NITAIONEAJE HAYA INJILI YA KRISTO WAKATI INJILI NI UWEZO WA MUNGU ULETAO WOKOVU KWA KILA AAMINIYE?

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la kututengeneza ili tuwe tayari kwa ufalme wa MUNGU wa uzima wa milele.
Leo tunajifunza 
''Utaioneaje haya injili ya KRISTO wakati injili ni uweza wa MUNGU uletao wokovu Kwa kila aaminie?''
Injili ya kweli ipo moja tu ambayo ni injili ya BWANA wetu YESU KRISTO. Hiyo ndio injili ambayo haitakiwi tuionee haya maana ni uweza wa MUNGU uletao Wokovu kwa kila aaminie na kumpokea YESU KRISTO kisha kuanza kuyaishi maisha safi ya wokovu.
Warumi 1:16-20 '' Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa MUNGU uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. Kwa maana haki ya MUNGU inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani. Kwa maana ghadhabu ya MUNGU imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu. Kwa kuwa mambo ya MUNGU yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana MUNGU aliwadhihirishia. Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru;'' 
-Je kuna sababu yeyote ya kuionea haya injili ya KRISTO?. Ukweli ni kwamba hakuna sababu hata moja ya kuionea haya injili ya KRISTO, kwa maana injili ya KRISTO ni uweza wa MUNGU uletao wokovu kwa kila aaminie. Ghadhabu ya MUNGU ipo ndio maana injili ya KRISTO ilikuja ili watu wasiende tena upotevuni.
Naipenda injili maana ni uwezo wa MUNGU uletao Wokovu.
Injili maana yake ni habari njema za ufalme wa MUNGU na Neno wokovu maana yake  ni hali ya kusalimika na adhabu ya Mwenyezi MUNGU, ndivyo kamusi ya kiswahili sanifu inavyosema. Ukiangalia maneno hayo mawili yaani INJILI na WOKOVU yanategemeana sana.Injili lazima izae Wokovu. Ukiipokea injili ya kweli ya BWANA YESU harafu isizae Wokovu kwako hiyo inamaana umeipinga kweli ya MUNGU kwa sababu zako mwenyewe ambazo hazitakusaidia. BWANA YESU alilifafanua jambo hilo kama ifuatavyo 

Mathayo 13: 3-9 ''Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda. Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina;  na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. Mwenye masikio na asikie.'' 

-Kumbe mbegu ni  Injili, ni Neno la MUNGU linalohubiriwa kwa Mtu mfano kama unavyohubiriwa wewe leo kupitia ujumbe huu. Mbegu ni neno la MUNGU ambalo hupandwa katika shamba liitwalo moyo wako. mbegu ni injili njema inayohubiriwa kwako lakini kama injili hiyo haitazaa wokovu maana yake wewe una tatizo. na matatizo hayo BWANA YESU aliyafafanua kama ifuatavyo.

Mathayo 13:19-23 '' Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia. Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa.
Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai. Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini.'' 


. Je! Neno la MUNGU linalopandwa kila siku katika moyo wako limezaa Wokovu kwako?
Kama injili imezaa Wokovu kwako nakupa hongera sana maana umeipokea kweli ya MUNGU na kweli hiyo ya MUNGU inaitwa habari njema za ufalme wa MUNGU, Na hizo habari njema za ufalme wa MUNGU huzaa Wokovu ambao maana yake  ni hali ya kusalimika na adhabu ya Mwenyezi MUNGU. na maana nyingine kwa mjibu wa kamusi ya kiswahili sanifu Wokovu Maana yake ni KUOKOKA. Hivyo injili unayohubiriwa kila siku na watumishi waaminifu wa KRISTO ina maana moja tu ya kukuleta kwenye WOKOVU.
 Kumbe ndio maana hakuna haja ya kuionea haya injili maana injili ni uweza wa MUNGU uletao wokovu kwa kila aaminie. Kama hutaiamini na kuipokea injili ya KRISTO Biblia inasema neno hili kwako kwamba 
''Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake KRISTO aliye sura yake MUNGU. Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali KRISTO YESU ya kuwa ni BWANA; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya YESU. Kwa kuwa MUNGU, aliyesema, Nuru itang'aa toka gizani, ndiye aliyeng'aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa MUNGU katika uso wa YESU KRISTO.-2 Kor 4:3-6 ''

-Kusitirika maana yake kujificha au kutoonekana hivyo kama injili ya KRISTO imejificha au haionekani kama ni kitu cha thamani sana basi ni kwa hao tu wanaopotea, ambao shetani amewapofusha macho yao ya rohoni hata hawaoni. shetani anaitwa mungu wa dunia hii. hapo naomba ujifunze kati ya MUNGU/Mungu na mungu. mungu inayoanza na herufi ndogo inamaanishia shetani na MUNGU ni YAHWEH au YEHOVA.
MUNGU wa kweli ni mmoja tu na anapatikana katika KRISTO YESU  maana KRISTO ndiye aliyemfunua MUNGU kwetu wanadamu wote. 
Yohana 1:18 ''  Hakuna mtu aliyemwona MUNGU wakati wo wote; MUNGU Mwana pekee aliye katika kifua cha BABA, huyu ndiye aliyemfunua. '' 

-Ndio maana binafsi huwa siwashangai wale ndugu ambao humkataa KRISTO na kujidai kwamba mungu ni mmoja tu. ni kweli mungu ni mmoja tu  lakini pia MUNGU ni mmoja vilevile, hivyo usijidai kwamba uko upande wa mungu mmoja huku humtaki MUNGU wa kweli aliye katika KRISTO YESU pekee.
 kama uko upande wa mungu mmoja uko sahihi kabisa maana Biblia haijaandika popote kwamba kuna shetani wawili bali ni mmoja tu, na kama huyo ndio mungu wako basi hakika una haki ya kutangaza kwamba mungu ni mmoja tu na hana kiumbe wa kufanana nae, uko sahihi maana hakuna hata mmoja anayetamani kufanana na shetani aliye mungu mmoja tu tena ni mungu wa dunia tu na si zaidi ya hapo. Lakini kwa ndugu yule anayeitaka kweli ya MUNGU basi ni lazima aipokee injili ya KRISTO ambayo huzaa wokovu kwa kila aaminiye.
Hatuna haja ya kuionea haya injili ya KRISTO maana ni uweza wa MUNGU uletao wokovu kwa kila aaminie. MUNGU BABA wa mbinguni mara nyingi sana amewaita watumishi wake ili watuletee injili yake ambayo kama tukiishika itazaa Uzima wa milele kwetu.
2 Kor 9:13-15 ''  kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo, wanamtukuza MUNGU kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya KRISTO, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote. Nao wenyewe, wakiomba dua kwa ajili yenu, wawaonea shauku kwa sababu ya neema ya MUNGU iliyozidi sana ndani yenu. MUNGU ashukuriwe kwa sababu ya kipawa chake, tusichoweza kukisifu kama ipasavyo. '' 

=Injili ya KRISTO inatutaka  tufanye yafuatayo.

1.   Tumpokee YESU kama BWANA na MWOKOZI wa maisha yetu(Mathayo 11:28, Matendo 4:12, Yohana 14:6, Warumi 10:9-10)

2.   Tutubu na kuacha dhambi(Matendo 3:19, Mathayo 3:2, 2 Petro 3:9, Luka 5:32)

3.   Tuishi maisha matakatifu (  Wakolosai 1:21-22,  Waebrania 12:14,  Yakobo 3:17, Mithali 28:23) 

4.   Tuuvue utu wa kale na kuvaa mpya ( Wakolosai 3:9, Waefeso 4:23-24, Warumi 12:17, 2 Kor 8:21, 2 Kor 4:2) 

5. Tukue kiroho na kuzaa matunda (  Mathayo 7:24,  Yohana 15:2, Wafilipi 1:6, 1 Timotheo 6:12)

Injili ya KRISTO ni muhimu sana kwa kila mwanadamu.
Injili huzaa Wokovu na wokovu huo umepatikana kwa gharama kubwa sana ambayo MUNGU mwenyewe aliilipa pale msalabani. 
Hatutakiwi kuionea haya injili hii ya uzima. kuionea haya injili ya KRISTO ni kumuonea haya KRISTO mwenyewe jambo ambalo halifai popote. na BWANA YESU analizungumzia jambo hilo kwamba 
'' Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa BABA yake pamoja na malaika watakatifu. -Marko 8:38  '' 

Ndio maana lazima tujue kwamba hatukaiwi kuionea haya injili ya KRISTO maana injili ni uweza wa MUNGU uletao wkovu kwa kila aaminie. 
-Ndugu,Naamini umejifunza na utachukua hatua njema ya kumpokea BWANA YESU kama hujaokoka ili awe BWANA na MWOKOZI wako tangu leo na utaanza kuishi maisha matakatifu

KAMA UNATAKA KUTUBU RUDIA MANENO HAYA KISHA TAFUTA KANISA LA KIROHO UKAJIUNGE NA KUANZA KUISHI MAISHA MATAKATIFU.

''BABA katika jina la YESU KRISTO Niko mbele zako mimi mwenye dhambi, lakini leo nimetambua kosa langu na naomba unisamehe dhambi zangu zote, nisamehe dhambi ninazozikumbuka na pia zile ambazo sizikumbuki. futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike jina langu katika kitabu cha uzima. Neno lako katika Warumi sura ya 10 Mstari wa 9 na wa 10 Neno lako linasema ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu '' . BWANA YESU mimi nimekuamini leo na hivyo naamini sasa napokea wokovu wako na hakika nimeokoka. Kuanzia leo Naufunga ukurasa wa dhambi na ninaufungua ukurasa wa matendo mema na matakatifu. BWANA nipe ROHO wako Mtakatifu ili aniwezeshe kushinda dhambi na anasa zote za dunia. Kuanzia leo mimi nimeokoka na ni mtoto wa MUNGU mwenye haki zote. ninafuta laana zote na kila roho ya shetani inayonifuatilia naiharibu kwa jina la YESU KRISTO kama neno la MUNGU linavyosema katika Yeremia sura ya kwanza mstari wa 10. BWANA YESU nakushukuru sana kwa kuniokoa. Yote haya kwa imani nimepokea na niko tayari sasa kwa ROHO MTAKATIFU kunitumia. Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea .
Amen.''
Kama umetubu toba ya kweli hakika wewe kuanzia sasa ni mshindi na ni shujaa. Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine. ulishindwa kumpokea BWANA YESU nafasi yako bado ipo na muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili

Comments