WALIOTAKA UAIBIKE WANAAIBIKA WAO





Na:   BRYSON LEMA (RP) &
         Dr. GODSON I. ZACHARIA (SNP)
Utangulizi: Imeandikwa katika YEREMIA 17.18…[Na waaibike watu wanaoniudhi, lakini nisiaibike mimi; na waone hofu kuu, lakini mimi nisione hofu kuu; ulete juu yao siku ya uovu; uwaangamize maangamizo maradufu.] ..Katika maisha ya  kila siku kuna vitu huwa vinaibuka maana kuna watu wanataka wewe uaibike. Kuna watu wamekaa vikao na wanataka wewe uangamie na uende kuzimu, lakini leo hayo maangamizi na hiyo aibu inarudi kwao. Bwana anasema hiyo aibu itapiga kona na kurudi kwao walioituma, maana unaye dereva Yesu Kristo anayeendesha maisha yako. Jehova anasema yeye ndiye dereva anayeendesha maisha yako haijalishi aibu waliyokuwekea maana yeye alikujua toka tumboni mwa mama yako na akakutakasa. Usihofu maana dereva uliyenaye yupo macho halali anazunguka kuangalia adui zako naye anafanya njia mahali pasipo na njia katika maisha yako. Haijalishi  tatizo lako limekaa muda gani na nani aliyelitengeneza maana ninachojua sitaaibika maana imeandikwa “achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe na ategaye mtego utamnasa mwenyewe”. Tunaona Goliathi alipoyatukana majeshi ya BWANA, Daudi alipoenda hakuangalia ni nani, ndipo akasema ni “nani anayeyatukna majeshi ya Bwana”. Ndivyo Bwana anavyosema kwako pia ni nani anayekutukana, ni nani anayekuletea aibu‼.
Mungu tunayemtumikia hawezi kukuacha uangamie, lakini mwanadamu anataka uangamie maana anachora michoro ili uangamie na uaibike, lakini tunaye dereva Yesu ambaye atakuongoza. Umefika mahali unaona kila mtu anakupinga na kukuambia kwa nini unaenda kusali mbali, wasichokijua ulikuwa na dereva Yesu aliyekuongoza kuja katika Bonde la Maono, Ufufuo na Uzima. Adui amekaa ili uaibike lakini Bwana anasema hiyo aibu haitakupata. Pamoja nao wamekesha usiku kucha  lakini kila wanachokifanya hakitakupata bali kitawarudia wao na uzao wao, maana maandiko yanasema “Bwana asipolinda mji waulindao waulinda bure”. Umesahau yupo wapi Yule Siseri aliyekuwa na magari ya chuma na yupo wapi mfalme  Ogu ambaye alikuwa ni mtu hodari kuliko wafalme wote lakini wana Waisraeli walimshinda kwa kuwa Ogu alitumainia nguvu zake mwenyewe , wakati wana Waisraeli walimtumainia Mungu, na hivyo wote walishindwa kusimama mbele ya wana Waisraeli. Hivyo usimwogope yule aendaye kwa waganga bali mwogope Mungu (ZABURI 35:1-4).
Wakati Daudi hana kitu hakuna aliyemwinukia hata mmoja, lakini baada ya kupakwa mafuta ndipo watu waliinuka juu yake ili kumpinga. Kumbe adui wanainuka juu yako baada ya kuona kitu ndani yako cha thamani kama vile Daudi. Vita ni vingi duniani kwa sababu hakuna mwanadamu anayetaka mwenzake afanikiwe, na ni furaha kwao wanapokuona unaangamia. Wote waliomwita Bwana , Bwana aliwaponya wote, hivyo unapomtumainia Bwana ndipo anapokuponya na aibu walizokuandalia adui zako. Kama vile Modekai alivyowekewa aibu na Naamani lakini Bwana alimtetea na hakuipata aibu hiyo bali ilimrudia Naamani mwenyewe.
Ipo vita iliyotengenezwa mbele yako, lakini wakati wao wanasherekea  kwa ajili ya aibu yako ndipo aibu itawarudia wenyewe. Leo  kila aliyeinua aibu juu yako tunamwambia Bwana geuza hiyo aibu iwarudie wenyewe na tunaomba Bwana aigawe vipande vipande kwa kiwango walichokutendea.
Unatakiwa ujue yale unayokutana nayo yupo aliyoyaandaa, maana kabla ya kuzaliwaBwana alishakuandalia baraka zako. Lakini adui wameinuka na kukuondelea yale ambayo ulikusudiwa uyapate. Sara alichelewa kupata mtoto hadi  katika umri wa miaka 90 maana huo ndio ulikuwa wakati wake ingawa alishakata tamaa. Hivyo nawe inawezekana sasa ndio wakati wako ingawa umeona umechelewa kupata.

Ili aibu isikupate unatakiwa kufanya yafuatayo:-
1.      Cha kwanza ni kubadilisha mtazamo wako kwanza.

Kila mtu ana mtazamo wake kwa sababu ya ile imani au jinsi unavyo muona Mungu, jinsi unavyo muona Mungu ndivyo unaweza kupata matokeo. Kama tunavyo muona Shedrack, Meshack na Abgenego walipokaa kwenye moto maana walikuwa wanamjua Mungu wanayemtumikia na kwamba atawaokoa na ni kweli akawaokoa.

Uwezo wako wa kumfahamu Mungu ndiyo uwezo wako wa kushinda. Lakini wewe unaliangalia tatizo na unalipima na uwezo wako na kujiona kama sisimizi mbele ya hilo tatizo. Maana unaliona hilo tatizo kama ni kubwa na limezidi na ndio maana miaka yote uko hapo hapo na tatizo halitoki, hivyo ni lazima ubadili mtazamo wako na umwangalie Mungu unayemtumikia. Tunamwona Gideon anapokutana na malaika, malaika anamwambia wewe ni shujaa wakati Gideon alikuwa akijificha kwenye ngano akiwaogopa Wamidiani. Ndivyo ilivyo kwako umekuwa ukijificha kwa ajili ya adui zako na kujiona udhaifu wakati ni shujaa. Gideon hakuombewa bali alibadili mtazamo wake na kujua yeye ni shujaa.

Utakapobadilisha mtazamo wako ndipo utaona uwezo wako na kuweza kushinda na pia utaona muujiza wako. Ibrahim hakuamini Mungu alipomwambia atapata mtoto Isaka katika uzee wake, ndipo Mungu akamtoa nje na kumwonesha nyota na kumwabia azihesabu ila akasema ni nyingi mno, ndipoMungu akamwambia huo ndio uzao wako. Kila alipokuwa akiangalia nyota za angani alimwona Isaka na ndio maana hata alipoambiwa amtoe Isaka hakuogopa.

Historia ni historia, hivyo usiangalie historia ya nyuma kama kuna makosa uliyafanya, bali iangalie kesho yako kwa kufuta makosa ya nyuma na kusonga mbele ili kuitengeneza kesho ya maisha yako. Ukifanikiwa kugeuza mtazamo ulionao juu ya tatizo ulilo nalo, muelekee Mungu aliye jibu la maisha yako.  Usiogope watu kukuongelea vibaya, bali wanapofanya hivyo na wewe jisifu kwa sababu una nguvu. Ukiona watu wanakusemasema ujue wameisha kuchungulia ndani, wanaona hapo ulipo sio pako wanataka uende sehemu nyingine, lakini hiyo aibu haitakupata maana ni lazima uivuke ng’ambo.
Saa imefika yakufanya ile aibu iwarudie wenyewe na saa yenyewe ndio sasa.Unatakiwa usiweke macho yako kumwangalia adui bali mwangalie Mungu maana amesema hata kuacha hadi mwisho wa dahari.  Haijalishi ni nani anaye kushambulia maana wamekaa katika njia yako ili kukuzuia na kukupinga lakini sisi tunaye Mungu mkuu kuliko miungu yote ambaye atawavua mavazi yao ili waaibike maana wanajifanya kama kondoo lakini ndani mwao ni mbwa mwitu.
2.      Baada ya kugeuza mtazamo, cha pili usikate tamaa.
Usikate tamaa maana Shetani huwa anacheza na macho yako akipima ukubwa wa tatizo na ukaliona ni kubwa kwa mapana yake. Biblia inasema Shetani ni kama Simba angurumaye, kumbe ni kama Simba lakini siyo Simba, hivyo hutakiwi kumuogopa. Lazima ifike mahali upambane kama kuku wa kienyeji maana kuku wa kienyeji huwa anakufa kishujaa. Inatakiwa uamke usikubali kutishwa, ile aibu waliyokutengezea kwa ajli yako ikawarudie wao wenyewe.

Comments