HISTORIA YA MAISHA YA MWIMBAJI FAUSTIN MUNISHI.






BWANA YESU asifiwe ndugu
Siku ya leo nakuletea historia ya mwimbaji nguli wa nyimbo za injili ambaye kwa sasa makazi yake yapo nchini kenya.
Leo nazungumzia historia na Faustin Munishi.
Karibu msomaji wangu wa blog hii bora ya maisha ya ushindi.
Faustin Munishi alizaliwa Mwaka 1960 huko  Moshi mkoa wa kilimanjarohapa hapa nchini  Tanzania. Aliokoka mwaka Mwaka 1980 Mjini Arusha baada ya kuisikia injili ya Yesu akaamua kumpa Yesu maisha yake. Baada ya kukoka alianza moja kwa moja kumtukuza MUNGU ambapo Alianza kuimba mwaka huo 1980 na aliitoa album yake ya kwanza mwaka 1986. 

Kwa sasa anaishi Nairobi Kenya lakini naomba ujue kwamba 
Faustin Munishi Alienda kwa mara ya kwanza Kenya mwaka 1984 kwa mwaliko wa Ndugu Kabachia Stephen ambaye ni DR. Kabachia sasa hivi.
Je ilikuwaje?
Ilikuwa hivi. Kundi lililojiita wavunaji wa YESU walitembelea Arusha kwa huduma ya Injili. Katika kanisa la pentekoste Arusha walihudumu na Munishi akiwa mshirika wa kanisa hilo, alihudumu kwa nyimbo. Dr. Kabachia na kundi lake walibarikiwa sana na huduma ya Munishi na wakampa mwaliko azuru Kenya ndipo baadae akaenda huko.

Akiwa Kenya Munishi alihubiri Karatina, Garisa, na kisha Kiambuu na Nairobi kabla ya kurejea Tanzania. Akiwa katika kumaliza ziara yake Kenya Kabachia alimjulisha kwa Mchungaji Brown Masinde ambaye sasa hivi ni DR. John Brown Masinde wa delivrance Church Umoja, wakakutana. Akiwa na Masinde walihudhuria mkutano Charter Hall Nairobi ambako Munishi aliimba kwa mvuto wa hali ya juu. Projucer wa VOK ambayo kwa sas ni KBC bwana Karanja kimwere alivutiwa na uimbaji wa Munishi na kumtaka kabla hajarejea TZ amrekodi nyimbo zake kwenye studio za VOK.
Munishi na mtayarishaji wa vipindi KBC wakati huo VOK, hawakujua wakenya na Afrika ya mashariki na kati watapenda nyimbo za msanii huyu ambapo kila mtu alikuwa akipiga simu VOK kutaka nyimbo za Munishi zichezwe tena na tena. Kuanzia hapo maisha ya Mtumishi wa MUNGU Munishi yalibadilika na nyimbo zake zikaupata umaarufu mkubwa.

 Vyombo vya habari vilichangia pakubwa kumjulisha Munishi kwa mashabiki wa nyimbo za injili, Lakini Munishi siku zote anampa MUNGU utukufu kwani nyimbo na waimbaji wako wengi na walikuweko wengi. Kwamba Nyimbo zake zilipata kibali kikubwa hivyo anaona ni MUNGU pekee na siyo media wala binadamu anaestahili utukufu. 

Miaka ya mwanzoni wa huduma yake, Kuna wakati Munishi hakuwa ametoa Albam yeyote kutokana na ukosefu wa Pesa za kulipia Studio Akiwa mjini Nakuru, na hii ni baada ya kwenda TZ na kurudi tena Kenya, Alikutana na Mzee Wiliam Bomet ambaye alipendezwa sana na nyimbo zake akaamua kusaidia pesa ili anakili nyimbo zake kwenye kanda.
Akiwa kwa Mchungaji Mark Kariuki ambaye alikuwa tu ameacha kazi yake ya ualimu wa shule ya msingi na kuamua kuanzisha kanisa la DC Delivrance Church Nakuru. Kariuki alimwomba DR. Brown Masinde amruhusu Munishi akae naye Nakuru kusaidia kuanzisha kanisa hilo. Masinde alikubali na kumpeleka Munishi Nakuru kusaidia katika kazi hiyo. Kidogo nyakati hizo kulikuwa na ugumu wa Kazi ya MUNGU kiasi kwamba hata mlo wa kila siku ulikosekana lakini watumishi wa MUNGU Mark Kariuki na Munishi hawakufa moyo. Walisimama imara mpaka kanisa kubwa Nakuru likasimama. Na hapo Nakuru ndipo Munishi alipoutunga wimbo maarufu katika kanda yake ya kwanza NINYIME GITHERI UNINYIME UGALI NIACHIE YESU.

Mzee Wiliam Bomet alimpata Munishi kwa DR. Mark Kariuki na akaamua kumsaidia pesa 7000 ambazo zilimsaidia Munishi kurekodi nyimbo zake za kwanza katika MUNISHI VOL.1 FASHION NI YESU. 

Baada ya kurekodi kanda yake ya kwanza Munishi aliweza kujilipia nyumba na chakula kutoka mauzo ya kanda yake hiyo ambayo ilitoka mwaka 1986. 
Mwaka 1988 alitoa kanda yake ya pili NIKO CHINI YA MWAMBA.
Hapo alipata pesa za kuposa mke wake PRISCA ambaye walifunga pingu za maisha 1989. Wameishi katika maisha ya ndoa kwa miaka zaidi ya  20 sasa na Munishi anasema pamoja na pandashuka za ndoa, wamesameheana na kusonga mbele na maisha hadi sasa. 

Mwaka 1990 walitoa kanda ya tatu pamoja na mke wake Prisca. MUNISHI VOL.3 ambayo ilikuwa na wimbo maarufu NDEGE AKILIA USIKU WASEMA WAMELOGWA.
Mwaka huo huo 1990 walibarikiwa na mtoto wao wa kwanza MOJASHI MUNISHI ambaye sasa ni msichana wa miaka zaidi ya 20. Amemaliza kidato cha nne 2009 na kwenda CHUO kikuu kwani alifaulu vizuri sana.
Mwaka 1992 alitoa kanda yake ya nne MUNISHI VOL 4 ambayo ina wimbo MAKOSA NI KOSA. Ilifuatiwa na Munishi VOL.5 UTAJAZA MWENYEWE mwaka 1993. Mwaka 1995 alitoa kanda yake ya sita iliyojulikana kama MUNISHI VOL 6- MALEBO. Katika kanda hii Munishi aliimba kumhusu rafiki yake MALEBO ambae amekataa kuokoka.

Miaka mitano ilipita kabla Munishi hajatoa kanda nyingine jambo lililowapa mashabiki wake wasiwasi na maadui zake wakasema pengine Munishi amekwisha. Kumbe ukimuona KOBE kainama usidhani amekwisha bali anatunga sheria. Au Ukimwona simba kanyeshewa usidhani ni paka umwekee kidole. Utararuliwa. Bado ni simba amenyeshewa tu.
Vyombo vya habari hasa magazeti ambayo siyo yaliyomuonyesha Munishi kwa watu, yalianza kuvumisha uvumi mara MKE WA MUNISHI KATOROSHWA NI MZUNGU NA MUNISHI AMEBAKI BILA MKE. Uvumi huu ulienea sana mwaka 1995 mpaka 1999. Mwaka 2000 Mtumishi wa MUNGU Munishi alipoibuka, aliimba kaseti yake ya saba ambayo wengi wameiita THE BEST OF MUNISHI. ALBUM hiyo kwa jina MUNISHI VOL. 7 - MPENDE ADUI Iligusa kila sehemu ya maisha ya jamii. Kwa mjibu wa Munishi mwenyewe aliwahi kudai kwamba
  Serikali ya Tanzania iliipiga marufuku kanda hiyo, kwa kisingizio ilikashifu CCM chama kinachotawala Tanzania pamoja na Nyerere mwanzilishi wa chama hicho. Munishi anasema nia yake ilikuwa kuwaonyesha umma wa Tanzania kwamba sera za MUNGU ni za kudumu na hazishindwi kinyume na sera za Ujamaa wa Nyerere ulioshindwa Tanzania na kuwaacha wananchi masikini wakishiriki umasikini.
Mtumishi Munishi alionya katika kanda hiyo kwamba wakati umefika kwa Watanzania kuachana na sera mbovu za ujamaa wa Nyerere ulioshindwa, na wakumbatie sera za wokovu wa YESU ambazo zinamsaidia mwanadamu kiroho na kimwili.

Maajabu ya kanda hiyo yalikuwa hayajaisha, kwani vyombo vya habari navyo vililalamika kwamba Munishi amevikemea katika wimbo NAWAOMBEA WAANDISHI WA HABARI. Katika wimbo huo Mtumishi wa MUNGU Munishi aliikumbusha jamii kwamba maovu mengi duniani husambazwa na vyombo vya habari. Alihoji kama Wanahabari wangeiamini injili basi dunia na maovu yake yangepungua kama si kumalizika kabisa. Alidai kwamba wanahabari ni  wakosoaji nambari moja walipokosolewa, ikawa ni mkuki kwa nguruwe lakini si kwa mwanadamu. Nguruwe ikiwa na jamii ambayo Media huikosoa kila uchao, na Mwanadamu ikiwa ni wanamalaika Media ambayo inajifanya sawa na MUNGU. Haina makosa Haikosolewi, Inajua kila kitu, Inaamua nani asikike na nani aisikike.
Tofauti na serikali ya Tanzania ambayo mbali na kuipiga marufuku kanda hiyo iliamuru wote watakaopatikana wakiiuza au kuisikiliza wakamatwe na wawekwe ndani bila dhamana, alidai Munishi .
Kwa upande wake Media waliipiga marufuku ya kimya kimya, anadai Munishi. Ikawa haichezwi na redio yeyote wala TV yeyote. Ni mgomo huo wa vyombo vya habari umefanya Munishi aonekane kama aliacha kuimba. Anaimba lakini hasikiki kwani vyombo vya habari vinasema navyo vimkomoe kwa kutokuicheza kanda toleo la saba la Munishi, Ndivyo alivyodai Munishi.
Pamoja na yote hayo Munishi aliamua kutumia mtandao wa Internet ambako alitengeneza  website mbili. www.munishi.com na www.gospelgtv.com pia na nafasi katika www.youtube.com/munishi2 ambako huweka video za nyimbo zake pamoja na mahubiri. Pia yuko kwenye FACEBOOK ambako ana kurasa nyingi. Mmoja ni GOSPELGTV ambao anautumia kuhojiana na mashabiki wake pamoja na kuwaruhusu kuziona video zake zilizoko youtube na kuwaonyesha kurasa tata zilizoko kwenye website zake. Ukurasa mojawapo wa FaceBook ni http://www.facebook.com/album.php…
Tangu mwaka 2000 mpaka mwaka 2010 Munishi amekuwa kimya jambo linalowapa wasiwasi mashabiki. 

 Mwaka huu 2010 Munishi alitoa albamu mpya inachojulikana kama MUNISHI VoL.8. Kuna nyimbo nyingi nzuri kama ule usemao NI KWA NEEMA SIYO MATENDO. Nyimbo zote hizo zapatikana sana kwenye mtandao wa internet 
Kwa sehemu kubwa umemfahamu Munishi na wimbo wake wa Malebo mimi binafsi ndio nadhani ndio wimbo bora zaidi.

Comments