu pia hisia zake za kidini.

SABABU ZILIZONIFANYA NIWE MKRISTO
Kijitabu hiki kinatoa ushuhuda wa kushangaza ya jinsi Mwislamu msomi aliyekuwa pia na cheo cha juu alipopata kuujua ukweli. Ingawa kisa hiki kilitokea zaidi ya miaka mia moja iliyopita, bado ushuhuda huu una mvuto wa kipekee. Kutokana na kujihusisha kwake katika mihadhara na kusoma Kuran and vitabu vya Hadithi (Mapokeo ya Kiislamu) huku akilinganisha yale aliyoyasoma na ukweli wa Biblia, mwishowe msomi huyu hakuwa na lingine ila kuukubali ukweli wa Biblia na hivyo akaweza kupata msamaha wa dhambi na amani katika Kristo.

USAFI NDIO UTAKATIFU
Waislamu wengi huamini kwamba uislamu ndio dini safi kuliko zingine zote. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, ni rahisi kudumisha usafi wa kimwili kuliko usafi wa kiroho. Lakini watu wenye roho safi ndio tu watakaomwona Mungu.

SABABU NNE THABITI
Trakti hii inatoa changamoto kwa kila mwanadamu ajisomee neno la Mungu yeye mwenyewe. Kwani kutofanya hivyo kutatufanya tunaswe katika mtego wa Shetani. Lakini je, tunalijua hilo neno la Mungu?

UNAFIKIRI NINI KUHUSU MASIHI
Upekee wa Masihi Yesu umeelezwa kwa kifupi lakini kwa njia ya kuvutia. Mambo ambayo yamezingatiwa kuonyesha kwamba Yesu ni zaidi ya nabii ni pamoja na kuzaliwa kwake, sifa zake, ushindi wake dhidi ya kifo, na mengine mengi. Bila shaka huu ni ujumbe mwafaka na unaofaa sana hasa kwa Mwislamu ambaye mnakutana naye kwa muda mfupi tu.

KIDOLE CHA MUNGU
Hebu fikiria ujumbe ulioandikwa moja na mkono wa mungu. Bila shaka hili ni jambo la kushangaza nala kuogofya. Lengo la trakti hii ni kumfanya msomaji afikirie kwa makini hali yake ya kiroho, sasa na itakavyokuwa baadaye.

YUSUFU AULIZA PETER - FATUMA AULIZA GRACE
Hii ni trakti ambayo inampa Mkristo majibu kwa maswali yote ya msingi ambayo Waislamu hutoa ili kujaribu kuipinga Biblia na Ukristo kwa jumla. Hiki ni kitendea kazi kwa Muinjilisti Mkristo kubeba kila wakati popote aendapo na hata kumpa Mwislamu ili ajisomee mwenyewe.

STORY TELLER
Huu ni msururu wa trakti tano. kila moja inasimulia kisa kifupi kutoka Mashariki ya Kati. Mafunzo yaliyomo yanagusia maisha ya kila siku ya Mwislamu. Kwa hivyo trakti hizi zinafaa kwa kila Mwislamu popote alipo. Kadiri msomaji anaposoma, ndipo mafunzo muhimu ya Injli yanajitokeza kwa njia ambayo si ya kutisha. Hiki ni chombo kizuri sana cha kupanda mbegu ya Injili.

Comments