BAADA YA KUOKOKA UNATAKIWA UFANYEJE?


BWANA YESU atukuzwe sana ndugu yangu.
Karibu tujifunze neno la MUNGU.
 Waefeso 2:8 '' Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU;''
Baada ya kuokoka sikuwa najua natakiwa nifanye nini katika kazi ya MUNGU. Lakini kupitia kujifunza Neno la MUNGU kila mara niligundua kwamba BWANA YESU hakuniokoa ili nikae tu kanisani bali niitende kazi yake. Nilijiona nina jukumu kubwa la kuwaambia ndugu zangu ili waokoke.
Nilivyokuwa nafundishwa neno la MUNGU ndivyo nilivyoanza kuijiwa na huruma sana kwa ajili ya ndugu, rafiki zangu na kila mtu. Hakika nilijua nina kazi kubwa sana ya kuwaambia watu wote waje kwenye ufalme wa MUNGU.
Nilipokuwa nafundishwa kwamba wachawi hawawezi kuurithi ufalme wa MUNGU, Niliwakumbuka baadhi ya watu ambao walikuwa wanatuhumiwa kwa uchawi ninaowafahamu.
Nilipogundua kwamba wazinzi wa walevi hawataurithi ufalme wa MUNGU niliogopa na kujua kabisa nina jukumu kubwa sana la kuhubiri injili maana nusu ya ndugu zangu na marafiki walikuwa wahusika wa dhambi hizo.
Sikuwa najua sana Biblia na nilitamani mtu anifundishe jinsi kuwaeleza wanadamu na wakanielewa.
Lakini kudumu katika neno na katika fundisho ndiko kulikonipa mwanga na pa kuanzia.
Huyo ni mimi kipindi naokoka. Hakuna mtu anayeokoka kwa bahati mbaya, ila kila mtu anaokolewa na BWANA ili alitimize kusudi la MUNGU.
Je, unajua unatakiwa ufanyeje baada ya kuokoka?

Baada ya mtu kuokoka anatakiwa afanye yafuatayo.

       1. kuwa anakusanyika na wengine kanisani.
Waebrania 10:25 '' wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.''
-Katika kukusanyika kanisani, huko tunajifunza kila jema ambalo tunatakiwa kuliishi.
-Katika kukusanyika kanisani huko tunakuwa kiroho na kuimarika kiimani.
Ni muhimu sana kukusanyika pamoja kanisani.


       2. Ajazwe nguvu za ROHO MTAKATIFU.
Matendo 1:8 ''Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu ROHO MTAKATIFU; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.''
-Kabla BWANA YESU hajaondoka kwenda mbinguni, alitangaza ujio wa  ROHO MATAKATIFU, ambaye atakaa ndani yao wateule siku zote.
Ahadi ya ROHO MTAKATIFU ni ya kila Mkristo ambaye anaokoka. Hivyo kila anayeokoka anatakiwa kufanya juhudi za kiroho ili ajazwe nguvu za ROHO MTAKATIFU.

       3. Autafute ufalme wa MUNGU na haki yake.
Mathayo 6:25-33 '' Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na BABA yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti
nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa MUNGU huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu BABA yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.''

-Ufalme wa MUNGU ndio muhimu zaidi kwa kila mkristo.
-Ufalme wa MUNGU hutafutwa, kupaliliwa na kujengwa. Kazi za kutafuta, kupalilia na kujenga vyote viko kwa mwamini, Hivyo ni muhimu sana mwamini mpya kujua umuhimu wa kuweka kipaombele chake cha kwanza kwamba ni ufalme wa MUNGU tu.

       4. Amtumikie MUNGU.
Yohana 12:26 '' Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, BABA atamheshimu.''
-Kumtumikia YESU ni kujikana, kuichukia dunia ili umpate KRISTO aliye na uzima wako wa milele.
-Wakristo wote wanatakiwa kuwa watumishi wa MUNGU.
Kila anayeokoka anatakiwa ajue kwamba utumishi wake kwa MUNGU ni wa muhimu sana.
-Ukimtumikia BWANA YESU hakika MUNGU BABA atakuheshimu. ukiheshimiwa na MUNGU una heri wewe, ukiheshimiwa na MUNGU hakika utapata neema kuu ya MUNGU.

       5. Awe na umoja na kanisa.
Yohana 17:11 '' Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. BABA mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.''
-YESU KRISTO na BABA yake wana umoja wa kipekee, na umoja huo inatakiwa na wateule wa wake wawe na umoja.
-Umoja katika kanisa ni muhimu sana, hivyo Mkristo Mpya aliyeokoka siku za karibuni anatakiwa kujua kwamba kwamba umoja ni nguvu ya kanisa, umoja ni silaha ya kumshinda shetani na mawakala wake.
-Huwezi kuwa mwanakanisa mzuri harafu ukawa huna umoja na kanisa.
Kanisa ni watu wamoja wanaotakiwa kuifanya kazi ya MUNGU kwa umoja, hivyo ni jukumu la mwamini mpya kujiunga katika umoja wa kanisa kwa ajili ya kuitenda kazi ya MUNGU.

       6. Awe kielelezo cha mambo mema.
 1 Timotheo 4:12 '' Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.''
-Ni muhimu sana kujifunza kuwa kielelezo katika usemi na mwenendo wako.
-Tabia njema ni kielelezo kizuri, usafi wa mwili na roho ni kielelezo kizuri hivyo mwamini mpya lazima ajifunze kuwa kielelezo.

       7. Awe kiumbe kipya kisichofuata tena ya zamani.
2 Kor 5:17 '' Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.''
-Kuwa kiumbe kipya ni kuachana na kila uovu wa zamani kabla hujaokoka.
-Kiumbe kipya kiroho ni mtu aliyebadili mfumo wake wa maisha kutoka kuishi maisha ya dhambi  kuanza upya kuishi maisha matakatifu yanayoelekezwa na neno la MUNGU.

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke.
Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

0714252292.
mabula1986@gmail.com

Comments