MTUMAINI BWANA KATIKA MAMBO YAKO YOTE NAWE UTABARIKIWA


Na; Hosea G. Paul. Yeremia. 17:7 “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana ambaye Bwana na tumaini lake”
Shalom watu wa Mungu!
Nabii Yeremia anayanena maneno ya Mungu akisema amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana. Biblia inaposema kumtegemea ni sambamba na kusema kumtumaini. Ni ile hali ya kujishusha kiasi cha kutoweza kufanya jambo lolote lile ila kwa uweza na nguvu za Mungu.

Paulo mtume wa Yesu; yeye anawaambia watu wa mji wa Filipi kuwa anayaweza mambo yote katika yeye amtiaye nguvu (Wafilipi 4:13 SUV). Katika kuwaza au fikra; tunapashwa kumtegemea Bwana. Katika kufanya jambo lolote lile tunapaswa kumtegemea Bwana. Na hata katika mipango yetu yote tunapashwa kumtegemea Bwana. Sijiamini mwenyewe; bali najiamini sana, wala siogopi lolote kwasababu nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Kumbe sitegemei akili zangu mwenyewe wala uweza wangu binafsi wala nini ila yupo ninayemtegemea; ambaye ananitia nguvu. Akinitia nguvu mimi ninaweza yote.
Zab.125:1-2; “Wamtumainio Bwana ni kama mlima wa Sayuni; ambao hautatikisika, wakaa milele. Kama milima inavyouzunguka Yerusalemu, ndivyo BWANA anavyowazunguka watu wake; Tangu sasa na hata milele”. Tunazidi kuona maandiko yanavyosema kuhusu kumtumaini na kumtegemea Bwana. Wamtumainio Bwana hawataweza kutikiswa na jambo lolote lile. Katika maisha halisi ya wanadamu; changamoto ni sehemu ya maisha. Yumkini kwa ukubwa wowote wa changamoto; hakuna itakayomweza mtu anayemtegemea Bwana. Kama yumkini unazimia katika changamoto basi biblia inasema nguvu yako ni ndogo (Mithali 24:10 SUV).
Wapendwa; nabii Isaya anasema hivi; Je! Mwanamke aweza kumsahau mwana wa tumbo lake, asimhurumie? Anasema hawa wanaweza. Isaya 49:15-16 Tunashuhudia na kusikia kila kukicha; wamama wakiwatupa watoto wao wachanga katika majalala na hata vyooni. Pia dada zetu wanatoa mimba hovyo. Hawana huruma hata kidogo hata hawakumbuki uchungu wote wa uzazi.
Mungu anasema kwa kutumia kinywa cha Isaya nabii kuwa MIMI SINTAKUSAHAU WEWE. Nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu na kuta zako ziko mbele zangu daima. Mungu anawatambua walio wake; na hao ndio anaowataja katika Timotheo na Mambo ya Nyakati. Hao ni wake kwani wanamtumaini na kumtegemea yeye. 2 Mambo ya Nyakati 7:14 inasema “ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu…….” Asema Bwana pia katika 2 Timotheo 2:19 inasema “Bwana awajua walio wake……”. Biblia hii inasema tena katika kitabu Zaburi 137:5 kuwa Mungu hatausahau mji wa Yerusalemu kama asivyoweza kuusahau mkono wake wa kuime.
Point; Ukimtegemea na kumtumaini Mungu hatakusahau wala hatakuacha kamwe bali atakubariki sana.
Yer.17:5; “Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana”.Awali tumeona kumtegemea Bwana na sasa tunaona yule ambaye anamtegemea mwanadamu.Unaweza ukawa unamtegemea mwanadamu katika namna mbili;
1. Kumtegemea mwanadamu mwingine kwa chochote.
2. Kutegemea akili zako mwenyewe.

Katika tafsiri ya sheria ya kimataifa ya kosa la uuaji; mtu atahukumiwa kutenda kosa la mauji kama aidha amemwua mwenzake au amekuwa katika harakati za kujiua yeye mwenyewe. Yule mtu anayesalimika wakati amejinyonga kwa aidha kamba ama kitu kingine atahukumiwa kwa kosa la mauaji. Chukua…. Ahaa! Kumbe kuzitegemea akili zako mwenyewe ni sawa na kumtegemea mwanadamu na siyo Mungu.
Mithali .3:5 inasema mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee “akili zako mwenyewe”. Neno la Mungu linatutambulisha umuhimu wa kumtegemea Mungu moja kwa moja bila kujaribu kutegemea kingine. Inafika sehemu watu wa Mungu tunategemea tupate nafasi kwa watu tunaowaita wenye uwezo??? Ati anazo zakutosha…. Ukiumwa unao uhakika wa kupata matibabu kwani unaowategemea wanazo fedha… Ukipata tatizo wao watakusaidia kwani uwezo wanao na mamlaka ya utawala wameshika wao. Wapendwa nawashangaa wale ambao hata katika karne hii wanaenda tu kwa waganga wa kienyeji kupata chanjo ya kinga na kubebeshwa mauchafu eti matunguri…. Nawashangaa sana.
Biblia inasema Bwana asipoulinda mji waulindao wakesha bure… Linganisha na walinzi wa mwili wa Yesu kaburini; alipofufuka walimwona???. Usipomtumaini Bwana jitihada zako na msaada unaoutegemea kwao si kitu. Ukimtegemea Bwana; yeye anaishi milele ila ukimtegemea mwanadamu ipo siku atakufa ama asipokufa atafilisika ama ataachia ngazi.
Mungu awabariki;
E-mail: hospau2808@gmail.com
WhatsApp: +255 788 574 220.

Comments