MAOMBI YA KUFUTA MAAGANO YOTE YA KISHETANI.



BWANA YESU asifiwe.
Leo nataka tuombe maombi ya kuvunja maagano.
Mwanzoni wa wiki hii tukiwa katika maombi ya mkesha kanisani sauti ilinijia kusema vunja maagano ya giza, ufafanuzi ulikuwa mkubwa na nikashangaa sana.
 Kumbe kuna maagano mabaya mengi ya adui ili kuhakikisha hatusongi mbele lakini ashukuriwe BWANA YESU maana damu yake ya Pasaka inaweza kufuta maagano yote ya kipepo.

Kutoka 23:32 ''Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao.''
Agano ni kitu kikubwa sana, Agana la kipepo ni mapatano ya kishetani, ni mikataba ya kishetani na MUNGU hataki tuingie agano lolote na shetani wala mawakala wake.
Adui kwa kulijua hilo kwamba hatumtaki na mipango yake yote basi kuna vitu huwa vimefanyiwa maagano tayari kwa ajili yetu kitu ambacho tusipoomba kuna madhara ya kiroho na hata ya kimwili.

-Kumbe kuna maagano kwenye baadhi ya vyakula hivyo ni muhimu sana kuombea chakula.
-Kuna vitanda vina maagano mabaya.
-Kuna maeneo yamejaa maagano mabaya.
-Hata ardhi yako adui anaweza kuifanyia maagano mabaya ili usifanikiwe.
-Mambo mengi sana yamewekewa maagano na adui ndio maana tunatakiwa kuomba sana.
unaweza kujiuliza swali dogo tu kama hili; kwanini wanawake wengi ndio huteswa sana na mapepo?
Jibu ni vitu wanavyotumia maana vingi vina maagano ya kipepo, vingi vina mapando ya shetani mfano vipodozi, mapambo, nywele bandia n.k.
Adui anapanda kitu kidogo tu lakini ukizubaa utajikuta mara unavalishwa pete na mwanaume usiyemjua dotoni kumbe jini maana vitu vyako ndivyo vilivyofungua mlango kwa jini huyo kuingia kwako, na akikuweza anaweza hata kukuzuilia kufunga ndoa au kwenda kanisani au kusoma biblia huku ukitamani lakini umeshindwa.
Adui anaweza kupanda kitu kidogo tu na ukizubaa utajikuza unapenda miziki ya kidunia tu na nyimbo za MUNGU utaona machukizo kumbe adui anakuendeza kipepo.
Adui ukimpa nafasi kidogo tu, ukizubaa unaweza kujikuta kila siku unaota ndoto ukizini kumbe shetani anaongeza maagano mengine zaidi ili hata kupata mtoto baadae iwe tatizo.
Ndugu yangu, maagano ya kipepo lazima yaondoke kwa jina la YESU KRISTO ndio utakuwa huru.
-Kuna watu sura zao zimefanyiwa maagano ya kipepo ya kuchukiwa na kila mtu,  unaweza ukakosa mme au mke kwa sababu tu ya tatizo hilo la kishetani la maagano.
Maagano ni mabaya sana.
-Kuna maagano kwenye baadhi ya mavazi tunayonunua N.K, hivyo ni muhimu sana kutakasa Tunavyonunua  kwa jina la YESU.

Hata kuna baadhi ya vitanda vina maagano mabaya, na MUNGU anapokataza uzinzi ni kwa lengo la kukusaidia tu mwanadamu wewe na sio vinginevyo. maana uzinzi unaweza ukaongeza tatizo zaidi badala ya dhambi tu basi na maagano ya giza juu yake.

Isaya 57:8 '' Na nyuma ya milango na miimo umeweka kumbukumbu lako; kwa maana umejifunua nafsi yako kwa ajili ya mwingine, si kwa ajili yangu, ukakwea juu; umekipanua kitanda chako, nawe umefanya maagano na hao; ulikipenda kitanda chao hapo ulipokiona. ''
-Maagano mabaya ni jambo baya sana ndugu. kama zamani uliwahi kuingia maagano ya kishetani basi kimbilia kanisani ukaombewe maana maagano ni mkataba na ukiingia mkataba na shetani mwishowe anaweza kukuangamiza tu na uzima wa milele ukaukosa.

Hosea 10:4 ''Hunena maneno yasiyo na maana; huapa kwa uongo wafanyapo maagano; basi ndipo hukumu huchipuka kama mbaruti katika matuta ya shamba.''

-Maagano ya kishetani ni mabaya sana na ni muhimu kujitenga nayo kwa kumkimbilia BWANA YESU na nguvu zake.
Wachawi wakati mwingine wanaweza kuifanyia maagano mabaya sauti yako na ndio maana kinywa chako kila siku kinakutendesha dhambi.
-Sio kila zawadi unapokea tu bila hata kuiombea.
-Sio kila mialiko lazima uende. omba kwanza na msikilize ROHO.
Adui ana mbinu  nyingi lakini kama  utakuwa mwombaji hakika utashinda.
Kuna maagano mengine inahitajika nguvu kubwa sana ili kuyavunja na nguvu kubwa ni mbili tu, Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO.
Najua umejifunza kitu na utachukua hatua ya kuomba na kujiunga na kanisa la kiroho ili uwe kwenye mzunguko wa maombi.
Kuna watu huwa nawaambia wajiunge na kanisa na wanapofanya hivyo tu mateso yao ya kuteswa na wachawi yanakoma. unajua ni kwanini? ni kwa sababu wanakuwa katika mzunguko wa maombi, mfano mchungaji kama atafunga au ataomba kwa ajili ya huduma yake ni lazima akujumuishe na wewe maana uko katika huduma hiyo, kama viongozi wa wamama au viongozi wa vijana watakuwa wanaombea vijana wao au wamama au wababa lazima na wewe utakuwa unaombewa hivyo ukiongeza na maombi yako mwenyewe na kuhudhuria ibada hakika adui atakimbia hata kama hataki maana atakuwa anapata kipigo kila saa, kama anadhani umelala wewe akisogea tu anapata kipigo maana wakati huo mchungaji anaomba, wakati huo kundi la maombi linaomba.
Kujiunga na kanisa na kuanza kuishi maisha mataktifu ya wokovu wa BWANA YESU ni jambo la muhimu sana.

Maombi ya kuvunja maagano ya kishetani.

BABA yangu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe milele, ninakushukuru BWANA kwa kunilinda na kunipa afya njema.
Ninakushukuru kwa kuwalinda ndugu zangu na familia yangu.

BWANA YESU, mimi ni binadamu na yawezekana kabisa kuna sehemu nimekosea, BWANA naomba unisamehe dhambi zangu zote, zile ninazokumbuka na zile ambazo sikumbuki. Neno lako Katika Matendo 3:19 linasema ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;'' . BWANA ninatubu leo na naomba unisamehe MUNGU wangu. nipe kuishi maisha ya ushhindi dhidi ya dhambi na nipe kumtii ROHO MTAKATIFU maana ndiye mwangalizi wa roho yangu. nakushukuru JEHOVAH BWANA maana naamini umenisamehe MUNGU wa uzima.
BWANA neno lako linasema katika Isaya 41:21 kwamba '' Haya, leteni maneno yenu, asema BWANA; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo.''. BWANA hoja yangu yeye nguvu ni maagano ya kipepo yote ambayo ninaomba yafutike leo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO. Maagano ya magonjwa na maagano ya ardhi ninayokaa nayafuta kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO maagano ya mavazi na maagano ya maagano ya vyakula nayafuta kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO, Kila aina ya agano la shetani maishani mwangu ninalifita leo kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO. Kila agano la giza, haijalishi nililifanya mimi au wazazi wangu ninafuta agano hilo kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO. Kila agano la kishetani kwenye ardhi yangu au nyumba yangu ninalifuta kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO. kila agano la giza kwenye kitanda nilichowahi kulalia au kwenye mashuka niliyowahi kujifunika ninafuta maagano hayo kwa jina la YESU KRISTO. Kila agano la giza  kutoka kwa wote niliowahi kufanya nao mapenzi kimwili au ndotoni ninafuta maagano hayo kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO. Kila agano ambalo yawezekana silijui au nalijua ambalo nila giza ninalifuta kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila agano la giza kuanzia leo limefutika kwa jina la YESU KRISTO, kuanzia sasa niko huru mbali na maagano ya kishetani, kuanzia sasa mimi ni mishindi kwa jina la YESU KRISTO. Nakushukuru BABA wa mbinguni maana umenishindia, nakushukuru BWANA YESU maana damu imenena mema kwangu kuanzia sasa maana maagano mabaya yote yamefutika kwa jina la YESU.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi. Amen Amen AMEN KWA yesu.


Ndugu Yangu, Usikubali Kumkana YESU Na Hakikisha Unajikana Ili Umpendeze MUNGU.
Usitende Dhambi Maana Kutenda Dhambi Ni Kumkana BWANA YESU.
Ukidumu katika mema bila kumkana YESU utafanya vyema.
Yeye BWANA YESU anasema '' Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. -Yohana 10:28 ''

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana.
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments