UPENDO WA KWANZA II

Na Frank Philip Seth.

“Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu. Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, KUMBUKA NI WAPI ULIKOANGUKA; UKATUBU, UKAYAFANYE MATENDO YA KWANZA. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu. Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu” (Ufunuo 2:1-7).
Nimesoma tena mistari hii na kujiuliza swali juu hili kanisa la Efeso; huyu mtu anayenenwa hapa kapungua nini hata aitwe “aliyeanguka” na sasa anatakiwa “kutubu”? Angalia tena, kumcha Mungu ni kuchukia UOVU, huyu mtu anachukia uovu (matendo ya Wanikolai), inamaana anampenda Mungu kweli, kwa maana “kumpenda Mungu ni kuchukia uovu” sasa shida iko wapi?
Nikatazama tena na kuona, huyu mtu anakabiliwa na jambo moja, “kuondolewa kinara chake katika mahali pake ASIPOTUBU”. Sasa angalia mambo mawili: Kwanza, ameacha UPENDO wake wa KWANZA, na pili, kwa sababu ameuacha upendo wake wa kwanza, kuna MATENDO ambayo alikuwa anatenda zamani, sasa AMEACHA.
Nilipofika hapo, nikarudi na kujikagua mwenyewe, na kujiuliza je! Ni matendo gani nilifanya kwa sababu ya BWANA na sasa NIMEACHA? Je! Ni mambo gani ambayo nilifanya bila SHURUTI, KULALAMIKA au bila KULEMEWA na sasa naona ni MZIGO? Kumbuka siku zote, “UPENDO hupunguza wingi wa dhambi”, naam, hata uzito wa mzigo hupungua mabegani mwa apendaye.
Sasa je! Unaona mzigo umelemea? Je! Umefika mahali pa kuona “sasa basi”? Angalia hatua ya kanisa la Efeso walikofika, hawakufika mahali pa kukata tamaa, kuchoka wala kutamani dhambi au hata kutenda dhambi. Subira yao na jitihada yao ilisifiwa na BWANA, ila UPENDO wa KWANZA ulipungua! Yaani wanapenda ila sio kama kwanza (wangekuwa hawapendi basi wangefanya au kutamani matendo ya Wanikolai).
Napenda tena kukumbusha jambo moja, ukikaa kwa Ibilisi utabeba mizigo tu, na utakuwa mtumwa wa dhambi, na ukikaa kwa Kristo utabeba Msalaba wako KILA SIKU na kumfuta, tofauti ni aina ya NIRA na UZITO wa MZIGO utakao beba. Kwa Yesu, nira ni LAINI na mzigo ni MWEPESI. Angalia BWANA anasema, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi” (Mathayo 11:28-30). Kwa Ibilisi kuna MIZIGO ila kwa BWANA kuna MZIGO lakini nira yake ni LAINI na huo MZIGO wenyewe ni MWEPESI, na utapata RAHA nafsini wako.
KUMBUKA NI WAPI ULIKOANGUKA; UKATUBU, UKAYAFANYE MATENDO YA KWANZA. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu.
Frank P. Seth.

Comments