MWALI WA MOTO WA MADHABAHU



Na Askofu Mkuu Josephat Gwajima, Ufufuo na uzima.

Waamuzi 13:20
“Kwa maana, ikawa, mara huo mwali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa Bwana akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakainama kifudifudi.
Madhabahu, kuhani, kafara, Mungu wa madhabahu, nguvu ya madhabahu au mwali wa moto wa madhabahu. Mungu huwatembelea watu kupitia madhabahuni. Ukiona nchi Mungu hadhihiriki maana yake hakuna madhabahu ambayo inamuunganisha na nchi hiyo. Ukitaka kujua madhabahu yenye nguvu ni madhabahu ambayo vitu vinavyotamkwa kwenye madhabahu hiyo visambaa kila mahali kwenye nchi nzima.
Madhabahu ni daraja linalotoka ulimwengu wa rohoni kuja ulimwengu wa mwilini na kutoka ulimwengu wa mwilini kwenda ulimwengu wa rohoni. Maana yake Mungu anapotaka kuleta kitu anatoka kwenye ulimwengu wa rohoni kuja ulimwengu wa mwilini kupitia madhabahuni, iwe ni Baraka iwe ni miujiza iwe ni laana au jambo lolote lazima lipitie madhabahuni.

Kuna madhabahu za aina mbili
1. Madhabahu ya ibilisi: astoresh, baali
2. Madhabahu ya Mungu.

Isaya 19:19 - 25
“Katika siku hiyo itakuwako madhabahu katika nchi ya Misri kwa Bwana, na nguzo mpakani mwake kwa Bwana. Nayo itakuwa ishara na ushuhuda kwa Bwana wa majeshi katika nchi ya Misri; kwa maana watamlilia Bwana kwa sababu ya watu wawaoneao, naye atawapelekea mwokozi mwenye kuwatetea, naye atawaokoa. Na Bwana atajulikana na Misri, na Wamisri watamjua Bwana katika siku hiyo; naam watamtumikia kwa dhabihu na matoleo, nao watamwekea Bwana nadhiri, na kuzitekeleza. Naye Bwana atapiga Misri, akipiga na kuponya; nao wakirudi kwa Bwana, atakubali maombi yao na kuwaponya. Katika siku hiyo itakuwako njia kuu itokayo Misri na kufika hata Ashuru; Mwashuri atafika Misri, na Mmisri atafika Ashuru, na Wamisri wataabudu pamoja na Waashuri. Katika siku hiyo Israeli atakuwa wa tatu pamoja na Misri na Ashuru, watakuwa baraka kati ya dunia; kwa kuwa Bwana wa majeshi amewabariki, akisema, Wabarikiwe watu wangu Misri; na wewe Ashuru, kazi ya mikono yangu; na wewe Israeli, urithi wangu.

Neno nguzo maana yake ni viongozi na madhabahu maana yake ni daraja, Mungu anamaanisha siku za mwisho Mungu atainua madhabahu kutokea Misri ambayo ni Africa na uamsho wa siku za mwisho atainua maajabu kupita akili za wanadamu na maajabu hayo yataanzia Afrika na kuzikumba nchi za kiarabu na baadaye kuikumba Israeli kwa nguvu za Mungu. Bwana atajulikana kwa waafrika. Mungu amewavisha waafrika akili katika kumjua yeye na matendo yake makuu. Kutoka Afrika Mungu anatengeneza njia kuu ya uamsho, uponyaji, maajabu, miujiza kutokea kuelekea ashuru.
Kwenye agano la kale Wayahudi waliishi kwa muda wa miaka 430, Mungu alionyesha maajabu katika nchi ya Afrika, mahali ambapo maajabu 12 yaliyopigwa, Maana yake Mungu alikuwa anaonyesha katika siku za mwisho atafanya mambo ya ajabu na makubwa. Musa alizaliwa katika nchi ya farao aliishi huko na kukulia huko lakini alikuwa na wito wa kuwapeleka watu wa Bwana kwenye nchi ya kutiririka maziwa na asali. Mungu alimtuma Joshua baada ya Musa kufariki na Mungu akamwambia Joshua uwe na moyo wa uhodari na ushujaa maana yeye ndiye atakaye wafikisha kwenye nchi ya ahadi. Joshua alipochukua mamlaka aliamua kupita kwenye njia tofauti na baba yake, kwa kuanza safari kabla maji hayajagawanyika na Biblia inasema wana wa Israeli walipoukanyaga mto maji yaliganda na wakapita kwenda kwenye nchi ya ahadi. Wakati Musa anaomba na kutembea naye. Ukiona kuna kanaani ujue kuna Musa na Joshua. Na kama Joshua yupo basi hakuna mtu atakaye simama mbele yake.
Musa alimwoa mwanamke mwafrika na dada yake akawa anamchukia na kulalamika kwa Musa kumwoa mwanamke mwafrika lakini Bwana akajitokeza na kusema akiwepo nabii katikati yenu nitaongea naye ndoto lakini sio kwa mtumishi wangu Musa yeye nitaongea naye ana kwa ana na Mungu akamkasirikia Mariamu kwa kumnenena vibaya Musa na akaondoka na palepale mariamu akapatwa ukoma. Maana yake Mungu alikuwa anamaanisha waafrika ni watu anaowapenda hataki mtu awachezee.

Israeli atakuwa watatu pamoja na Uarabuni na Afrika. Misri ni watu wa Bwana, Ashuri ni Afrika kazi ya mikono yake na Israeli taifa lake. Madhabahu hiyo naomba Mungu iwe ni Tanzania ambayo itakuwa daraja la kwenda Uarabuni na akuishia Israeli ili kuwa utatu wa Baraka za Mungu hapa duniani.
1 Wafalme 18:30
“Naye akajibu, Si mimi niliyewataabisha Israeli; bali ni wewe, na nyumba ya baba yako, kwa kuwa mmeziacha amri za Bwana; nawe umewafuata mabaali. Basi sasa upeleke watu, unikusanyie jamii ya Israeli katika mlima wa Karmeli, na wale manabii wa Baali mia nne na hamsini, na wale manabii wa Ashera mia nne, walao chakula mezani pa Yezebeli. Basi, Ahabu akapeleka watu kwa wana wa Israeli wote, akawakusanya manabii pamoja katika mlima wa Karmeli. Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno. Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri. Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng'ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini. Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya. Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe. Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika. Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia. Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza.

Baali alijenga madhabahu na wayahudi walikuwa wameunganishwa kwenye madhabahu ya kishetani ambapo Kulikuwa hakuna uhusihano kati ya kuzimu na kwenye nchi yao, wakati huo madhabahu ya Mungu ilikuwa imevunjika. Waliomba kuanzia asubuhi mpaka jioni kupandisha moto tokea chini kuja juu lakini hakuna kilichotokea. Hata kwenye baadhi ya nchi kuna madhabahu ambazo zinaongoza kutokea kuzimu ambapo watu wa nchi hizo wanakuwa na akili na tabia za aina fulani kutofautiana na nchi zingine. Eliya alijenga madhabahu ya Bwana kwa mawe ili ashushe moto juu yake kutokea mbinguni na amdhihirishe Mungu kuwa yeye ndiye astahiliye kuabudiwa na ikawa hivyo. Mungu wa Eliya ndiye tunaye mwabudu sisi.
2 Nyakati 33:16
“Akaijenga madhabahu ya Bwana, akatoa juu yake dhabihu za sadaka za amani, na za shukrani, akawaamuru Yuda wamtumikie Bwana, Mungu wa Israeli.

Mungu aliwaambia wana wa Israeli popote pale watakapoingia wavunje madhabahu za baali. Unapoona jambo lolote duniani lazima limetoka kwenye madhabahu ya Mungu au madhabahu ya shetani.
Waamuzi 2:2
Nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani?”

Mungu alitaka wabomoe madhabahu za adui ili kukata mawasiliano yao na kuzimu na kujenga madhabahu yake ili aingie kwenye maisha yao na kutenda kazi na kuwabariki, kila tatizo unaloliona hapa duniani limetokea madhabahuni.
Neno la Mungu lazima lihusihane na maisha yetu ya kila siku, kwenye magonjwa, laana, mikosi, umasikini, taabu na matatizo yote ufumbuzi wake upo kwenye neno la Mungu.
Neno madhabahu limeandikwa kwenye Biblia Zaidi ya mara 300, kwenye kitabu cha mambo ya walawi limeandikwa mara 72 kwasababu makuhani wametokea kwa walawi na kitabu cha walawi kinahusu watumishi Mungu, pia anamaanisha na ukitaka kuwa mtumishi wa Mungu lazima ujue mambo ya madhabahu. Kwenye kitabu cha kutoka neno madhabahu limeandikwa mara 53 maana yake ukitaka kutoka lazima ujue kuna madhabahu. Neno madhabahu kwenye kitabu cha Wafalme limeandikwa mara 43 maana yake ukitaka kuwa mfalme lazima uwe na madhabahu inayokuongoza.
Waamuzi 6: 1 – 10, 22
“Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana; Bwana akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome. Basi ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao wana wa mashariki; wakakwea juu yao; wakapanga marago juu yao, na kuyaharibu hayo maongeo ya nchi, hata ufikapo Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki ziwazo zote; kondoo, wala ng'ombe, wala punda. Kwa maana walikwea na ng'ombe zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia walikuwa hawana hesabu; nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu. Israeli walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani; nao wana wa Israeli wakamlilia Bwana.

Kisha ikawa, hapo wana wa Israeli walipomlilia Bwana kwa sababu ya Midiani, Bwana akamtuma nabii aende kwa hao wana wa Israeli; naye akawaambia, Bwana, yeye Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi niliwaleta ninyi mkwee kutoka Misri, nikawatoa katika nyumba ya utumwa; nami niliwaokoa na mikono ya Wamisri, na mikono ya wote waliokuwa wakiwaonea, nami niliwafukuza watoke mbele zenu, nami niliwapa ninyi nchi yao; kisha niliwaambia, Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu; msiiche miungu ya Waamori, ambayo mwaketi katika nchi yao; lakini hamkuitii sauti yangu. 22 Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa Bwana; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona Bwana uso kwa uso. Bwana akamwambia Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa. Ndipo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri. Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo.
Leo tumebomoa madhabahu inayoshikilia Tanzania na watu wake kwa jina la Yesu, madhabahu ya magonjwa, laana, umasikini, matatizo, shida, wizi, ujinga, zinavunjika kwa jina la Yesu.
Karafa ya madhabahu ya wakristo ni Kafara ya Yesu alipokufa msalabani na nguvu yetu ni nguvu ya Roho mtakatifu.
Wachawi wapo na wana madhabahu zao ambazo ndipo sehemu wanayokusanyikia kufanya mambo yao, wana viwanja vyao ambapo ndipo wanapoweka mawazo yao ili yafanyike. Kila familia ina mchawi wa familia ambaye ni mtu anayependa kupindisha familia hiyo. Jina lako linaweza kwenda kwenye madhabahu hizo za kichawi na mtu huyo aliyelipeleka anaambiwa atoe sadaka ya madhabahu kama kafara. Kafara hiyo inaweza ikawa ni damu ambayo inakuwa inanena mabaya yaliyokusudiwa yakupate, mahala ambapo damu hiyo ipo panaitwa madhabahu ya wachawi na damu hiyo inakua inanena tena na tena lile jambo lilikusudiwa limpate mtu fulani mfano;- Fulani afe afe afe, afilisike afilisike, awe maskini awe maskini, ashindwe ashindwe, ashindwe, afariki afariki afariki.

Inatakiwa wewe mwenyewe uamue kuzifuata hizo madhabahu na kuzibomoa kwa jina la Yesu, unasema katika jina la Yesu nazifuata madhabahu zilizo nilaza akili yangu, zilizo zuia biashara yangu ninazivunja katika jina la Yesu, ninawafuata makuhani wote wa madhabahu za familia yangu ninawateketeza kwa damu ya Yesu, nina wa fyeka kwa jina la Yesu.
1 Wafalme 16: 31 – 34
“Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia. Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria. Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia. Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.

Herieli mbetheli aliamua wanawe wafe ili asimamishe ukuta wa utawala wa yeriko uliokatazwa usijengwe tena na Bwana. Kuna maisha ya watu ambayo yanaimarishwa kwa kuwatoa kafara za watoto ili wajenge tawala zao za uchumi, siasa, biashara au kazi.
2 Wafalme 3: 26 – 27
“Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki. Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe

Mfalme wa Israeli anakweda kupigana na mfalme wa moabu na Mfalme lakini mfalme Moabu alipoona anaelekea kushindwa alitoa kafara ili ashinde vita hiyo, ndipo wana wa Israeli walipoona amemtoa kafara mwanaye wakaamua kukimbia. Farao alikuwa anawatupa watoto baharini kama kafara ya kuimarisha utawala wake. Na kuna watu wametoa kafara ili washinde uchaguzi wa uraisi, ubunge, au udiwani na leo tunazivunja kafara hizo zote kwa jina la Yesu kristo na kubomoa madhabahu zao zote kwa jina la Yesu.
Kuna kafara ilitolewa miaka elfu mbili iliyopita ambayo ni kafara inayozitafuna kafara zingine zote kafara hiyo ni damu ya Mwanakondoo Yesu kristo.
Unaposema katika jina la Yesu ninaifuata madhabahu iliyonishikilia madhabahu ya kichawi iliyoshikilia taifa la Tanzania ,madhahu iliyo Ikulu, madhabahu iliyo bungeni, madhabahu iliyo lindi, madhabahu ya mwenge, madhabahu iliyo mahakani, madhabahu iliyo baharini ninaifuata na kuivunja kwa jina la Yesu kristo.
Unaposema hivyo kwenye ulimwengu wa rohoni unakuwa umekwenda na kuzifuata madhabahu zote sababu wewe ni roho na Mungu naye ni roho hulituma neno lake likaenda na kuzivunja, ukiwa unatamka unaziangamiza kabisa sababu umepewa uwezo huo kwa Jina la Yesu.

Comments