SHERIA YA UFALME.

Na Askofu Mkuu Dr Josephat Gwajima, Ufufuo na uzima

Isaya 9:6
Ufalme wa mbinguni tayari upo duniani na ndani ya ufalme huo kuna nguvu za Mungu na utukufu wa Mungu,ndani ya nguvu hizo za Mungu kuna jeshi la Ufalme ambalo ni malaika watakatifu pamoja na watakatifu na raisi wa Ufalme huo ni Yesu Kristo mwenyewe na katiba yake ni Biblia takatifu. Ndani ya Ufalme wa Mungu kuna funguo za Ufalme za kufungulia biashara, ndoa, mafanikio, elimu, safari, utajiri n.k na kila mtu anayempokea Yesu anakuwa tayari ameingia ndani ya Ufalme na Kuwa na funguo hizo. Ufalme wa Mbinguni ni nchi ya mbinguni iliyopo hapa duniani na ili kuingia ndani yake unatakiwa uzaliwe mara ya pili.

Ufalme wa Mungu hauigwi bali unaigwa mfano wake ni kama “chachu inayochachua donge zima” Ufalme wa Mungu unaimarika sana hapa duniani kiasi kwamba unakuwa unaushawishi mpaka kwenye wizara za serikali, mpaka Ikulu, mpaka Bungeni na nchi nzima inageuka na kuwa Ufalme wa mwanakondoo. Ufalme wa Mungu ukienea na kuimeza nchi inafikia watu wakiwaona raia wa Ufalme wameingia mahali ‘wanasema wale watu walioupindua ulimwengu wamefika na huku’ mpaka kufikia kila sehemu watu waseme majeshi majeshi.
Ndege kubwa kuliko zote aina ya Boeing 737 yenye uzito wa tani 270 ikitaka kupaa inaanza kukimbia mpaka sipi yake ifikie kilomita 160 kwa lisaa limoja ndipo inakuwa na uwezo wa kupaa hewani kasababu inakuwa imeshajitengenezea uwezo wa kupingana na Sheria ya uvutano wa kwenda chini na kutengeneza Sheria ya uvutano wa kwenda juu. Kwa uhakika napoanza kwenda juu ule uvutano wa kwenda chini unapungua kwasababu ya spidi iliyotengeneza Sheria ya kupaa juu na inakuwa haipungui kwasababu ikipungua Sheria ya kwenda chini itapata nguvu zaidi. Kutokana na Sheria hii tunajifunza unatakiwa ukianza kupaa kwenda juu usipunguze spidi yako na kumuomba Mungu akupe nguvu zaidi ya kupaa juu ya matatizo na magumu yote kwa spidi ile ile uliyoanza nayo kwa jina la Yesu.
Sheria ya kutembea Juu ya maji
Kwenye maisha kuna jambo ambalo mtu limemshinda kabisa amekata tamaa au kuna njia imeziba na hakuna matumaini tena, mtu huyo anatakiwa atumie Sheria ya Ufalme ya kutembea juu ya maji.

“Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari. Naye Yesu aliposikia; hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao. Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao. Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula. Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula. Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili. Akasema, Nileteeni hapa. Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume wapata elfu tano, bila wanawake na watoto. Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu.Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.” Mathayo 14: 6 - 33
Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake waende peke yao ngambo ili awafundishe Sheria ya kutembea juu ya maji, Sheria hii ndiyo inayokusaidia mahala ambapo unaona utakufa haufi na mahala unapoona utaanguka hauanguki. Ni Sheria ambayo Yesu alikuwa anatufundisha kwamba kipindi ambacho huna msaada wowote unatakiwa uitumie Sheria ya kutembea juu ya maji na utafanikiwa.
Sheria ya Ufalme ni Sheria inayofuta Sheria nyingine.

Yesu kabla hajakwenda kuitumia Sheria ya kutembea juu ya maji alianza kuomba kwanza, maana yake kabla hatujaanza kuitumia Sheria ya kutembea juu ya maji lazima tuombe. Maombi maana yake ni kuyaomba makao makuu ya mbinguni yaingilie kati maisha yetu na kutupatia ufumbuzi. Tunatakiwa tuombe tuombe kula siku ili tuwe na uwezo wa kuitumia Sheria ya kutembea juu ya maji.
“ Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.” Luka 18:1
Mathayo 14:24
Kwenye zamu ya nne Yesu hutembea juu ya maji kukifuata chombo. Kwenye kinywa chako kuna Sheria ya Ufalme wa Mungu inayozifuta Sheria zingine zote na ukisema kitu kinakuwa vilevile kama ulivyosema.
Wanafunzi wa Yesu walipomwona Yesu anakuja juu ya maji walipiga kelele kwa hofu na uoga, lakini Yesu aliwaambia wajipe moyo ni yeye. Inamaanisha ukiwa ndani ya dhoruba kali Yesu huja kwenye zamu ya nne na kuituliza dhoruba hiyo nayo ikamtii.
Ukiri
“ Bwana Yesu ikiwa ni wewe uliyeniponya magonjwa, ikiwa ni wewe uliye ikomboa familia yangu, ikiwa ni wewe uliyefufua wafu, ikiwa ni wewe uliyeniokoa kwenye mitego ya mauti naomba uniamuru nitembee juu ya maji”

“Tumeambiwa tutembee juu ya maji kwasababu tumeamriwa”
Petro alimwambia Yesu ikiwa ni yeye amwamuru amfuate na yesu alimwambia NJOO ndipo Petro alishuka chomboni akatembea juu ya maji huku akimfuata Yesu na alipojaribu kuangalia maji akaanza kuzama. Tunajifunza kwamba unaweza kumwona mtu ameokoka hana fedha, hajaenda shule, hana elimu yeyote lakini anaishi bila wasiwasi maana yake anatembea juu ya maji lakini akianza kuangalia matatizo yake na mambo mengine ya maisha yake yanavyokwenda tofauti na wengine mtu huyo ataanza kuzama kwasababu ya kupoteza imani,
Usiangalie matatizo yako mwangalie Yesu pekee ndiye mwenye kukupa uwezo wa kutembea juu ya maji, usingalie maadui au marafiki wanasema nini bali mwangalie Yesu na utafanikiwa kwa jina la Yesu.
Utakapotuliza chombo utajulikana wewe ni mwana wa Mungu.
Sheria ya Ufalme inaweza kubatilisha mambo ambayo hayawezekani kabisa yakawezekana mambo ya kuhuzunisha, mambo ya kutia balaa, kuangamiza, mambo ya kuogopesha yakaepukika na kutokutokea kwasababu ya Sheria ya Ufalme ya kutembea juu ya maji na Mungu huwa anasubiri zamu ya nne ndio atende kazi yake Mungu huingilia mambo yako pale unapomruhusu.

Ukiri.
Nabatilisha kila mpango wa kuzamisha chombo kwa jina la Yesu, ninatembea juu ya maji kwenye kazi yangu kwa jina la Yesu,natembea juu ya maji kwenye biashara zangu kwa jina la Yesu,natembea juu ya maji kwenye maisha yangu kwa jina la Yesu, mimi sio mtu wa kuliallia ninasimama na kusonga mbele nikiwa juu ya maji kwa jina la Yesu. Mimi ni mwana wa Ufalme wa mbinguni, mimi ni raia wa Ufalme, mimi ni mwana wa Mungu, mimi ni balozi wa Mbinguni hapa duniani naishi ndani ya Ufalme kwa jina la Yesu Kristo. Amen

Comments