KUPINGWA NA MUNGU - I

Na Frank Philip Seth
“Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema” (1 Petro 5:5).
Kwa miaka mingi nimeweka moyoni mwangu neno “Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema”. Nimejiuliza katika matafakuri yangu, hivi kupingwa na Mungu maana yake ni nini? Mungu anampingaje mtu? Je! Utajuaje kama sasa una kiburi na unapingwa na Mungu?
Kuna mambo machache ya kutazama:
i. Mifumo ya kidunia
Dunia na vilivyomo havikuumbwa ili viendeshwe kwa MIUJIZA japo Mungu ni mtenda miujiza.
Mungu alipomuumba Adam, na kisha Hawa, hakuwaambia kabisa habari za miujiza, ila aliweka mifumo na njia za kuishi kisha akawakabidhi MAJUKUMU na kuwaelekeza yawapasayo kufanya. Kufanikiwa kwao hakukuwa katika NGUVU za MIUJIZA ila KULITII Neno la Mungu.
Miujiza ipo, na ni dhahiri sana, ila kwa SABABU na KUSUDI maalum. Siku zote Mungu hutumia MIFUMO halisi Aliyoiumba KUTIMIZA malengo yake, na IKISHINDIKANA, Yeye huweza kufanya jambo ZAIDI ya uwezo wa KIMFUMO (muujiza), ila kwa SABABU na KUSUDI maalumu. Yeye ni Mungu.
Angalia mfano wa BWANA Yesu. Siku zote alitumia mashua kuvuka mto (majini) (Mathayo 9.1, Mathayo 8:23-26). Siku moja, BWANA alitaka kujipatia nafasi ili ahubiri vizuri, hakuonesha ‘show’ ya kusimama majini huku anahubiri, alitumia mashua (Mathayo 13:2). Siku BWANA alipowaambia wanafunzi watangulie kwenda ng’ambo, na ikawa ni jioni, hakuna namna ya kuvuka ng’ambo kuwafuata, ndipo alipoita muujiza wa kutembea juu ya maji (Mathayo 14:22-27). Kumbuka, hapakuwa na WATAZAMAJI na wala hakufanya Muujiza huo ili WATU WAONE tu na kujua UWEZO wake.
Tunasoma habari ya bahari ya Shamu kupasuka na watu kuvuka kwa miguu. Hiyo ilitokea ila mara moja (kwa Musa), watumishi wengine wote wa Mungu walivuka, ila kwa vyombo vya majini. Yordani ilipasuka, ila mara tatu tu (kwa Joshua, Elia na Elisha), watumishi wengine wote walivuka kwa vyombo vya majini (mifumo ya kidunia). Imekupasa kufanya kazi na kutii Neno, miujiza ipo ila sio suluhisho la kwanza, chukua hatua zako ukiongozwa na kutii Neno la Mungu, utafanikiwa; Ikibidi, ita muujiza.
ii. Neema zaidi ya ile iokoayo
Neema imetafsiriwa kama “kitu cha bure, ambacho mtu hupokea pasi na kustahili”. Nimesikia watu wengi wakitafsiri neema kwa maneno hayo. Sipingani nao sana, ila nimeona kuna maana pana zaidi ya neema na KUGUNDUA kwamba neema sio kitu cha BURE tu. Sawa, inawezekana umepewa pasipo kustahili (hukuwa na haki ya kudai kama ilivyo malipo), bali jua kwamba unauwezo mkubwa sana wa KUIKUBALI au KUIKATAA neema! Basi nikaona jambo hili, yapo “mambo” unapaswa kufanya (sio bure) ili upate NEEMA, moja wapo ni KUONDOA kiburi ndani yako!
Kwa lugha nyingine, kuna GHARAMA kwa wote wawili, apokeaye au ATOAYE neema. Ndio maana “tumenunuliwa kwa Damu ya thamani”, hatukupatikana bure, BWANA alilipa gharama, naam, nasi pia, tunalipa gharama KUIPOKEA hii neema, japo ni bure (kwa sisi tupokeao), ila, imetupasa kulipa gharama maana hii neema INATUFUNDISHA namna ya kuishi (kukataa dhambi na mambo ya kidunia), je! Hiyo sio gharama?
Nikatazama tena nikaona GHARAMA ingine, na NEEMA ingine; jinsi tuishivyo na watu wengine katika jamii. Petro anasema, “…watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema”. Hii mistari inaonesha namna ya kuenenda ili KUFUNULIWA neema zaidi ya ile iliyokuokoa! Lakini ufunguo wake unapatikana kama hatuna kiburi.
iii. Kupingwa na Mungu
Mara nyingi neno “kupingwa na Mungu”, limechukuliwa kama Mungu kuingilia kati mambo yako na kukuzimisha kama mtu apulizavyo mshumaa. Kiburi hakimwangamizi mtu kwa mtindo huo, ila taratibu. Ndio maana tunaambiwa “aonywaye MARA NYINGI akishupaza shingo itavunjiaka na wala hapati dawa”. Neno “Mara nyingi” maana yake ni kurudia rudia kwa muda mrefu, sio ghafla tu. Na kwa sababu ya kiburi, mtu hupuuza MAONYO, TAHADHARI au MAFUNDISHO na kisha kuangamia. Hakuna mtu ambaye ataangamia kwa kiburi chake ASIJUE mahali alipoonywa, aitha kwa ‘sauti ya ndani’ au ‘ya watu wengine’ wakimwambia juu ya jambo lile lile na hakuchukua hatua zozote.
Kupingwa maana yake ni kukosa NJIA au RUHUSA ya kufanikiwa katika jambo fulani. Ghafla! Hii mifumo ya kidunia ambayo Mungu aliiweka kwa ajili ya wanadamu inaanza kushindwa kufanya kazi kwako, mambo yasiyotarajiwa yanaanza kukumba japo umeweka nguvu na jitihada zako. Na hii inaanza kujitokeza kidogo kidogo, huku maonyo yakikujia. UkiZIDI kushupaza shingo, mifumo itaZIDI kukupinga hadi kukumaliza.
Mfano, fikiri mafuriko yanawakumba wote, mwenzako anasukumiwa mwambani ili awe salama, wewe unasukumiwa kwenye maporomoko ukaangamie huko. Wote wawili mmesukumwa na mafuriko yale yale, mmoja anapata NEEMA (kwa kusukumiwa mwambani), na mwingine hapati na kuangamia. Ona tena, shida ya mvua ni kwa wote, mwenzako anavuna angalau kidogo, wewe unaambulia mabua matupu! Neema inakuja kuingilia kati mahali ambapo wewe huwezi tena, naam, hapo ni mahali pa muujiza pia.
Frank P. Seth.

Comments