TALAKA DUME INAVYOTESA NDOA NYINGI.

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU apewe sifa ndugu.
Karibu tujifunze. 
Mwalimu leo nina ka ujumbe ka tofauti kidogo.
Baada ya Baba mzazi kufariki tarehe 20/7/1990 nikiwa na miaka 3  na nusu, Mama alituacha na nikaja kumuona miaka 10 baadae ikiwa ni miezi 2 kabla ya kifo chake. Na mama nilimuona kwa masaa Machache tu kisha sikumuona tena hadi kifo chake lakini siku nilipomuona tuliongea vitu vya miaka 10, na ilikuwa siku ya kipekee kwangu.
Baada ya  Baba kufariki na sisi tukatengana na mama, tulichukuliwa na Bibi na kwenda kuishi kwake Kibehe Wilaya Chato, tulizoea Mwanza mjini lakini sasa maisha yalikuwa kwingine baada ya kifo cha Baba. Huko Kibehe tuliishi Babu na Bibi pamoja na sisi wajukuu.  Lakini kila siku ambapo Babu alikunywa pombe basi nyumbani kulikuwa na mapigano maana pombe ilipelekea babu kumpiga bibi na kupelekea familia nzima kulia sana, Bibi akilia na wajukuu wote tulilia. Maisha ya ndoa ile yaliharibiwa na pombe. Je umejifunza nini? Leo nazungumzia talaka dume.
 Yokobo 4:1 ''Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu?''
-Vita vinatoka wapi?
Vita haiji bila chuki kwanza kuja, ukiidhibiti chuki , vita hutaiona kamwe.
Chuki huzaa vita na tena chuki katika ndoa inaweza kuzaa talaka, na kama talaka haitakuwepo kwa sababu hairuhusiwi talaka kutoka basi kutakuwa na talaka dume, na ndio hiyo leo nimeguswa kuizungumzia, maana kuna ndoa itaenda kupona kupitia ujumbe huu.
Talaka Dume Inawatesa Wanandoa Wengi. 
Talaka Dume Ni Kitendo Cha Wanandoa Kuishi Kwenye Ndoa Yao Bila Umoja Wala Upendo, Wanaishi Nyumba Moja Ila Kila Mtu Analala Chumba Chake, Au Chumba Kimoja Ila Vitanda Tofauti, Au Kitanda Kimoja Lakini Kulala Ni Karata Mzungu Four.

1 Kor 7:10-11 '' Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila BWANA; mke asiachane na mumewe; lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.''
-Amri  ya MUNGU ni kwamba wanandoa wasiachane?
Ikiwa wamefikia hatua ya kuachana basi kila mmoja asitafute mwingine na kama kila mmoja ataona hawezi kuishi bila mwenzi basi warudiane wao na sio kutafuta kwingine.
Kutafuta kwingine ni  dhambi na ni kuukimbia uzima wa milele. 

Zipo sababu 2 zinazoweza kuwatenganisha wanandoa;

1. Kifo ( 1 Kor 7:39 '' Mwanamke hufungwa maadamu mumewe yu hai, lakini ikiwa mumewe amefariki, yu huru kuolewa na mtu ye yote amtakaye; katika Bwana tu. '') 

2. Uzinzi (Mathato 19:9 ''  Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini. '' )

-Hizo ndizo sababu 2  za Kibiblia ambazo zinaweza kuwatenganisha wanandoa lakini pia ni muhimu kujua kwamba Biblia inaagiza kusamehe saba mara sabini kwa siku moja. Luka 17 :4 ''  Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.''  
Licha ya kuambiwa samehe saba mara sabini naamini hata ukiambiwa msamehe huyo unayetaka kumpa talaka basi hakika utamsamehe maana agizo ni kwamba usamehe. lakini pia wengi hujisifia kutoa talaka lakini Biblia inatuamuru tusameheana saba mara sabini kwa siku lakini pia ni muhimu kukumbuka kwamba usiposamehe na wewe hutasamehewa na MUNGU. Mathayo 6:14- 15 ''Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na BABA yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala BABA yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.''
Kumbe kujidai kutoa talaka kwa sababu hutaki kusamehe inaweza kukuingiza jehanamu vilevile.
Lakini pia wewe ambaye umeshindwa kujiheshimu hadi unataka kupewa talaka unataka nini zaidi? lini utajitambua na kujidhamini?
 Unaleta makwazo kwa mwenzi wako, kwanini? 
Mathayo 18:6-7 '' bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari. Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini ole wake mtu yule aliletaye jambo la kukosesha! '' 
-Usione raha kuwakosesha wengine maana ni machukizo kwa MUNGU.
Talaka dume leo zimejaa.
Ni kama wana ndoa hao wameachana ila tu bado talaka.
Kuna ndoa mama ana mambo yake na baba pia ana mambo yake, kila mtu kivyake.
Kuna ndoa kila mhusika anasema '' tusijuane''
Kuna ndoa kila mhusika wa ndoa hiyo anasema '' najuta kukufahamu''
Vita vya toka wapi?
Waefeso 5:28-31 '' Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama KRISTO naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. '' 
-Agizo la MUNGU ni wanandoa wapendane kama Biblia inavyosema kwenye andiko hapo juu lakini ndoa nyingi leo hazina upendo.
-Kuna ndoa kuna mashariti mengi na magumu kuliko mashariti ya kuomba mkopo benki.
-Kuna ndoa kuna manyanyaso kuliko gerezani.
Vita vya toka wapi?
Hawa ni kama wametalikiana maana zile habari za mwili mmoja hazipo tena, upendo wa kwanza umepoa, furaha hamna, shetani anawamiliki na kila mmoja hata hataki kumtafuta BWANA YESU ili aifufue ndoa yao kama alivyomfufua Lazaro lakini kazi imebaki kulaumiana na kujuta tu.

 Hiyo Ni Talaka Dume.
 Kila Siku Kutukanana Na Mafarakano.
Kila Siku Ni Kunyosheana Vidole Na Kuogopana Kama Polisi Na Mwizi.
Hiyo Ni Talaka Dume Yaani Ni Kama Mmetalikiana Hata Kama Mnaishi Pamoja. 

Ndugu, Je Uko Kwenye Talaka Dume? 
Biblia Inasema Hakuna Kuachana Mpaka Kifo Kiwatenganishe
(1 Kor 7:10- Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila BWANA; mke asiachane na mumewe;
Tena "Mume Ampe Mkewe Haki Yake, Na Vivyo Hivyo Mke Ampe Mumewe Haki Yake-1 Kor 7:3.''
  Tena Ndoa Na Iheshimiwe Na Watu Wote, Kuanzia Wanandoa Wenyewe Hadi Watu Wa Nje
(Waebrania 13:4,Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.).

 Je Unataka Kuiponya Ndoa Yako? 
Je Unataka Kuirudisha Katika Hali Safi Ndoa Iliyokufa? 
-Ndugu, Tubu Kwa Ajili Ya Ndoa Hiyo
Luka 13:3 '' Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. '' 
-Karibia Kiti Cha Rehema Cha BWANA YESU
Waebrania 4:16 '' Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.   ''.
- Anayeweza Kuiponya Ndoa Yako Na Kirudisha Kwenye Furaha Ni YESU Pekee.
BWANA YESU anasema
Mathayo 11:28 '' Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.''

 Upendo Wa Kweli Haushtaki Wala Kulaumu Bali Hupigana Wenyewe Ili Kuhakikisha Mambo Mazuri Yanabaki Pale Pale.
Kama upendo wa kweli haupo basi talaka dume itatawala.
Ndugu, kuiponya ndoa yako ni jambo ambalo linawezekana kabisa na tena ni jambo rahisi sana kwa MUNGU katika KRISTO YESU.
Iponye ndoa yako kwa kumkimbilia BWANA YESU ili akuokoe na aiokoe na ndoa yako.

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments