JIFUNZE KUOMBA MSAMAHA.

Na Mchungaji Gasper Madumla.Beroya bible fellowship church.(Kimara,Dar,TZ)

Bwana Yesu asifiwe...
Neno `` Nisamehe" ni neno dogo mno lakini ndilo neno lenye nguvu zaidi ya maneno mengi tunayoyatamka. Kwa sababu neno hili linaleta urejesho pindi linapotamkwa na mtu. Mfano,ikiwa mtu amemuudhi kisha mtu huyo akapanga adhabu ya kukupa,lakini kabla hajaitekeleza adhabu yake wewe ukamuwahi kumuomba msamaha,basi ni dhahili kabisa adhabu hiyo iliyopangwa kwako hatafanikiwa. Au hata kama atafanikiwa kukuadhibu,basi ujue adhabu hiyo aitafanana na vile ilivyopangwa hapo awali tena kutakuwa na utofauti mkubwa. 

Neno hili `` nisamehe " ni la kujifunza kila siku katika maisha yetu,yaani kulifanyia mazoezi maana si wengi wenye moyo wa kulitamka. Ikumbukwe ya kuwa watoto wamepewa neno hili vinywani mwao ndio maana tumeambiwa tuongoke na kuwa kama watoto katika ili tupate fursa ya kuingia katika ufalme wa mbinguni. Mimi nakumbuka siku moja mwanangu alikuwa amekosa sasa mama yake akataka kumchapa fimbo,katika hasira za mama ndipo mtoto akamwambia mama huku akilia kwa uchungu `` nisamehe mama,sitarudia tena" lile neno `` nisamehe..." likamfanya mama yake kurudisha fimbo chini kisha nikasikia akimwambia `` ole wako urudie tena " Ndiposa nikagundua umuhimu wa neno hili `` nisamehe " 

Yawezekana neno hili wewe hulitumii na kwa sababu hulitumii hata hujaona umuhimu wa neno hili,bali niulize mimi faida ya neno hili ``nisamehe" nikuambie. Katika biblia tunaona nguvu iliyopo katika toba kwa wale waliotubu mfano mtazame Petro
alipomkana Yesu,alitubu ( Mathayo 26:69-75 ). N.K. Lakini ninachokizungumza hapa sio toba mbele za Bwana,bali kuomba msamaha mbele za mwanadamu mwenzako juu ya makosa yote uliyomtendea. 

mch.MadumlaNataka ujifunze kusema ``nisamehe" kila ufanyapo makosa. Wale wote waliotamka neno hili,walipokea jambo jipya mioyoni mwao hata kama mwenye kuombwa msamaha hajawasamehe. Kwa sababu jukumu la kusamehe ni lake yule mwenye kuombwa,lah!kama hataki kusamehe hiyo ni juu yake na Mungu wake lakini wewe uliyeomba msamaha umekwisha tengeneza vizuri na yeye,pamoja na Mungu wako. Uwe na uhakika utapokea amani ndani yako,ambayo kwa hiyo amani itafungua malango ya maisha yako.

Tatizo lako hutaki kuomba msamaha!!! Yamkini wadhani kuomba msamaha ni ushamba hivi,au wadhani ukiomba msamaha utaonekana mjinga. Hapana! Kumbuka neno msamaha ni neno la la kiungu,tazama Bwana Yesu akimfundisha Petro (Mathayo 18:21).
Kuna kipindi watakiwa kujishusha pasipo kuangalia hadhi yako wala kuangalia unaonekanaje,bali wewe sema ``nisamehe" sababu wapo watu wasioweza kabisa kuomba msamaha hata kama wamekosa. Tazama maisha ya ndoa ya leo yalivyo,wanandoa wengine hawawezi kuomba msamaha kwa wenzi wao hata kama wamewakosea,. Sijui kwako wewe!

Wengi wamewapoteza wenzi wao kwa sababu ya kushindwa kuomba msamaha. Wengi wamepoteza kazi,tena wengine wamepoteza wachumba kisa wameshindwa kujishusha kwa kuomba msamaha.


Yamkini waweza kuwa wewe ni mmoja wa watu wa namna hii ambao wamefanya makosa,na wanajijua kwamba umefanya makosa lakini hutaki kuomba msamaha kwa yule uliyemkosa. Jitahidi ufanye hivyo mpendwa ili amani ikae ndani yako. Ona sasa umekosa amani kwa sababu hukulitumia neno ``nisamehe" tu. Jifunze neno hili kulitamka kwa uliyemkosa.

Na ukiona labda unashindwa kabisa kwa sababu yoyote ile au labda kwa sababu ya ukubwa wa kosa lako,basi nakuomba unipigie ili tusaidiane hapo na amani ya Kristo Yesu ikae ndani yako.
Usiache kunipigia,kwa huduma ya maombezi piga +255 655111149.
Mchungaji Gasper Madumla.
Beroya bible fellowship church.(Kimara,Dar,TZ)
UBARIKIWE.

Comments