KUONDOA MABAYA NYUMANI MWAKO

Na Frank Philip Seth.

"Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake" - (Mithali 17:13).
Nimetafakari sana Mithali 17:13 na kuangalia maana ya kurudisha mabaya badala ya mema. Nimeona mambo yafuatayo:
Neno "badala" linaonesha kwamba mtu alitendewa jambo jema ila yeye akatenda baya kwa huyo aliyemtendea jambo jema. Lakini pia ukiangalia kwa maana pana zaidi, inawezekana mtu hutendewa mema na watu fulani lakini yeye huwatendea watu wengine mabaya tu, bila kujali kama hao watu walimtendea nini.
Sasa angalia tena kwa namna nyingine. Fikiri mtu fulani anashida, na unajua shida yake (kwa msukumo wa ndani) ila ukakaa kimya hadi shida yake ikamwangamiza. Je! hiyo nayo sio kutenda ubaya? Mwingine atasema, "kwani aliniomba?" Sawa, ni haki kuombwa msaada ndipo utoe, ila kumbuka, "haki yetu ISIPOZIDI ya mafarisayo (watu wa sheria na utaratibu) hatuwezi kuurithi Ufalme wa Mungu".
Dawa ya kuondoa MABAYA sio kutengeneza SILAHA bora zaidi na kujifunza mbinu bora zaidi za VITA, ila ni KURUDISHA MEMA au KULIPA mema kwa UBAYA. Na hii ndio maana halisi ya KUWAPENDA adui zetu. Kama tunawapenda, basi hatutawatendea mabaya. Kumbuka, Kanuni ya BWANA, "kuwaombea wanaotuudhi", usipoweza kumwombea anayekuudhi hata akiwa katika UHITAJI hutaweza kumtendea WEMA.
Faida ya kufanya haya ni KUONDOA mabaya nyumbani mwako na kujiongezea AMANI nafsini mwako, naam, zaidi sana, kujiongezea haki zaidi ya ile ya Mafarisayo ambao hutenda mema kwa sababu pia walitendewa mema.
Kumbuka, kadri UMTENDEAVYO adui yako MEMA, hofu yako kwake inaongezeka. Ukitaka kujua jambo hili, fuatilia hadithi ya mfalme Sauli na Daudi wakati Sauli anamwinda Daudi ili amuue. Kadri Daudi alivyozidi kumlipa Sauli mema badala ya mabaya, ndivyo Sauli alivyozidi kumwogopa Daudi.
Frank P. Seth

Comments