KADIRI WALIVYONITENDA, NDIVYO NITAWATENDA





Na:   BRYSON LEMA (RP) &
Dr. GODSON I. ZACHARIA (SNP) 

Utangulizi: Wapo Wafilisti waliomuonea Samsoni, kwa kuwa tu walishazoea sana kuwaonea wana wa Israeli, wakiwaona ni wanyonge na wa kawaida, na hivyo wakawafanya wanavyotaka. Kwa kipindi kirefu  hali hii iliendelea, na wana wa Israeli wakaizoea. Hatimaye Mungu  alimweka shujaa mmoja wa familia ya Manoa,  ili aje kuwaokoa watu wake Israeli. Imeandikwa katika WAAMUZI 15:9-11 kwamba...[Basi Wafilisti wakapanda wakapiga kambi yao katika Yuda, wakajieneza katika Lehi. 10 Watu wa Yuda wakasema, Mbona mmekuja kupigana nasi? Wakasema, Tumepanda ili kumfunga Samsoni, kumtenda yeye kama alivyotutenda sisi. 11 Ndipo watu elfu tatu wa Yuda wakatelemka hata ule ufa wa jabali la Etamu, wakamwambia Samsoni, Je! Hujui ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hii, basi, uliyotutenda? Akawaambia, Kadiri ile walivyonitenda mimi, ndivyo nilivyowatenda wao.]… Wafilisti wanaonekana kuijua kanuni hii muhimu: “ Ukitendewa  na wewe lazima uwatende”. Ndiyo maana watu wa Yuda walimfuata Samsoni kumuuliza kwa nini amefanya vile alivyofanya, kwa sababu wanajua kuwa na wao watafanyiwa vivyo hivyo‼.  Hata wewe hapo ulipo siyo mpango wa Mungu kupitia kile unachopitia katika maisha yako. Siyo kwamba Mungu alitaka uishi jinsi unavyoishi. Hata vile ulivyo  navyo usiridhike ukadhani ndivyo alivyokusudia Mungu uwe navyo, la hasha‼!  Shetani  ndiye aliyekuja na kukunyang’anya ile hati miliki yako, ili upitie yale unayopitia leo hii au umiliki vile uvimilikivyo  leo hii.
Kwa siku ya Leo hatujaja kanisani kwa ajili ya kusali, kama yupo mtu mwenye fikra hizo amekosea‼!. Leo tumekuja kanisani ili kuwatenda wale waliotutenda maishani kwetu. Unapoiona ndoa yako haiko sawa, siyo  kwamba mumeo au mkeo ndiye mbaya. Kuna kitu‼! Unapomuona mwanao hafanyi vizuri darasani pamoja na kumpeleka tuition siku zote, ujue kuna kitu‼! Adui ndiye amekuingizia kitu hicho, na usikubali kusema eti hiki ni kitu cha kawaida katika familia au ukoo wako. Kila kitu kina chanzo  na mwanzo wake. Hakuna ugonjwa ambao utamwelezea daktari  halafu  aseme eti ni ugonjwa mgeni usio kuwa na chanzo chake.
Kila unachopambana nacho sasa hivi ujue kina mwanzo wake.  Wana wa Israeli walifahamu kabisa wapo watu wanaopambana nao kila wakati. Ndiyo maana wakamuuliza Mungu swali, kuwa kwa kuwa Yoshua amekufa, ni nani atakayewaongoza kwa ajili  ya kupambana na adui zao? Imeandikwa  WAAMUZI 1:1…[Ikawa baada ya kufa kwake Yoshua, wana wa Israeli wakamwuliza Bwana, wakisema, Ni nani atakayekwea kwanza kwa ajili yetu juu ya Wakanaani, ili kupigana nao?]… Cha msingi  hapa ni kwamba wana wa Israeli  walitambua kuwa wana adui na adui yao ni nani‼ Hata wewe na mimi, kama Mkristo inabidi ufahamu kuwa katika  maisha ya kila siku, lazima uwe tayari kupigana na pia kumjua adui yako ni nani unayepigana naye.
Sihitaji kumtafuta adui yangu ni nani‼ Ninachotakiwa kufanya ni kulipiga tatizo, na nikimuona yupo anayelia  papo hapo nitafahamu kuwa ndiye chanzo cha tatizo  langu. Hii ni kwa sababu, ya ile kanuni kuwa ‘ukienda kumfungua punda aliyefungwa, atakayekuja kukuuliza kwa nini unamfungua ujue ndiye mwenye punda’.  Hatuhitaji kuwa kama wapiga ramli.  Sisi  kazi  yetu ni kupiga tatizo na atakayefungua mdomo kulia tutajua ndiye alikuwa mmiliki wa lile tatizo‼!
Pamoja na shida iliyosimama mbele yangu, Kanaani tunaingia. Pamoja na ugonjwa uliosimama mbele yangu, Kanaani nitaaingia.  Pamoja na Bahari ya Shamu iliyosimama mbele yangu, Kanaani tunaingia…. Tumechoka kwenda makanisani na kuagwa kwa kuambiwa “Amani ya Bwana iwe nanyi”…. Lakini hata hivyo, ukutanapo njiani na mganga wa kienyeji atakuwa anakucheka. Kwa nini? Kwa sababu huyo mganga wa kienyeji amefanikiwa kukuchezea usiku kucha, na hivyo amani uliyopewa kanisani hauna. Je, ni nani  mbabe kati yenu wawili? Ni dhahiri mbabe ni huyo mganga wa kienyeji. Inafaa ifike wakati ambapo hata mganga wa kienyeji awe anakiri mbele za watu kuwa “Mungu  unayemtumikia siyoMungu  wa kawaida‼” Leo ni siku ya kupambana na wale waliotutenda, nasi tuwatende vivyo hivyo.
Leo tumejipanga kupambana na adui yetu katika maeneo matatu:
1.      Kwanza ni  AFYA, kwa kuwa adui  anajua kuwa mwili wako ukiwa mgonjwa, hauwezi kupigana. Magonjwa siyo mpango wa Mungu. Kila ugonjwa umetengenezwa na shetani kuzimu. Lazima umnyang’anye shetani afya yako asiimiliki. Wapo wanaopata mishahara yao tena mikubwa tu, lakini  yote huishia kwenye matibabu  ya watu wa nyumbani mwao. Unaposikia  CHUMA ULETE,  siyo rahisi kuelezea kwa jinsi ambavyo magonjwa ya kutengenezwa yanapotokea, na kusababsiha fedha iishie kwenye matibabu‼‼. Shetani hana mamlaka ya kufunga kule mbinguni, ila uwezo wake ni wa kukufunga hapa duniani tu. Hata hivyo wewe unayo mamlaka  ya kufunga mambo yote ya shetani hapa duniani na hata mbinguni yawe  yamefungwa vivyo hivyo. Imeandikwa katika 2WAKORINTHO 10:4-5… [(maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) 5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;]… Tunayo mamlaka ya kuangusha kila kazi za kishetani zipate kumtii Kristo.
UKIRI
Kila kiwanda cha kutengeneza magonjwa, leo  nakiunguza kwa Damu Ya Yesu. Kila  adui anayetaka kurudisha kiwanda hiki namtangazia kifo kwa Jina la Yesu. Amen

2.      Sehemu ya PILI ambayo shetani hufuatilia maisha ya watu ni  katika MAFANIKIO. Wapo watu wasiopendelea kuona mafanikio yako. Imeandikwa katika KUMBUKUMBU 4:40…[ Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele.]…. Ni mpango wa Mungu ufanikiwe, wewe na uzao wako. Shetani kazi yake ni  kuzuia mpango wa Mungu usifike. Leo ni siku ya kudai chako, na vile  vya kwao, pia tunavidai view vyetu kwa Jina la Yesu‼‼ Wale walioiba kipato chako kwa muda wa kutosha, leo ni  siku  ya kuwafanya kama walivyokufanya wewe. Leo tunawagusa tu waliotugusa, ambao  hawajatugusa leo hatuwagusi kamwe kwa Jina la Yesu.
Mungu  alisema “Ahabu lazima afe”.  Hata hivyo, Ahabu aligoma akasema hatakufa. Walipoenda vitani, Ahabu alitumia ujanja/hila kwa kuyavua mavazi yake ya ufalme, na kumvisha Yehoshafati.  Wakiwa vitani, askari walikuwa wameagizwa wamtafute mfalme  Ahabu pekee na kumuua. Hata hivyo, Yehoshafati hakujua kitendo cha kuvaa mavazi ya Ahabu kingemfanya awindwe na kufa vitani. Walipomfuata Yehoshafati wamuue, ilibidi Yehoshafati apige kelele aseme yeye siye Ahabu. hata hivyo, Kijana mrusha mshale, alifanikiwa kuurusha mshale angani,  na ulipokuwa unarudi ili kutua ardhini ulienda moja kwa moja kumtafuta Ahabu alipo na kumuua‼‼! Hii ni saa ya kurudishiwa vilivyo vyetu.  Tena Biblia  inasema mwizi akikamatwa, atarejesha mara saba.
UKIRI
Ninakivunja kiwanda cha umaskini, Kwa Damu  ya  Mwanakondoo. Leo najiondoa kwenye orodha ya  maskini wa Taifa hili  Kwa Damu  ya  Mwanakondoo. Kwa Jina la  Yesu, leo naushika mshale,  maana imeandikwa Elisha alipokuwa anaumwa, Yehoashi mfalme wa Israeli akamwendea, naye Elisha akamwambia “Rusha mshale, na unapourusha sema hivi ‘Mshale wa Bwana, Mshale wa Kushinda” (2 Wafalme 13:14-19)…. na mimi  leo natangaza mshale wa Bwana mshale  wa kushinda. Na mimi leo naachia mshale wa kuangamiza kila kiwanda cha umaskini, leo nakishambulia kiwanda cha umaskini kwa Jina la Yesu. Ewe adui mwenye kiwanda nakutangazia kuwa sitakuwa maskini kamwe Kwa Damu  ya  Mwanakondoo.  Amen.

3.      Eneo la TATU la kushughulikia ni kwenye VIFUNGO,  ambavyo kwavyo  unakuwa unavipitia bila kujua. Maisha yanakwenda kwa ugumu kwa sababu ya vifungo maishani mwako. Hata Lazaro baada ya kufufuka, Biblia inasema alikuwa  amefungwa miguu yake na leso usoni mwake. Maana yake ni  kuwa,  unaweza kweli kuwa umeokoka,  lakini kumbe umefungwa na hivyo  maisha unayopitia ni ya ugumu ugumu tu. Leo ni siku ya kuwafanya kama walivyotufanya sisi. Kila aliyenifunga,  nami namfunga. Imeandikwa, “Nitakachounga hapa duniani na mbinguni kitakuwa kimefungwa
UKIRI
Kwa Damu Ya Yesu, leo nafanya  vita kukata kila kamba iliyonifunga viungo  vyangu  vya mwili. Ewe adui uliyenifunga leo nakuteketeza kwa moto wa Damu ya Mwanakondoo. Kuanzia sasa, nimetoka mautini naingia uzimani kwa Jina la Yesu. Amen
 

Zipo sababu ambazo waganga wa kienyeji na wachawi huzitumia ili kufanikisha mambo yao ya kuwatenda watu wengine kaatika maisha. Mojawapo ni hizi sababu zilizoandikwa katika MALAKI 3:7…[Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi,  nami nitawarudia ninyi, asema Bwana wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani? ]… Mtu yeyote anayeampenda Yesu lazima akimbilie kwa Yesu. Huwezi kumtenda adui yako kama alivyokutenda kama hujamrudia Bwana  Yesu. Leo tunataka tumrudie Bwana Yesu ili tuweze  kuwapiga wale waliotuonea.
Pia imeandikwa katika MALAKI 3:8-9….[Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. 9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. ]… Kumbe  kitendo cha kumuibia Mungu kinaitwa ‘laana’.  Sasa ili  kuziepuka laana hizi, kila mmoja wetu anatakiwa  kulipa zaka na dhabihu zote kwa Bwana.
Kumtolea Mungu zaka na dhabihu ni njia mojawapo ya kumfanya shetani akose uthibitisho wa kukushtaki au  kukulaani.  Imeandikwa katika MALAKI 3:10-12…[Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. 11 Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi. 12 Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema Bwana wa majeshi.]… Zaka ni kodi ya Mungu. Chakula katika nyumba ya Bwana siyo ubwabwa, ila ni neno la Mungu. Hivyo  kwa kutoa zaka, ni ili kuwezesha neno  la Bwana liweze kuhubiriwa kila mahali.
Kwa wewe ambaye hujaokoka, leo ni fursa muhimu sana kufanya maamuzi hayo ili uweze kuwatenda wale waliyotenda mabaya maishani mwako.

KWA SIKU TANO ZOTE WIKI NZIMA TUTAFUNGA NA KUOMBA

ILI KUWATENDA ADUI ZETU SAWASAWA NA WALIVYOTUTENDA SISI.

Comments