HATA HAPO ULIPO TUMAINI

Na Pastor Bryson Lema, Ufufuo na uzima, Morogoro.
Utangulizi: Katika maisha ya kila siku,tunapita katika vitu vigumu na vizito. Ulalapo usiku,  huwa unamshukuru Mungu kwa sababu siku kama ile maishani mwako haijirudii tena. Hata hivyo imeandikwa katika  2WAFALME 18:19 kwamba…[Yule amiri  akawaambia, Haya, mwambieni Hezekia, kusema, Mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Ni tumaini gani hili unalolitumainia?]… Hata sisi ndivyo ilivyo kwamba kuna nyakati tunajiona hatufai tena. Ujue kuwa tatizo lako halipo kwenye ile shida uliyo nayo, bali lipo kwenye ‘tumaini’ ulilo nalo maishani mwako. Jambo la kwanza ni kubadilisha mtizamo wako, bila kuhesabu idadi ya miaka yako kwenye wakovu. Yesu Kristo alipoambiwa na Shetani ageuze jiwe liwe mkate, alimjibu shetani kuwa “mwanadamu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu”.  Weka macho yako kwenye tumaini lako.

Tatizo ulilonalo ni dogo mno bali tatizo lipo kwenye tumaini unalolitumainia. Musa hakuona Bahari ya Shamu kama kikwazo chake, kwa sababu ile bahari haikuwa pale kwa ajili ya kumuangamiza. Wana wa Israeli waliotoka Misri walikuwa ni  wengi sana, lakini ni wawili  tu waliofika nchi ya Ahadi, (Joshua na Kaleb). Siyo kwamba watu hawa wawili hawakuwaona wale manefili,  lakini kilichowasaidia ni kuwa na tumaini kwa Mungu wa Israeli. Watu hawa wawili waliweza kwa sababu tumaini lao lilikuwa kwa Mungu. Tumaini lako umeliweka wapi? Je, unamwekea tumaini ndugu yako kwa sababu amesoma sana? Kumbuka kuwa, Mungu huyo huyo aliyewaokoa wana wa Israeli ndiye aliyewaangamiza pia wale Wamisri.

Tumaini ni kama usukani ndani ya mwanadamu. Hivyo bila tumaini huwezi kwenda. Wengi akili zetu zinakuwa zimetengeneza picha, inaweza ikawa "picha za kushindwa au kushinda". Maisha ya mwanadamu ni kama msafiri na dereva uliye naye ni tumaini ulilonalo je litakufikisha salama. Unapokuwa na tumaiani ndani ya Yesu Kristo haijalishi tatizo ulilonalo. Angalia maisha yako ni kwanini hofu na mashaka zimejaa ndani yako? Ni kwa sababu umekosa tumaini katika maisha yako.Hata Yesu Kristo hakuwaponya wagonjwa wote.  Yesu alikuwa anaangalia tumaini la mtu lipo wapi. Shetani  hupenda sana kuchenzea akili za watu kwenye eneo la tumaini.  

Imeandikwa katika ISAYA 12:2…[Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;  Nitatumaini wala sitaogopa;  Maana Bwana YEHOVA ni nguvu zangu na wimbo wangu;  Naye amekuwa wokovu wangu.]… Isaya anasema Mungu ndiye tumaini lake naye hataogopa. Anasema hivi kwa sababu hofu ndio kitu cha kwanza kinachoondoe “tumaini”. Siri kubwa ya shetani ni kukuingiza hofu,  ili zipeperushe kila tumiani la watu kwa Mungu. Ili kushinda tatizo siyo  kulikimbia tatizo, bali ni kupita katikati ya hilo tatizo. Vita vikiinuka kazini, suluhisho siyo kukimbia hiyo kazi, bali mtafute aliyesababisha tatizo  na kushughulika na ile roho ya hilo tatizo ndani mwake.  Kulikimbia tatizo siyo ushindi dhidi ya hilo tatizo, bali ni sawa na kuahirisha hilo tatizo. Mungu tunayemtumikia sisi anataka tupambane na adui zetu na siyo kuwakimbia. Unapotaka kuitwa mpiganaji, lazima upigane. Ili uitwe shujaa ni lazima upambane.
Mtu yule anayepigwa ngumi ndiye anayejua uzito wa ngumi.Tunaona wana wa Israeli walipo uzunguka ukuta wa Yeriko bila wao kujua kila siku walipozunguka walikuwa wanarusha ngumi, na siku ya saba ilipofika ukuta ukaanguka. Na ulipoanguka Yoshua akasema na alaaniwe atakaye jenga tena huu ukuta. Kumbe ukuta unapoanguka laana hutolewa palepale. Hivyo hata wewe rusha ngumi juu ya adui zako. Kila unaporusha ngumi misuli yako inabadilika na inakuwa si ya kawaida, ni kama Samson alivyowekwa gerezani na kuanza kusaga ngano, Kila siku alipokuwa akisaga ngano kulimpa nguvu na uwezo misuli kukua. Tunaona siku aliyoangusha nguzo aliweza kuuwa watu wengi mno kuliko  kipindi cha nyuma.
Yesu Kristo aliliweka tumaini lake kwa Mungu, na ndiyo maana akiwa pale msalabani alimwambia Yule mwizi kuwa “Hakika, leo hii tutakuwa wote paradiso”. Imeandikwa katika YOHANA 14:1-3…[Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. 2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. 3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.]… Usiweke tumaini lako kwa mwanadamu, bali kwa Yesu Kristo, ambaye alisema anaenda mbinguni kuandaa makao,  ili alipo yeye na  wewe uwepo.   Ni Yesu pekee aliyesema alipo yeye anataka na wewe uwepo, hivyo ndio mtu unayetakiwa kumtumainia. Ukimtumainia Yesu atakupa unacho hitaji.
Kuna msemo unasema aliyeshiba hamwangalii mwenye njaa. Hivyo usitegemee kusaidiwa hata na ndugu yako maana anaweza asikusaidie. Acha kumtumainia mwanadamu maana inapotokea hatari atatafuta usalama wake kwanza na baada ya hapo ndipo ataangalia kama kuna nafasi kwa ajili yako ili akusaidie.
Siri ya mkristo wa kweli ni kupigana. Utaona Bwana asema, Bwana ni mtu wa vita, Bwana ndio jina lake. Pia anasema hiki ndio chuo cha vita. Hivyo kama mkristo ni lazima uingie kwenye chuo cha vita na upigane. Pale unapokuwa na shida ndipo mahali Mungu anajitokeza. Tunaona hata Musa alipokuwa kwa Farao penye raha, Mungu hakuweza kusema naye lakini tunaona Mungu aliweza kusema naye kwenye kichaka mahali ambapo hapakuonekana kama panafaa. Hivyo inatakiwa tatizo ulilonalo ng’ang’ania hapo hapo pambana na upigane. Hilo tatizo lililoko mbele yako ni la kupiga, haupaswi kuliogopa. Unapoiona dhahabu, ujue upo mwamba mgumu ulipasuliwa hadi ikapatikana. Unapoona mtu amefanikiwa ujue mtu huyo amepambana hadi amefanikiwa. Hivyo ili ufanikiwe ni lazima upambane.

Kuna vitu viwili kwa mwandamu miaka na hatma. imeandikwa katika YOHANA 17:1-4.. [Maneno hayo aliyasema Yesu; akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe; 2 kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. 3 Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma. 4 Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.]… Tunaona Yesu anasema Baba kazi yako uliyonipa nimeimaliza. Ina maana alikamilisha ile hatma yake baada ya miaka ile kuisha. Tunaona wana wa Israeli walikaa utumwani miaka 430 badala ya 400 ili kwenda Kanaani, NCHI YA AHADI, kwa sababu hawakujua muda. Ila baada ya Mungu kusikia kilio chao ndipo alipowatoa utumwani. Hivyo nawe ni lazima umlilie Bwana ili asikie kilio chako.
Kazi kubwa ya shetani ni kukufanya uogope. ZABURI 20:7…[Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu.]…. Ukilitaja jina la Bwana Mungu wa majeshi, utakuwa na ushindi katika safari ya maisha yako. Ukitaka kuwa mfalme kama alivyokuwa Daudi, usitaje magari wala farasi bali taja jina la Yesu.Daudi akasema toka ujana wake hadi uzee hajawahi kumuuona mwenye haki akitangatanga na kuomba barabarani. Hivyo tumaini lako liweke kwa Yesu maana hata kuacha uaibike.
Endapo Mtu hujaokoka, leo  ni fursa nyingine kwa  wewe kufanya maamuzi hayo,  ili uweze kupata ushindi sawasawa na ahadi za Mungu maishani mwako.

Comments