NATAMANI KILA MWANAMKE AYATAMBUE MAMBO HAYA 10.





Scholar Mabula

Na Mtumishi Peter M Mabula.

BWANA YESU atukuzwe sana ndugu yangu.

Karibu tujifunze na kupata ufahamu mzuri sana unaozaa
matunda mema sana.

Mwanzo 1:27 ‘’ MUNGU akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa MUNGU alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. ‘’
-Kumbe MUNGU aliwaumba wanadamu wa jinsia zote tena kwa mfano wake MUNGU. maana yake wanadamu wameumbwa wakiwa na roho, mwili na nafsi au akili. hatufanani na MUNGU kwa sura bali tukikaa katika utakatifu hakika tunakuwa tunatimiza kufanana na MUNGU maana MUNGU ni mtakatifu.
Kumbe tumeumbwa kwa mfano wa MUNGU Hivyo ni vizuri sana kila mtu kujua hilo kwamba tumeumbwa kwa mfano wa MUNGU, na sio kwamba tumeumbwa ili tufanane na MUNGU kwa sura. 
Kwa mfano maana yake ni kama mtu anatembea na watu wengine wakakiona kivuli chake na kusema kinafanana na mtu lakini kivuli sio mtu, na wanadamu ni hivyo tumeumbwa kwa mfano wa MUNGU lakini sisi sio MUNGU.
Biblia inapozungumza kwamba Wanadamu tumeumbwa kwa mfano wa MUNGU maana yake mwanadamu ni kiumbe tofauti katika viumbe vyote alivyoviumba MUNGU.
 Tumepewa heshima kubwa kupita viumbe vyote vilivyoumbwa na MUNGU vilivyo hapa duniani.
Kila mwanamme duniani ni wa kipekee kuliko viumbe vyote duniani na kila Mwanamke ni wa kipekee maana amepita viumbe vyote duniani.

Leo nazungumzia wanawake Wakristo wacha MUNGU,  katika kweli ya MUNGU ambayo ni KRISTO.

Mwanamke aliye mteule wa KRISTO ni mrithi  wa uzima wa milele, kama ilivyo kwa mwanaume aliye mteule wa KRISTO.

Mwanamke kaumbwa na MUNGU kama alivyoumbwa mwanamume.

Japokuwa mwanamke ametokea katika Mwanamme lakini pia wanaume wote hutoka katika tumbo la Mwanamke.

Mwanamme hakuuumbwa kwa ajili ya mwanamke lakini mwanamke aliumbwa kwa ajili ya mwanaume kama maandiko yasemavyo(1 Kor 11:9, Wala mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanamume. ), lakini hiyo haiondoi thamani ya mwanamke.

Kwa kanisa wanawake ni wa muhimu sana na ndio wengi zaidi kanisani kwa sababu walio wengi wameishinda dhambi ya kiburi cha kukataa wokovu wa KRISTO. Wokovu wa KRISTO Ndilo jambo muhimu zaidi kwa kila mwanadamu duniani lakini makanisani wamama ndio wengi zaidi kuliko wababa. Biblia inawathamini sana wanawake ndio maana wanawake waliookoka wanaitwa jeshi kubwa(Zaburi 68:11, BWANA analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa; )
Sina haja ya kuzungumzia jeshi na kazi zake lakini wanawake waliookoka ni jeshi kubwa la kupigana vita ya kiroho. Wanapoitwa jeshi maana yake ni wanajeshi wanaopigana na kushinda vita.
Leo nataka niseme hivi;

Mwanamke lazima ajitambue na mambo haya  10 yatamsaidia mwanamke  kujitambua na kufanya kazi ya MUNGU kwa ujasiri. Pia mambo  haya 10 yatamfanya mwanamke ajitambue na kujua thamani yake ili aendelee mbele katika ushindi mkuu ulio katika KRISTO YESU.

     1. Mwanamke jikubali kwamba wewe ni mwanadamu mwenye thamani sawa na wengine wote mbele za MUNGU.
-Jikubali katika kila eneo katika hatua zako za maisha huku ukimtii KRISTO.
-Jikubali katika huduma yako.
-Jikubali kwa sura na umbo lako maana wala hukukosewa kuumbwa. Kama mtakuwa kundi la wanawake 1000 kisha akaja mtu akasema ''Wanawake 20 warembo watoke mbele'' toka kwa kujiamini bila kujali kuna wanawake 1000.
Kumbuka kuwa kila Eva ana adamu wake na adamu huyo hutoka kwa MUNGU kupitia maombi na utakatifu wako Mwanamke.
Wanasaikolojia wanasema kwamba ''Kila mwanadamu duniani kuna watu 5 duniani wanaompenda sana na wako tayari kwa lolote kwa ajili yake. jambo la pili kila mwanadmu kuna watu 15 duniani wanampenda sana na wanatamani kuwa kama yeye''
Hii ni maana ya kiutafiti wa kibinadamu lakini inawezekana kabisa kila mtu duniani kuna watu zaidi ya 50 wanampenda sana na wanatamani kuwa kama yeye haijalishi ana umbo gani, ana sura gani au yuko katika mazingira gani.
-Mwanamke jikubali kwamba una ROHO wa MUNGU ndani yako maana ROHO MTAKATIFU hukaa katika watakatifu wote bila kujali jinsia zao.
BWANA anasema  '' Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.-Yoeli 2:28-29 ''

   2. Mwanamke jiamini maadamu hufanyi dhambi kwa MUNGU.
-Jiamini katika maamuzi.
-Jiamini katika  kuwasaidia wengine na jiamini katika kuwaeleza ukweli wengine.
Jiamini na usikubali kusema ''mimi siwezi labda fulani''
Warumi 14:18-19 '' Kwa kuwa yeye amtumikiaye KRISTO katika mambo hayo humpendeza MUNGU, tena hukubaliwa na wanadamu. Basi kama ni hivyo, na mfuate mambo ya amani na mambo yafaayo kwa kujengana.'' 

   3. Mwanamke jitambue.
-Jitambue kwamba wewe ni wa thamani sana.
-Jitambue kwamba wewe ni mtu muhimu sana katika jamii, katika familia na katika kanisa la MUNGU.
Mwanamke akijitambua hatajiona mnyonge na ataomba kwa MUNGU BABA ili yeye mwanamke asiwe wa  kutumikishwa tu kama mashine ya kusaga mahindi. asitumikishwe katika maamuzi, asitumikishwe na shetani kisa tu mmewe ni mganga wa kienyeji. asitumikishwe na majini kisa tu mmewe ni mfuga majini. asitumikishe katika kuchagua mchumba bali ashauriwe lakini maamuzi yawe yake huku akimtegemea ROHO MTAKATIFU.
Wagalatia 5:16 ''  Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. ''

  4.  Mwanamke  jithamini maana wewe ni wa thamani sana mbele za MUNGU.
-Tambua kwamba, kama hutajithamini hakuna hata mmoja atakayekuthamini.
-Thamani yako ni kubwa sana lakini lazima uijue na uitetee.
- Mwanamke anayejithamini hawezi kuwa mchafu.
wengi badala ya kujithamini wao hujithaminisha kitu ambacho hakina maana sana.
-Kujithamini huongeza thamani yako jambo hilo naomba ulijue na ulikariri siku zote. Mwanamke anayejithamini Biblia inasema Moyo wa mmewe humwamini.
Mithali 31:10-12 '' Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani. Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato. Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake. ''

   5.  Mwanamke Jielewe
- Mwanamke akijielewa kwamba pasipo MUNGU hawezi kuishi basi atamtegemea MUNGU. MUNGU ni utakatifu na naomba ujue jambo hilo kwamba moja ya vitu ambavyo  hunyonya nguvu ya MUNGU ndani ya wanawake Waaminio ni umbea, masengevyo, husuda na wivu. binafsi mtu anayeteswa na mambo hayo mimi humuona kwamba huyo bado hajielewi kwamba yeye ni nani. maana kama angejielewa basi angebaki katika kusudi la MUNGU la utakatifu.anayejielewa lazima ajiepushe na haya.
Wagalatia 5:19-21 '' Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa MUNGU.''
 
   6.  Mwanamke Jitunze na tunza utu wako.
-Ni muhimu mwanamke kujitunza hasa mwili.
-Kuna wamama leo wanateseka na watoto waliowazaa bila ndoa na sababu ya hayo yote ni kutokujitunza.
-Kuna wadada hujiuza na kupelekea kuyaweka rehani maisha yao maana zamani hizi zimejaa magonjwa, chanzo cha kujiuza ni kwa sababu ameshindwa kujitunza tangu mwanzo.
Mithali 31:30 ''Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye BWANA, ndiye atakayesifiwa. ''
 
-Heshima inayotokana na binti kujitunza ni kubwa sana. Mwanamke ukijichukulia kwamba wewe ni mama huruma wenzako watakuchukulia kwamba wewe ni dambo la kutupia takataka zao.
Mwanamke ni muhimu sana kujitunza kimwili na kiroho. tunza uhusiano wako na BWANA YESU maana huo utakufikisha uzima wa milele. tunza mwili wako na tunza utu wako. Mtumainie MUNGU na sio wanadamu.
Zaburi 146:3 '' Msiwatumainie wakuu, Wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake. ''

    7. Mwanamke Jilinde na linda familia yako.
-Mwanamke lazima ajilinde kwa maombi.
-Mwanamke lazima ailinde familia yake kwa maombi.

Yeremia 31:22 '' Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume. ''
-Maombi ya wamama yana nguvu sana. Kama mama anadhani mlinzi wa familia yake ni mmewe naomba ajue kwamba ulinzi wa MUNGU ndio muhimu zaidi na ulinzi huo huja kwa maombi hivyo ni jukumu la kila mwana familia akiwemo mama kuilinda familia na kujilinda mwenyewe kwa maombi. 
hata kutokutoka nje ya ndoa pia ni kuilinda ndoa yako.
Kumbukumbu 23:9 '' Utakapotoka kwenda juu ya adui zako nawe u katika marago, jilinde na kila neno baya. ''
 
   8.  Mwanamke Jikomboe na uukomboe wakati

Mimi Peter natokea katika jamii ambayo zamani binti akikaribia kumaliza darasa la saba anaweza kuambiwa ajifelishe ili akimaliza tu shule aolewe, wazazi wapate ng'ombe.
-Tumia fursa njema vizuri ili ujikomboe.
-Jikomboe kutoka kwenye maagano mabaya ya familia, jikomboe kutoka kwenye utumwa na jikomboe kutoka kwenye utegemezi. Kumbuka MUNGU ni wa wote hivyo kama kuna wanaoomba ili wapate kazi na wewe omba na usikate tamaa maana muujiza wako upo tu kama ilivyotokea kwa wengine.
-Komboa wakati kwa kuishi maisha mataktifu.
Ukomboe wakati kwa kuifanya kazi ya MUNGU.
Waefeso  5:17 ''Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya BWANA.''


    9. Mwanamke Jisahihishe.
-Mwanamke jisahihishe kwa kuacha kuvaa nguo zinazokudhalilisha na kuanza kuvaa nguo za heshima. kama kuna sehemu ambapo wamama wengi wamefeli ni kwenye mavazi. huwa najiuliza, kwa sababu kila mtu duniani anajua kwamba kuna nguo za heshima na nguo ambazo sio za heshima, kwanini wanawake walio wengi hupnda zaidi kuvaa nguo ambazo sio za heshima?
Kuna wadada hawana nguo za heshima hata moja huko wakijua kabisa kwamba jambo hilo halina faida hata moja kwao.
-Kwenye mavazi Hapa ndipo walipofeli wengi lakini mimi naomba kila anahyehusika na kuvaa nguo zisizo za heshima basi ajisahihishe kutoka kwa wamama wanaovaa kiheshimu maana wapo wengi tu. habari za kusema kwamba MUNGU anaangalia rohoni tu na sio mwilini hizo naomba kila mmoja ajue kwamba habari hizi zinatoka kwa shetani na sio kwa MUNGU.
-Wamama wengi huwa hawapendi kujifunza mambo mazuri kutoka kwa wamama wengine, wengi huiga staili za nywele tu lakini kuiga tabia nzuri kwa wamama walio na umri mkubwa ambao wengi huvaa nguo za kubariki, wanaojifunza kwao ni wachache sana.
MUNGU ni utakatifu hivyo ukiukataa utakatifu na MUNGU anakuacha.
Warumi 1:26 ''Hivyo MUNGU aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; ''

      10. Mwanamke jipende.
-Mwanamke lazima ajipende kwanza yeye ndipo na watu wengine watampenda.
-Kama hujipendi usitarajie kupendwa na wengine.
-Sifa namba moja ya mwanamke kujipenda ni kumcha MUNGU ndio mengine yanafuata.
-Mwanamke anayejipenda huheshimiwa.
Mithali 11:16a ''  Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima;. ''
Namani niseme mengi sana lakini naamini kwa leo inatosha.
jambo la mwisho ni hili.
Ndugu Yangu, Usikubali Kumkana YESU Na Hakikisha Unajikana Ili Umpendeze MUNGU.
Usitende Dhambi Maana Kutenda Dhambi Ni Kumkana BWANA YESU.
Ukidumu katika mema bila kumkana YESU utafanya vyema.
Yeye BWANA YESU anasema '' Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. -Yohana 10:28 ''

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana.
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
Mr na Mrs Peter Mabula.
.

Comments