HATARI ZA MAISHA


Na:     BRYSON LEMA (RP)        &
Dr. GODSON I. ZACHARIA (SNP)
Utangulizi: Paulo alikuwa anamwamini Bwana Yesu kama na wewe unavyomuamini. Paulo alikuwa mwanadamu kama wewe ulivyo. Hata hivyo iliifika wakati ambapo alijiuliza swali, kama ambavyo imeandikwa katika  1KORINTHO 15:30…[Na sisi, kwa nini tumo hatarini kila saa?]…Ndani ya maisha kuna hatari. Kama wewe hadi leo hujaweza kujua kwa nini unakuwa hatarini, hutaweza kufanikiwa. Hayupo aliyeyaongea mambo ya  maisha kama Paulo (Mfano aliongelea jela, njaa, dhiki n.k.). Paulo  anapoongelea hatari ni kwa sababu yeye pia ni mtu wa hatari. Hauwezi kushinda kama haupo tayari kupitia shida, hatari na magumu ya maisha.
Kwa macho tu ni mbaya sana kuangalia hatari za maisha.Lakini baada ya hatari ujue yapo mafanikio. Yeremia naye aliliona hili. Imeandikwa katika MAOMBOLEZO 5:9…[Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu; Kwa sababu ya upanga wa nyikani.]…. Hatari zipo kila siku kwa sababu hakuna aliye tayari kukuona wewe unafanikiwa na kusonga mbele. Mafanikio ya mwanadamu wa leo ni ya yule aliye tayari kuingia katika hatari. Hii ni kwa sababu kile ninachotaka kukipata, ni lazima nijihatarishe.
Shetani anakuona wewe ni hatari pale unapoanza kudai afya yako, watoto wako, uponyaji wako, mali zako n.k.  Ni rahisi sana kumtia moyo "mtu anayetoa uhshuhuda wake" kwa kumwambia hongera, lakini unasahau kumuuliza siri ya mafanikio yake.  Ndiyo maana Biblia inasema kuwa Eliya alisema “mvua haitanyesha ila kwa neno langu” na ikawa hivyo. Ukisoma katika Agano Jipya, Biblia inasema “Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi akaomba kwa bidiii na mvua haikunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu”. Daudi hakuvumilia kumuona Goliath akilitukana Jina la Bwana. Kwa siku moja tu, Daudi alimsikia Goliath akitukana na kuchukua hatua kwenye ile hatari, wakati wale Israeli walimsikia Goliath akitukana kwa siku zote 40 mfululizo bila wao kuchukua hatua yoyote, kwa kuogopa hatari.
Hatari zipo, lakini kuna baraka katika hizo hatari. Kuna kujiingiza katika hatari ili uweze kutoka hapo ulipo. Kumbuka Samsoni alimuua simba, Na baada ya siku ile Samsoni alijipatia asali ndani ya mzoga wa simba yule yule.
KUTOKA 13:18-21…[ lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha. 19 Musa akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajilia ninyi; nanyi mtaichukua mfupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi. 20 Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa ile jangwa. 21 Bwana naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; ]…. Hapo ulipo unatakiwa  kutoka na kuufuata ushindi wako pale ulipo. Nyakati zingine watu hawajui njia za kulibeba andiko na kulifanya liwe  lao. Wana wa Israeli hawakupigana wakiwa Kanaani. Wana wa Israeli walipokuwa Kanaani, hawakupigana na badala yake waliuzunguka ukuta wa Yeriko.Walipokuwa nyikani, Wana wa Israeli walipambana na Mfalme Ogu, na baada ya kumuua waliweza kusonga mbele.  Wakiwa nyikani walipambana na nyoka wa jangwani na ili kupona, iliwabidi waingalie sanamu ya nyoka wa shaba‼‼
Unapojiona wewe ni mgonjwa, ujue una tatizo. Kila ugonjwa una chanzo chake. Kila tatizo pia kwenye maisha yako lina mwanzilishi aliyelileta hilo tatizo.

1 SAMWELI 14:1-10…[Basi ikatukia siku moja, ya kwamba Yonathani, mwana wa Sauli, akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na tuwavukie Wafilisti ngomeni, pale ng'ambo ya pili. Walakini hakumwarifu babaye. 2 Naye Sauli alikuwa akikaa katika upande wa mwisho wa Giba, chini ya mkomamanga ulioko kwenye uga; na hao watu waliokuwa pamoja naye walipata watu mia sita; 3 na Ahiya, mwana wa Ahitubu nduguye Ikabodi, mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Bwana huko Shilo, mwenye kuvaa naivera. Tena hao watu hawakujua ya kwamba Yonathani ameondoka. 4 Na katikati ya mianya, ambayo Yonathani alitaka kuipitia ili kuifikilia hiyo ngome ya Wafilisti, palikuwa na genge la jabali upande huu, na genge la jabali upande huu; jina la moja liliitwa Bosesi, na jina la pili Sene. 5 Hilo genge moja limesimama upande wa kaskazini, mbele ya Mikmashi, na hilo la pili upande wa kusini, mbele ya Geba. 6 Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na twende tukawavukie ngomeni hao wasiotahiriwa; yamkini Bwana atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia Bwana asiokoe, kwamba ni kwa wengi au kwamba ni kwa wachache. 7 Naye huyo mchukua silaha akamjibu, Fanya yote yaliyomo moyoni mwako; angalia, mimi hapa ni pamoja nawe, moyo wangu ni kama moyo wako. 8 Ndipo Yonathani akasema, Tazama, sisi tutawavukia watu hawa, na kujidhihirisha kwao. 9 Nao wakituambia hivi, Ngojeni, hata sisi tuwafikilie; ndipo tusimame pale pale mahali petu, tusiwapandie. 10 Lakini wakisema hivi, Haya! Ninyi, tupandieni sisi; hapo ndipo tutakapopanda; kwa maana Bwana amewatia mikononi mwetu; na hii itakuwa ndiyo ishara kwetu.]… Yonathani anatukumbusha kuwa hakuna cha kumzuia Bwana kutenda;  Iwe ni  kwa wengi au  kwa wachache. Yonathani alikuwa anaijua ishara na sauti ya watu waoga.
Kila anayeingia katika safari yangu lazima apigwe nyundo. Haijalishi huyu mzuiaji ni  nani!!!. Yesu Kristo alikuwa na uhakika wa kufika ng’ambo ya Bahari,  na ndiyo maana alilala usingizi wakati ule merikebu inapigwa na mawimbi kona zote.  Leo hii tunamsoma Goliath kwa sababu ya Daudi. Mwisho wa Kitabu cha Samweli, Biblia inawataja mashujaa 320 wa Daudi ambao ni wale watu waliokuwa na madeni, wenye dhiki na kila aina ya adha.
UKIRI
Baba Mungu, leo nakataa kurudi nyuma, nakataa vitisho vya adui zangu, kila mamlaka za giza zinazokaa ili kunitisha, leo nazisambaratisha kwa Jina la Yesu. Ewe adui uliyesababisha vita hii, nakufuata, wewe na wajumbe wako na kila  mtu aliyekaa na wewe. Leo nafanya vita na kila vuruugu, kila adui na ninaanza kuwapiga kwa Jina la Yesu, mliokaa ili kuniletea vita leo nawasha moto  kwa Jina la Yesu. Amen.
Usioogope aliyekupiga vita au kusimama mbele yako. Kama upo na hujaokoka kwa kumpokea Yesu Kristo maishani mwako,leo ni fursa muhimu  ya kumwamini Yesu Kristo ili  aweze kukushindia yote.

Comments