MGAWO WA KISHETANI


Na Pastor Bryson Lema, Ufufuo na uzima  Morogoro.
Utangulizi: Upo "mgawo wa kishetani" kwenye maisha ya wanadamu. Katika Kitabu cha MIKA 2:4 imeandikwa hivi:…[Siku hiyo watatunga mithali juu yenu, na kuomboleza kwa maombolezo ya huzuni nyingi, na kusema,  Sisi tumeangamizwa kabisa;  Yeye analibadili fungu la watu wangu;  Jinsi anavyoniondolea hilo! Awagawia waasi mashamba yetu.]…. Jambo la muhimu  katika andiko  hili  ni kuwa kuna mgawo, tena wa mashamba. Na kama kuna mgawo, ujue yupo  mwenye kugawa. Swali la  kujiuliza hapa ni kuwa,  kwa nini mashamba haya yagawiwe kwa waasi? Maana yake, mali zangu,  vitu vyangu vimegawiwa kwa shetani, kwa sababu Biblia inamuonesha shetani kuwa aliasi kule mbinguni. Na kwa hiyo sasa, huyu  shetani amevikamata vitu vyangu,  akavifanya  kama vyake.
Ukisoma YEREMIA 1:5 imeandikwa:…[Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.]… maana yake,  kabla ya Yeremia kuzaliwa,  alishagawiwa mgawo wake unaomhusu.  Alitakiwa  aende katika mafanikio yake kwa sababu tayari anao mgawo wake kutoka kwa muumba wake, yaani Mungu (Jehovah).
Shetani alichokifanya ni kutuibia.  Biblia inasema katika YOHANA 10:10 [Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.]. Ndani ya maisha yako,vipo vitu unavyopitia visivyo kuwa vya kwako. Maana yake,  una vitu ambavyo unaviona kama vyako lakini kumbe ni  mgawo wa kishetani”. Walipokaa mashetani na mawakala wao, walikutengenezea ugonjwa,  na ambao unakaa nao kwa muda mrefu sasa, na hata imefikia wakati umeanza kuuita huo ugonjwa kuwa ni ‘ugonjwa wangu’.  Ayubu  vivyo hivyo, alipata magonjwa na adha mbalimbali, lakini vyote hivi hakugawiwa na Bwana, bali ulikuwa mgawo wa kishetani. Kosa ambalo wengi wameendelea kulikiri leo hii ni kuungana na maneno ya Ayubu kusema ‘Bwana ametoa, na Bwana ametwaa”. Siyo kweli  kwamba Bwana anapokupa anakuja mara ya pili  kutwaa kile alichokupatia.  Ingekuwa hivyo basi Ibrahimu alipoambiwa amtoe sadaka mwanae pekee Isaka,  basi siku ile ile Isaka angechinjwa. Ili kudhihirisha hili, Bwana hakuruhusu Isaka afe, na badala yake alimuepusha na kifo kile cha kutolewa sadaka na Ibrahimu baba yake.
Upo mgawo wa kishetani unaong’ang’ania maisha yako. Wakati mwingine unajikuta kuna mambo unashindwa kuyaacha maishani mwako kwa sababu tayari huo ni mgawo. Imeandikwa EZEKIELI 23:7…[ Akawagawia mambo yake ya kikahaba, watu wateule wa Ashuru, wote pia; akajitia unajisi kwa vinyago vyote vya kila mmoja wa hao aliowapenda.]… Unapoupata mgawo, huo mgawo unakuwa sehemu ya maisha yako. Ndiyo maana unakuta maisha ya mtu yanakuwa magumu kwa sababu kuna mgawo wa kishetani ndani ya  maisha yake, na siku ya leo ni maalumu kwa ajili ya kumrudishia  shetani migawo yake kwa Jina la Yesu.
Mwanadamu mara  zote anakuwa na Tabia ya kukataa mambo mapya.  Hata hivyo, baada ya mambo mapya kuanza na kuyazoea, mwanadamu husahau kuwa mwanzoni  hakuwa anafurahia hali hiyo. Mfano ni pale ambapo mtoto wakati wa kuzaliwa, hulia kwa sababu alishazoea maisha ya kukaa kwenye tumbo la mama yake,  na hivyo kukaa duniani nje ya hilo tumbo  hataki. Hata hivyo, baada ya mtoto huyu  kuzaliwa na kuzoea dunia, hapendi tena kutoka humu duniani (kufa),  kwa sababu ameshazoea maisha ya kuwa humu duniani. Ndivyo ilivyo hata kwa baadhi ya watu wanapopata matatizo. Mwanzoni mtu huyakataa matatizo/magonjwa/ au mateso fulani, na huwa tayari kuyakemea, lakini  matatizo haya yakiendelea kukaa kwa miaka miwili  na kuendelea, mtu huyazoea matatizo hayo na kuyafanya kuwa sehemu ya maisha ya huyo mtu.
Yesu Kristo alipokuwa anakutana na mgonjwa, kabla  ya kumponya alikuwa  akimuuliza “Je, unaamini?”. Lengo la swali kama hili ni kutaka kufahamu, je mtu huyu anao utayari kwa kupokea uponyaji? Inabidi awepo mtu  aliye tayari kubadilika. Kwa Yesu 'hakuna kujaribu’ bali kuna kudhamiria kupokea sawa sawa na imani  yako kwake. Kama unataka kumiliki ujiandae kuua visivyotakiwa kuwepo. Kwenye  Baraka zako, yupo Goliath anayekuzuia. Daudi alipomuoana Goliath, alisema “huyu  ni nani anayetukana majeshi ya Mungu aliye hai? Wakati umewadia ambapo Lazima kizazi cha Daudi kiamke katika taifa letu kwa Jina la Yesu.  Huu siyo  wakati  tena wa kuongozwa  na viongozi wanaotumia nguvu za giza. Siyo wakati tena wa kuongozwa na viongozi wanaoenda kwa waganga wa kienyeji ili kupata nguvu au uongozi. Je, hayupo Mungu  katika taifa hili hata watu hawa wazitegemee nguvu za giza?
Wapo waliokuibia urithi wako wakakugawia mateso na magonjwa,  na leo hii ni wakati wako wa kupambana ili  kurudia kilicho chako. Mtu anayeomba na asiyeomba ni watu wawili tofauti. Anayeacha maombi, humpa nafasi shetani kukaa ndani ya moyo wake. Ndiyo maana migawo ya kishetani inaendelea kuwepo kwa sababu mtu  apewaye  huo mgawo hana nguvu ya kuikaataa.

Imeandikwa 2NYAKATI 32:8…[kwake upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo Bwana, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.]…. Mgawo wa kishetani una mkono wa mwili, mkono wa kibinadamu. Leo kataa kuwa chini ya mgawo wa kishetani  ambao adui amekugawia kwa Jina la Bwana. Upo  mkono wa Bwana kukusaidia ili kuangamiza kila  mgawo  wa kishetani maishani  mwako.  Kumbuka kuwa ndani mwako kuna mkono wa Bwana wa kukusaidia, kama Hezekiah alivyosema, kwa Jina la Yesu.
Kila "mgawo wa kishetani" utaweza tu kuuangamiza endapo umempokwa Yesu Kristo  maishani  mwako. Endapo mtu hujaokoka, chukua hatua ya kumpokea Yesu Kristo  maishani mwako, ili uweze kuiangamiza migawo yote ya kishetani  maishani mwako.
UKIRI
Kila  mgawo wa kishetani  uteketee kwa Jina la Yesu.  Leo naenda kinyume na kila mgawo wa kishetani maishani mwangu. Kila  uzao wa giza leo ninauteketeza kwa Jina la Yesu. Ninaikataa migawo yote ya mashetani. Leo ninakataa kupatana na wachawi. Achieni maisha yangu kwa Jina laYesu. Amen

Comments