PAPA FRANCIS ALEGEZA MASHARTI YA NDOA.

H1
Papa Francis
Uamuzi wa Papa Francis kulegeza masharti ya utaratibu wa kubatilisha ndoa kwa waumini wa kanisa hilo umepokewa kwa hisia tofauti.

Uamuzi wa kuondoa urasimu katika ubatilishwaji wa ndoa ulitangazwa juzi na makao makuu ya Papa. Kesi zinazohusu maombi ya ubatilishaji ndoa sasa zitachukua muda mfupi zaidi na mchakato wake hautakuwa na urasimu kama ilivyokuwa awali.

Baadhi ya viongozi wa kanisa hilo na waumini waliozungumza na Mwananchi wameupongeza uamuzi huo kuwa unazingatia mazingira halisi ya kanisa hilo kwa sasa.

Askofu msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini ameueleza uamuzi huo kuwa utaharakisha utendaji wa kazi za kanisa kwa kupunguza muda wa kusikiliza mashauri hayo na kuyapatia ufumbuzi. “Ni uamuzi mzuri unaoonyesha kwamba kiongozi huyo ana imani na maaskofu wake,” alisema Askofu Kilaini

Kwa upande wake, Padri Evodius Nachenga wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam alieleza kuwa kwa uamuzi huo, matatizo baina ya wanandoa yatakuwa rahisi kupatiwa mwafaka.

Mlei mmoja, John Lipingu alisema kuwa ni hatua nzuri kwa kuwa kanisa hilo limeangalia sheria na kanuni ambazo zimetumika karibu miaka 2,000 ambazo zimekuwa haziendani na hali halisi.

Juzi, Papa Francis kupitia jopo la wataalamu wa sheria za kanisa na theolojia alipitisha sheria inayolegeza masharti ya kubatilishwa kwa ndoa, ambayo yamekuwa yakitumika tangu mwaka 1908.

Sheria hizo, ambazo zilipitishwa mwaka 1740 zimekuwa zikitaka masuala hayo kujadiliwa kwa ngazi ya jimbo, kupitia mahakama maalumu ya kanisa hilo, kisha mapendekezo kufikishwa makao makuu ya kanisa hilo, Vatican kwa uamuzi.

Hata hivyo, gharama za kufikisha shauri husika Vatican zilikuwa kubwa na utaratibu huo ukichukua muda mrefu na kuwaathiri wanandoa ambao wengine walikosa fedha za kufanya hivyo.

Comments