KUSHINDA MAWAZO YA KISHETANI

Na Mchungaji Bryson Lema, Ufufuo na uzima Morogoro
Utangulizi: Shetani ana uwezo  wa kugeuka na kubadilika,  na kutumia maumbo au vitu tofauti kwa lengo la kuwakamata watu ili wasifikie hatima zao.  Shetani ana uwezo wa kugeuka na kufanana na jiwe (ingawa yeye siyo jiwe) lakini kwa macho ya kawaida unaliona ‘jiwe’ kumbe katika ulimwengu ule wa roho yeye siyo jiwe, amejigeuza tu. Anachofahamu shetani ni kwamba, akija na kukaa ndani yako, atatolewa mara moja pale unapoombewa ila akikaa ndani ya maumbo hayo au katika mavazi (nguo) wewe siyo rahisi umbaini.

Shetani huwa na uwezo wa kujificha hata katika mavazi bila wewe kujua. Unaweza kuwa unavaa nguo fulani na mara zote uzivaapo tatizo huanzia pale. Katika  kitabu cha MWANZO Mungu alishuka toka mbinguni kuja duniani kwa lengo la kumshonea Adamu na Eva mavazi kupitia ngozi ya kondoo  aliyemchinja kwa ajili hiyo. Mungu angeweza kumwambia Adamu afanye hiyo kazi, lakini unajua kwa nini alifanya mwenyewe? Mungu pia alimwambia Musa amtengenezee Haruni mavazi matakatifu. Kumbe mavazi yaweza kuwa matakatifu au kinyume chake.

Endapo maduka ya mavazi yapo mijini kote na wauzaji wake wanawasha  ubani kwa lengo la kuyalisha mashetani chakula, kipi kinatokea uyanunuapo vazi la aina hiyo? Maana yake,  wewe unaweza kulinunua vazi la aina hiyo  bila kujua kuwa nguo hiyo  ilikuwa inapuliziwa chakula  cha majini na ukaona ni nguo nzuri tu, kumbe haina uzuri wowote. Nyoka alipomuonesha Eva lile tunda, Eva kwa mara ya kwanza alilitamani akasema linavutia na lafaa kula. Lakini hebu jiulize, kwani Eva alikuwa mara zote halioni hilo tunda hapo bustanini?
Kwenye Biblia, Mavazi yaliponya watu. Yule mwanamke aliyekuwa anatokwa  damu,  alilishika pindo la vazi la Yesu. Kilichomponya siyo lile vazi, bali nguvu ya Yesu ilitoka kwake na kuingia kwenye lile vazi. Bartmayo kipofu wakati wa uponywaji wake, alilitupa lile vazi mara moja na papo hapo akapata uponyaji wake. Kumbe pengine lile  vazi ndiyo lilificha shetani wa upofu wake ule. Pale msalabani, nguo  za Yesu zilipigiwa kura,  na siyo viatu vyake. Kwa nini iwe hivyo? Tunaona katika Biblia watu wanatumia leso za mitume kama akina Paulo na papo hapo  wanapata uponyaji.
Nitajitoa je mimi nisivae hayo mavazi ya kishetani? Kwanza utambue kuwa Shetani anaweza kutumia vitu unavyonunua madukani.  Pili inabidi  ujue namna ya kuepuka au kufanyia  maombi vitu hivyo kabla ya kuvitumia.  Kila nguo  unayoinunua kuanzia leo hii inenee maneno  ya Bwana. Weka neno la Mungu katika hiyo nguo kabla hujaanza kuivaa. Kumbuka tunayo  mamlaka kuliko wao. Imeandikwa “tumempewa mamlka ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za Yule adui,  wala hazitatudhuru”. Weka maneno  ya Mungu kwenye hizo nguo unazonunua ili kwamba kila wakati utakapozivaa nguo  hizo neno  la Mungu litangazwe.

Imeandikwa katika 2 KORINTHO 2:11…[ Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.]….Katika maisha yako ya kila siku yapo mawazo ya shetani. Anaowaza shetani,  hupanga pia mipango ya jinsi ya kukukamata.  Njia atakazotumia shetani kukukamata wewe siyo hizo atakazotumia kumkamata mwingine.

AYUBU 1:6-10…[Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. 7 Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzungukazunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. 8 Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. 9 Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? 10 Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.]… Shetani ni mtu wa kufuatilia vitu na kuwaza jinsi ya kuwafunga watu. Mungu alitaka kujua kama shetani  amemuona Ayubu lakini  majibu ya shetani na mawazo yake ni kuwa, ‘ee Mungu  ondoa ulinzi uliomwekea Ayubu’. Shetani anajua uliinzi wa Mungu ukiondoka, mwanadamu hana chochote.
Inapaswa kujua kuwa, yapo mawazo  ya shetani  yaliyo kinyume na wewe kila iitwapo leo. Saa imefika na saa ni hii, kila wazo la  kishetani kwenye maisha yangu, kwenye ndoa yangu, kwenye kazi yangu au uzao wangu liteketezwe kwa Jina la Yesu. Unaweza kuwa kwenye amani, ukiwaza kuwa upo salama lakini  kile usichokijua ni  kuwa lipo wazo baya la kishetani ambalo linasogelea maisha yako au vitu vyako.
UFUNUO 2:24…[ Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.]…. Zipo fumbo za shetani. Shetani huwaletea watu vitu vinavoitwa ‘fumbo’. Ukiona fumbo ujue aliyelitengeneza ni mtu mwenye akili sana. Mtu wa kufumbua fumbo naye ni lazima awe na akili  sana kumpita aliyetengeneza fumbo.  Shetani anapotengeneza fumbo lake, anajua akilileta kwako siyo rahisi ulifumbue. Katika ndoa unaweza kuona mambo usiyoyaelewa, lakini wewe bila kujua unaanza kuwawazia majirani au marafiki lakini kumbe lile ni fumbo na hao unaowawazia siyo wahusika wakuu.  Ndiyo  maana wengi  hukimbilia kwenye kutibu matunda ya tatizo badala ya chanzo cha matatizo hayo.  Mfano: Mtu anapotaka aombewe kupata kazi, akidhani kukosa kazi ndiyo tatizo. Lahasha‼. Kukosa kazi siyo tatizo ila ni  tunda tu. Kipo chanzo cha hiyo kukosa kazi ambacho inabodi kishughulikiwe.

Hebu jiulize, je shetani ananiwazia nini mwaka huu? Vile vitu  unavoviwaza kuvifanya mwaka huu vimekaa je? Shetani katika hivyo vitu unavyowaza kwa mwaka huu amekuwazia nini? Usipoweza kufahamu  mawazo ya huyo shetani juu yako, hata yale uliyopanga hayatatokea.  Unaopopigwa na  mawimbi makali,  ni wakati wa kwenda kumuamsha Bwana ili asimamishe mawimbi. Yupo aliyeleta mawimbi. Petro alijaribu njia zote kwa kuwa alikuwa mtaalamu wa uvuvi na hivyo kwa yale mawimbi alivyoyaona,  akasema hapana, huu ni wakati wa kumuamsha Bwana na ndiye wa kuweza kuyanyamazisha. Mawimbi yanappokuja siyo kwa ajili ya kukuangamiza, lakini uyaonapo, ni budi kutafuta alipokaa Bwana Yesu ili aje na kuyanyamazisha mawimbi ili uende ng’ambo.

2 TIMOTHEO 2:26…[ wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.]… Paulo haongelei  mambo ya imani  hapa.  Anaongelea mambo ya ufahamu. Mtu  akitengeneza mpango,  inahitaji mtu mwenye ufahamu na akili  kugundua huu ni  mtego wa ibilisi. Kipo  kifungo ammbacho kinahitaji tu akili zako.  Ukirudi kwenye ufahamu wako,  utaenda kwa Yesu Kristo na kumweleza shida yako ili tatizo lililopo  litoweke kwa Jina la Yesu. Wenye ufahamu wa dunia hawawezi kukupa akili ya kufanikiwa, ila yupo  mmoja tu mwenye uwezo huo,  naye ni Yesu Kristo

1 YOHANA 5:18-20…[Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi. 19 Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu. 20 Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele.]… Dunia yote imekaa chini ya muovu lakini tumepewa akili za kuweza kuwatawala hao waovu. Shetani anatamba kwa kukusumbua pale ambapo unakuwa hujitambui. Kile usichokijua ni kuwa, hata boss wako anayekusumbua ofisini mwako unao uwezo wa kumfunga nyumbani kwako na kumwambia ‘nyamaza kimya’.  Cha kufanya ni kuyatiisha mapepo yaliyo ndani mwake na kuyaamrisha ‘kuazia leo mnyamaze kimya’na lazima yatakutii . Paulo kwa kujitambua, alimwambia Elima yulee mchawi maneno haya: MATENDO 13:11Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazungukazunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.’.Kila adui yangu kazini au katika uzao wangu au katika maisha yangu napaswa kumuambia ‘uwe kipofu’.  Sifa kuu ya kipofu ni kuwa hakioni kinachoendelea. 

Ninayo pia mawazo ya Mungu, zaidi ya yale mabaya anayoniwazia shetani. Imeandikwa katika YEREMIA 29:11…[Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.]…. Mungu anakuwazia mema lakini adui  anawaza mabaya. Uonapo vurugu katika ndoa ujue siyo mawazo ya Mungu bali ni shetani. Haya maovu ya shetani anayoniwazia,  ndiyo yanayonifanya niwe katika hali ngumu nisiyoitaka. Kiwanda kikiungua zile bidhaa hazitengenezwi tena. Kiwanda kinachotengeneza vurugu, shida na magonjwa ni cha mashetani.  Leo tunaingia kwenye hicho kiwanda na kukifunga kwa Jina la Yesu.
Leo ni siku ya kupiga X vibanda vyote ambavyo mashetani wamevijenga kwenye njia yako ya ushindi na baada ya hapo kuwaagiza malaika kazi ya kuchoma vibanda vyote vya adui zangu walivyojenga kwenye njia zangu za mafanikio. Kama vile malaika alivyopita Misri usiku ule na kuua wazaliwa wa kwanza wote wa Misri ambao alama ya damu ya mwanakondoo haikuonekana kwenye milango yao,  hata sasa itakuwa vivyo  hivyo kwa adui zako, na kila kibanda walichojenga kwenye barabara yako, leo ni siku ya kupita na kuweka alama ya X na malaika wa Bwana atafanya usafi  kwa kuviondoa vibanda vyote vya adui kwa Jina la Yesu

Imendikwa “Kila pando  asilolipanda Baba wa Mbinguni litang’olewa” nami  naamuru kwa Jina la Yesu, kila pando la magonjwa, pando la umaskini,  pando la matatizo na mikosi lazima yatoke kwa Jina la Yesu.  Gideoni alipoliona tatizo  ni nyumba ya miungu aliibomoa, na watu walipomfuata baba yake mzazi ili  kutaka kumwajibisha, Yoashi babaye aliwajibu yafuatayo: WAAAMUZI  6:31…[Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe hivi asubuhi; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake..]…. Kama shetani  anaweza kujitetea na ajitetee. Leo tutabomoa madhabahu za kishetani na vibanda alivyojenga kuziba mafanikio  yetu na kama shetani  anaweza kujitetea na ajitetee.
UKIRI
Kila wazo la kishetani lililokaa kunionea leo  nalishambulia kwa Jina la Yesu. Shetani aachia maisha yangu kwa ina la Yesu.  Wote wananifuatilia na mawazo ya giza leo nawashambulia kwa Jina la Yesu. Amen

Kuokoka kwa kumpokea Yesu Kristo maishani mwako kuwa Bwana na Mwokozi  wako ni hatua ya kwanza ili kuweza kupokea kibali cha Bwana na kuwashinda adui zako wote ambao leo  tunawashughulikia.
 

Comments