NGUVU YA KIAPO

Na Mchungaji Bryson Lema, Ufufuo na uzima Morogoro.
 

Utangulizi: Hivi kiapo ni kitu gani? Na kwa nini watu wanaapa? Kwa muhtasari, kama kiapo hakina mahusiano yoyote na Mungu au na wanadamu, hakuna ambaye angekifanya. Mungu naye huapa, na wanadamu vivyo hivyo. Imeandikwa katika EBRANIA 6:16-17…[Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na kwao ukomo wa mashindano yote ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha. 17 Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonyesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati;]….Maana yake,  mtu  aapo anaweka rehani uhai wake. Ni kuyaweka maisha yako  katika kile unachokiapia. Kumbuka kuwa uhai wa mwanadamu ndicho kitu cha thamani kuliko  vyote alivyo navyo. Ndiyo kusema kwamba, endapo  mwanadamu hana uhai ni sawa na ‘takataka’ tu. Tunasema hivyo kwa sababu ukeshachimbia shimo kitu na kukiweka huko, maana yake kile ulichokiweka huko ni takataka tu.
Kiapo ni njia ya mwisho kuliko zote aitumiayo mwanadamu kuondoa mabishano. Mtu umkutapo anaapa, huapa kwa jina la wazazi wake au jina la miungu  yake. Kwa nini iwe hivyo: ni kwa sababu wazazi ndio walio wakuu kuliko wote kwa maisha ya huyo mtu. Endapo mtu ataapa kwa jina la Mungu, nayo itategemea,  je huyu mtu ameapa kwa Mungu wa herufi ndogo (mungu, ambaye pia ni  shetani) au MUNGU wa Herufi  Kubwa (yaani Jehovah).
Katika ulimwengu wa roho kiapo ni kitu cha thmani sana. Unaposema ninaapa, maana yake unajiweka kwenye nafasi ya hicho kitu. Tunaona kuwa Mtu anapodhamiria kuapa anayaweka maisha yake rehani. Mtu afanyapo kiapo,  atahakikisha kuwa maisha yake  yule aliyemdhamiria katika hicho kiapo hayatakaa sawa hata kidogo.
Imeandikwa hivi katika MARKO 5:2-7 ..[ Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; 3 makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; 4 kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunjavunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. 5 Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe. 6 Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; 7 akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese.]…. Ukisoma maandiko, Huyo ndiyo pepo pekee aliyehojiana na Yesu Kristo. Pia ndiye pepo pekee ambaye Yesu Kristo alimuuliza jina lake ni nani? Kilichomfanya atoe ruhusa ya hao pepo kuwaingia wale nguruwe ni kwa sababu alimwapisha Yesu Kristo kwa Mungu. Pepo hili lilijua ‘nguvu ya kiapo’. Washirikiana nao wanaijua hii nguvu ya kiapo, na ndiyo maana huifanya afya ya mtu isiwe nzuri, au maisha yake kwa sababu kuna  watu walioweka kiapo mahali  fulani. Kumbuka kuwa, kiapo kinapofanywa,  walinzi wa kiapo  nao huwekwa ili kusimamia hicho kiapo.
Kafara ya kiapo hutofautiana kulingana na ukubwa wa kile kilichotolewa.  Kafara ni kama sadaka ambayo hchinjwa (kuku,  kondooo,mbuzi, ng’ombe au ikizidi sana mwanadamu). Damu ya hizi kafara zikiwamwagika, huongea zikiwa ardhini. Ndiyo maana Biblia inasema ‘Damu ya Yesu hunena mema juu yetu’. Hata Pilato alipokuwa akimhukumu Yesu Kristo, alinawa mikono yake na kusema ‘Damu ya mtu huyu hainihusu’.  Leo hii tupo huru kutokana na kafara ya Kalvari ya Damu ya Yesu Krsito. Endapo hii Damu  ya Yesu hadi leo inanena mema juu yetu, je, hizi kafara za waganga wa kienyeji na wachawi wanazotoa kwa ajili  yako zinanena kitu gani?
Wakati mwingine maisha yetu hayaendi vizuri kwa sababu ya kukamatwa na viapo. JOSHUA 6:26…[Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za Bwana mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo.]…. Joshua aliweka kiapo hiki kwa Jina la Bwana, Mungu aliye mkuu kuliko wote. Ni kitu gani  kilitokea kwa wale walioinuka kuujenga huu ukuta baada ya muda mrefu sana kupita tokea kuwekwa kwa hiki kiapo? Imeandikwa katika 1WAFALME 16:34 ….[Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza   na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa Yoshua   mwana wa Nuni.]… Kile kiapo  kilikuwa hai, ingawa wale waliokuwepo wakati Joshua anaapisha wale watu walikuwa walishakufa. Kiapo chaweza kuwa hai, na kufuatilia maisha ya mtu wakati wowote ule. Katika familia zetu za Kiafrika, mambo mengi hayaendi kwa sababu vipo viapo  ambavyo mababu zetu walivifanya, na usipokuwa makini  kujitoa humo, utaendelea na aina hiyo  ya maisha magumu.
Zipo  koo ambazo mapatano yalifanyika zamani  sana bila wewe kujua. Inawezekana kweli hujawahi kwenda kwa waganga wa  kienyeji, lakini unajua je kama babu au bibi yako  hakuwahi  kwenda kwa hao waganga wa kienyeji? Pengine babu yako  aliweka mapatano hayo enzi hizo na waganga wa kienyeji,  na kwa sababu hiyo familia yako inaendelea kufuatiliwa. Chale zifanywazo na waganga wa kienyeji  ni mojawapo ya aina za viapo. Ni kwa sababu damu ni uhai (kwa mujibu wa Biblia). Kila damu ina vinasaba (DNA), na pale waganga wakizichanganya, hufanya watu wa aina hii kupitia maisha yasiyokuwa yao.
Katika familia zetu kuna uwezekano wa mmoja wapo kuunganisha hiyo familia na kuzimu. Katika wale 12 wanafanuzi  wa Yesu Kristo, mmojawao alikuwa ni  shetani. Watu  wanaweza kuweka mapatano  na kuzimu. Pengine afanyaye hayo yote atakuwa tayari kukusaidia kwa kila jambo, ili usimgundue. Miili  yetu hii ni sawa na  majumba tu. Kumbuka ukiwa na nyumba unaweza kuwa ndani ya hiyo nyumba au ukawa nje ya hiyo nyumba. Katika ulimwengu tuliopo sasa,  usiamini mwanadamu wa nje, ila muhimu ni ile roho ndani mwake, kwa sababu mtu ni roho na siyo  mwili.
Kipo kiapo ambacho mababu zangu au baba yangu alikifanya,  leo ni saa ya kuvivunja hivyo viapo vyao kwa Jina la Yesu. Sikuja hapa duniani hivi hivi, na hata mimi ninacho kiapo changu.  Imeandikwa katika 1WAFALME 2:43…[Mbona basi hukukishika kiapo cha Bwana, na amri niliyokuagiza?]… Kumbe basi kipo KIAPO CHA BWANA. Kama wao walienda kwa mizimu na kuapa, hata mimi ninao uwezo wa kuweka kiapo na Bwana, kwa sababu kiapo huondoa mabishano. Ni wakati wa kuondoa ubishani. Kiapo cha Bwana kitakomesha kila balaa ndani ya maisha yangu. Kumbuka kuwa, Mungu wetu anapoapa huapa kwa nafsi yake  mwenyewe. Siyo kama miungu ya dini zingine ambayo huapa kwa vitu vilivyoumbwa.
Uonapo dada yako ana matatizo yanayofanana na wewe, jiulize kwa nini  iwe hivyo wakati ninyi wawili mpo tofauti? Unapomuona kaka yako ana matatizo yanayofanana na wewe, jiulize kwa nini  iwe hivyo wakati ninyi wawili mpo tofauti? Haya yote yametokea kwa sababu kuna kiapo mahali fulani na wapo waliokaa kwenye hico kikao cha kiapo na kusababisha hayo uyaonayo yaendele kutokea. Ni  saa ya kukata kila  mnyororo wa kiapo kwenye familia yako. Ni saa ya kutoa kiapo na kuweka kiapo.

WAEBRANIA 7:20….[  Na kwa kuwa haikuwa pasipo kiapo,]…. Hakuna kitu kilichofanyika pasipo  kiapo. Na ndiyo maana ili Mungu atende jambo, aliapa. Maana yake, mambo yangu pia hayafanikiwi kwa sababu hakuna kiapo.  Endapo hakuna kiapo, maisha yako yanakuwa na matatizo. Ndiyo maana hata shetani alishindwa kumgusa Ayubu kwa sababu kati ya Mungu  na Ayubu palikuwepo na KIAPO. Cha wewe kufanya ni kuamua yafuatayo:-  Sina msamaha na mchawi anayeniwangia usiku. Biblia inasema, “usimwache mwanamke mchawi kuishi”.  Kumbuka  Mungu huyuhuyu  ni Yule aliyesema “usiue”,  lakini kwa habari  ya wachawi na washirikina Mungu ameruhusu wasiishi, maana yake wauawe.
Israeli waliongozwa usiku na mchana, bila hata adui mmoja kuwasogelea wakati wanaenda zao nchi ya Ahadi. Lile wingu lililowaongoza mchana, kwa sababu  ya kile  kiapo cha  Mungu  na Ibrahimu  kwamba uzao  wake atawapa hiyo nchi. Hata kwa sasa, kinachowafanya Israeli wakae salama ni kwa sababu ya kile kiapo walichokifanya, kwa kusema “Damu yake  (Yesu) iwe juu yetu na juu ya kizazi chetu”. Ingawa hawakujua wasemacho, hata sasa Damu ya Yesu inazidi kunena mema juu  yao. Daudi alikosea kwa kuwahesabu Israeli yote,  na adhabu ambayo Mungu alimpatia achague mojawapo ya hizi zilivyoandikwa katika 2SAMWELI 24:13-14 … [ Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.14 Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.]… Maana yake ni kuwa, nchi yote ya Israeli ilikuwa iadhibiwe kutokana na kosa la Daudi kama  kiongozi wao.  Endapo vipo “Viapo vya Kishetani” vilivyowekwa na viongozi wa serikali yetu leo lazima tuvivunje kwa Jina la Yesu. Viapo vya kishetani vilivyowekwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza, au Awamu ya Pili au Awamu ya Tatu au ya Nne lazima tuvivunje kwa Jina la Yesu.  
Je, umemwamini  Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako? Huwezi kuweka kiapo na Mungu ambaye hujapatana naye. Unapoamua kuokoka unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuvunja viapo vyote vivlvyowekwa kinyume nawe, na utaweza kuweka kiapo na Bwana Mungu, aliye Mungu Mkuu  kuliko miungu  yote, kwa Jina la Yesu.
UKIRI
Kuanzia sasa kila kiapo cha giza niachie, wote walioshika afya yangu, au maisha yangu  leo nawasambaratisha kwa Jina la Yesu. Viapo vyote vilivyofanyawa juu ya maisha yangu naviharibu  kwa Damu ya Mwanakondoo. Amen

  

Comments