KUUSHINDA ULIMWENGU.

Na Mchungaji Bryson Mabena, Ufufuo na uzima.

Utangulizi: Wale wanaokuonea na kuyasumbua maisha yako  huitwa “watu wa ulimwengu huu”. Ukumbuke kuwa huu ulimwengu upo chini ya yule adui yetu shetani. GALATIA 1:4…[ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu.]… Je, dunia ndiyo mbaya au wakaao duniani ndio wabaya? Je, Mungu aliumba kitu au vitu vibovu. Mungu ndiye aliiumba hii dunia. MWANZO 1:1-31, uumbaji wa Mungu unaonekana,  na kila alichokiumba  Mungu alisema ni kizuri, tena kinachopendeza.  Kwa kawaida kitu kizuri kinachopendeza hata siku moja siwezi kukiita kibovu. Mungu aliiacha dunia ikiwa inapendeza. Kipo kitu kilichotokea na kuifanya dunia iwe mbovu.
1YOHANA 1:4-5…[Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu. 5 Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu?]… Mtu aliyeushinda ulimwengu ni yule aliyemkiri Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake.
Imeandikwa 1YOHANA 5:19…[Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu.]… Hapa tunagundua kuwa dunia hii inatawaliwa na shetani. Na mimi ambaye nimeokoka, sipo upande wa hii dunia. Kama dunia haipo upande wangu, ina maana  ya kwamba shetani anaweza kuwatumia wale wote wasiomwamini Yesu (ambao wapo duniani) ili kunipinga.  Ndiyo maana Yesu Kristo aliniokoa mimi na wewe kama mbegu ya kuzitikisa falme za hii dunia ili zote ziwe falme za mwanakondoo. Watu wa ulimwengu wanakupinga lakini Baba wa mbinguni alikujua na kukuandaa ili kuushinda ulimwengu na hiyo balaa iliyokuja mbele zako. Sikuzaliwa chini ya utumwa, bali nina kazi maalumu kwa ajili ya ushindi niliyopewa na Baba wa Mbinguni. Huyo adui anayekupinga hana kitu kwako, kwa sababu unayo mamlaka ya ushindi. Kabla ya vita yako, mshindi ameshatangazwa. Tatizo ni kuwa adui anayakamata mawazo na akili zako ili ujione kuwa uwezo wako ni huo kumbe siyo. Mamlaka na uwezo na nguvu ulizo nazo vyote ni vya Mungu, na kama Mungu hawezi na mimi siwezi. Ila kama Mungu anaweza na mimi naweza. Ndiyo maaana imeandikwa “waliozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu”. Yawezekana siyo leo au kesho lakini ninachokijua ni kuwa sitaondoka hapa kama aliyeshindwa bali kama mshindi.
Biblia inasema ujapopita katika bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya. Kwa kuangalia kwa macho unaona mauti, lakini mbele za Baba anona hayo mapito kama ‘uvuli wa mauti’.  Acha kulia na kusema maisha ni magumu. Kumbuka kuwa kati ya nuru na giza, chenye nguvu zaidi ya kingine ni nuru kwa sababu mahali penye giza ikiwekwa nuru giza hukimbia.  Kwa kuwa wewe umeokoka, ujue kuwa wewe ni nuru na wote walio gizani lazima wakimbie mbele zako. MATHAYO 5:13-16…[Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. 14 Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. 15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. 16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.]… Wanaokupinga wakikuangalia wanaona kitu kinang’aa na ndipo hutafuta namna ya kuifunika nuru yako. Wasichokijua ni kuwa hiyo nuru yako haijatoka kwa wanadamu. Giza haliwezi  kuiondoa nuru mahali popote. Fahamu kuwa waganga wa kienyeji ni giza. Ukiona giza linakufuatia ujue kuwa kuna mahali  ambapo taa yako imezimika. Inapaswa kuiwasha taa yako ili  kuifukuza giza mbele yako.
Kiu ya shetani ni kunizua nisitoke. Hata hivyo, sikuja kupata mafanikio kupitia watu ila mafanikio yangu yanatoka kwa Baba wa Mbinguni. Mtu unayemuona leo ni wa leo, ila usichokiona ni kesho yake mtu huyu.
Fahamu kuwa kazi ya shetani ni kukupinga na kukufunga. Imeandikwa  katika ISAYA 14:17…[Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao? ]… Mpango wa shetani na mawakala wake ni kuwafunga watu wasiweze kwenda kwenye ushindi wao. Hupaswi kuwaza juu ya mamlaka aliyo nayo wakala wa shetani (adui). Mamlaka uliyo nayo ni makubwa kuliko ya adui zako. Haipaswi kukaa ndani ya kanisa ambalo watu wake wanamtegemea tu Mchungaji wao kuwaombea kila wakati. Unapaswa kukaa kanisani ambapo unapata maarifa ya kuomba mwenyewe,  kwa sababu  hata huyo mchungaji wako anakuwa na mambo yake binafsi ya kuombea, na hawezi kuanza kukuombea wewe kabla ya yale ya kwake.
Andiko mojawapo la kukutia nguvu lipo katika YOHANA 14:30…[Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.]…. Ina maana kwamba, huyo  mkuu wa ulimwengu hata kwako hana uwezo katika maisha yako. Kushindana watashindana nami, lakini hawatanishinda. Kuwepo katikati ya mapambano siyo tatizo, kwa sababu hata mimi ni mmojawapo wa wanaopigana. Vita vikiwa mbele yako havipo kwa ajili ya kukuangamiza,  bali kwa ajili ya  wewe kushinda.
Msogelee  adui wa maisha yako,  ndoa yako, biashara yako n.k. siyo kwa sababu nyingine bali ni kwa Jina la Bwana wa majeshi. Usihesabu matatizo uliyo nayo bali hesabu ushindi ulio nao ndani  ya  Kristo. Imeandikwa “mateso ya mwenye haki ni mengi lakini Bwana humponuya nayo yote”.
MHUBIRI 9:11…[Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote.]… Kuna wakati wa kila jambo ndani ya maisha yangu. Maisha yako  hayatakaa katika ugumu wakati wote.  Ndege akipita juu  ya kichwa changu siyo tatizo lakini tatizo ni huyo ndege kutengeneza kiota chake juu ya kichwa changu.  Ukiona mambo yanazidi kuwa magumu, jua kuwa ushindi nao unakaribia.
Wanaokupiga vita wanakusaidia kwenda kutawala. Yuda Iskariote kwa kumuuza Yesu Kristo alisababisha Yesu afe na baada ya siku ya tatu YESU akafufuka na kupewa JINA LIPITALO MAJINA YOTE. Siyo wakati wa kumlaumu Penina, kwa sababu bila Penina hakuna Samweli. Hanna alimimina maombi yake mbele za Bwana kwa sababu ya Penina kumchokoza. Eli  hakuwahi kumuona Hanna akiomboleza,  lakini baada ya kuinuka Penina ndiposa Eli akakutana na Hanna na kumwambia “Bwana na akupatie haja ya moyo wako”. Nipo kanisani kwa sababu ya Penina wa maisha yangu. Ni saa ya kukutana na Eli na kumwambia Eli shida ya maisha yako.
Je ,umempokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako? Kama upo na hujaokoka,  ni saa yako  kuanza upya kwa kuzaliwa upya . 

Comments