Dada watatu wajifungua siku moja

Dada watatu waliojifungua siku moja
Imekuwa ni sadfa ya aina yake baada ya dada watatu kujifungua siku moja nchini Ireland, wa nne naye akitarajia kujaliwa mtoto wakati wowote.
Watoto hao watatu wote walizaliwa hospitali ya Mayo mjini Castlebar katika Kaunti ya Mayo Jumanne.
Dada hao ambao hukaa karibu sana eneo la Cloonfad, kaunti ya Roscommon, walisema hawakuwa wamepanga kujaliwa watoto wakati mmoja.
Wahudumu katika hospitali hiyo walisema watoto wote watatu wako buheri wa afya.
Mairead FitzPatrick alikuwa wa kwanza kujifungua, akimpata mvulana kwa jina Thomas Óg, saa 03:25 saa za huko.
Dadake Joeline Godfrey alijifungua msichana kwa jina Sorcha mwendo wa saa 11:00, naye wa tatu, Bernie Ward, akajifungua mvulana aliyepewa jina Phelim saa 20:30.
Dada yao mwingine, Christina Murray, pia amelazwa hospitali hiyo akitarajiwa kujifungua wakati wowote.

Dada asikitika

Bi Murray alisema amesikitika "kiasi" kwamba hakujifungua siku moja na wenzake, lakini anatumai atampata mtoto wake karibuni.
Bi FitzPatrick aliambia kituo cha habari cha RTÉ nchini Ireland, kuwa ingawa wote walitarajiwa kujifungua muda unaokaribiana, hawakudhani wangejaliwa watoto katika kipindi cha saa 24.
"Siku yangu ya kujifungua ilifaa iwe Ijumaa, 28 Agosti, na Christina alifaa kujifungua tarehe 30,'' akasema.
Aliongeza kuwa Joeline alijifungua kwa kufanyiwa upasuaji siku ya Jumanne ili hali Bernie, aliyefaa kujifungua siku ya Jumatano Septemba 2, alijifungua siku moja mapema.
Meneja anayesimamia kitengo cha kina mama kujifungua katika hospitali hiyo, Mary Salmon, alisema wahudumu walishangazwa na sadfa hiyo.
"Sote twalizungumzia hilo hali kwamba tuna dada wanne hapahospitalini na hili halijawahi kufanyika, kadiri ya ufahamu wetu." Alisema Bi Salmon.

Comments