KWA IMANI IBRAHIMU ALIPOITWA ALIITIKA.


Na Mchungaji Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe…
Tunayo mengi ya kujifunza pindi tusomapo habari za Ibrahimu baba yetu wa imani  (Warumi 4:16),lakini kubwa la kujifunza ni imani kuu aliyokuwa nayo pale alipoitwa na Mungu atoke katika nchi yake na kuelekea kule alipoambiwa na Mungu ( Mwanzo 12:1-5 )
 Ili uweze kuitika,basi ni lazima usikie maana huwezi kuitika pasipo kusikia sauti iliyokuita. Hii ni kanuni moja ya kawaida kabisa,na tunaona mfano mzuri kwa Samueli alipoitwa na Bwana alisikia lakini hakuweza kuitambua sauti ile kwa haraka kwamba ni Bwana Mungu ndie asemaye au nabii wake Eli? Lakini kusikia alisikia ndio maana aliweza kuitikia. ( 1 Samweli 3 :4 )

Kwa habari ya Ibrahimu,yeye naye alisikia sauti ya Bwana Mungu na kuitambua kwa sababu alikuwa na ushirika mzuri na Mungu wake. Kwa lugha nyepesi ni hivi kama mtu hana mahusiano mazuri au ushirika na Bwana basi anaweza kuisikia sauti ya Bwana Mungu lakini ikamchanganya kuijua ndio yenyewe au lah! Au anaweza hata asiisikie kabisaa! Hii ndio mbaya kweli kweli.
Sasa fikiria kwamba kama Ibrahimu asingekuwa na ushirika na Bwana wake,je unafikiri angeliweza kuisikia sauti ya Bwana na kutii? Hivyo utagundua kwamba Ibrahimu alikuwa na imani kubwa sana sababu alikuwa akiisikia sauti ya Bwana maana chanzo cha imani ni kusikia ( Warumi 10:17 )

 Mtu mwenye imani haba yule asiyeweza kuisikiza sauti ya Bwana Mungu kwa makini,kamwe hawezi kuwa na imani tena hawezi kuwa mtiifu wa Mungu. Mtu wa namna hii ajaposemeshwa na Bwana yeye siku zote hujua ni pepo anasema naye hivyo atua yake ya kwanza ni kuanza maombi ya kuvunja na kubomoa huku akiwa amefunga sababu hameshindwa kuijua sauti ya Mungu ni ipi na sauti ya shetani ni ipi.

Sasa jiulize ni mara ngapi umefanya maombi ya namna hiyo kupingana na sauti ya Mungu? Maana ipo wakati ambapo ni Mungu mwenyewe anasema nawe labda kuhusu utoaji,au kuhusu kuongeza utoaji wako,au anasema nawe kuhusu kumsaidia asiyejiweza kimaisha, kulimlipia karo ya shule, au hata kuwategemeza watumishi wa Mungu kwa upana zaidi ~ Lakini hata hapo umeingia kuvunja na kuteketeza sauti hiyo ya Mungu.

Tena wengine wamesikia sauti ya kuingia katika utumishi wa Mungu lakini wameiharibu sauti hiyo ya Mungu wakidhani ni shetani anasema nao,kumbe ni Mungu mwenyewe.Biblia haisemi kwamba Ibrahimu aliikemea sauti ile kwa kuomba maombi ya kuvunja na kuharibu,bali aliisikia na kuitii kwa sababu alikuwa akijua fika ni Mungu anayesema naye.Tazama tunasoma ;
Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;” Mwanzo 12:1~Ukisoma zaidi utakuta Ibrahimu akitii na kufanya yale aliyoelekezwa na Bwana wake.
Iko dhana potofu iliyosambaa akilini mwa watu wengi katika andiko hilo hapo juu kwamba watu hudhania kwamba Ibrahimu alipoitwa aliondoka yeye peke yake. Ukweli ni kwamba alipoondoka hakuwa peke yake bali alitoka yeye,mkewe Sara,mwanaye Lutu ( mtoto wa Harani nduguye )pamoja na watu aliowapata huko harani sawa sawa na kilichoandikwa katika Mwanzo 12:4-5

 Hii ikiwa na maana kwamba uendapo kwa Bwana basi usikwende peke yako bali chukua na mke/mme wako,chukua na familia yako kama vile asemavyo Yoshua ” … lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana.” ( Yoshua 24:15 ) isipokuwa kwa habari ya wito tu,ndio unapaswa uende wewe kama wewe. Yapo mambo mawili ambayo Ibrahimu aliyafanya pale alipoisikia sauti ya Bwana.
Kwanza aliitika wito wake, ambao huo ulikuwa unamuhusu yeye peke yake lakini pili alichukua watu wake wakaribu akaenda nao katika wito alioitiwa.Leo,mtu aweza kuitwa na Bwana katika huduma fulani na ukashangaa akatoka yeye peke yake pasipo mume/mke wala familia yake!!!  Hii inaonesha mawili,inawezekana mtu huyo hajui tofauti ya kile alichoitiwa na huduma kwa ujumla,Au inawezekana anajua ila anakaidi.

Ibrahimu aliweza kutofautisha kati ya wito wake na huduma,maana wito ulikuwa wake mwenyewe lakini huduma ilikuwa pamoja na watu wake. Ikumbukwe kwamba,baada ya Ibrahimu kutoka katika nchi ya baba yake,ndiposa anaanza kumjengea Bwana madhabahu jambo hili likiwa na maana kwamba sasa alikuwa akitembea katika wito. Imani na utii aliokuwa nao Ibrahimu,ilimuwezesha kutoka katika nchi yake na kwenda alipoelekezwa ambapo hata yeye mwenyewe alikuwa hapajui maana imeandikwa;
” Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.” Waebrania 11:8.Jambo moja tunaloweza kujifunza siku hii ya leo ni kwamba Ibrahimu alikuwa akimuabudu Mungu wa kweli ( Abram was a worshiper of a true God ) maana imeandikwa ;
Yoshua akawaambia watu wote, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Baba zenu hapo zamani walikaa ng’ambo ya Mto, maana Tera, baba yake Ibrahimu, naye ni baba yake Nahori; wakaitumikia miungu mingine. “Yoshua 24:2.

Biblia inaweka wazi juu ya baba yake Ibrahimu na akina Nahori ndugu wa kunyonya wa Ibrahimu kwamba waliitumikia miungu mingine isipokuwa Ibrahimu ambapo neno halisemi kwamba Ibrahimu aliitumikia miungu bali yeye alimtumikia Mungu wa kweli. Kumbe miungu ya Tera na nduguze iliwazuia kusikia sauti ya Mungu wa kweli,na kwa sababu hawakuweza kusikia basi hawakuwa na imani ya kweli.

Hata wewe ~ yamkini ipo sauti ya Mungu uliyoizuia kwa sababu ya miungu unayoiabudu kama vile akina Tera walivyofanya. Wapo watu wengine kwa sababu ya kungangania mahali pa mapokeo ya kidini,wameshindwa kuisikia sauti ya Mungu wa kweli. Ikiwa unamuabudu Mungu wa kweli basi utaisikia sauti yake maana hata neno linasema walio wake anawajua. 

 Kuachana na mapokeo ya kidini yasiyofaa sio dhambi. Wala kuiacha miungu sio dhambi hata kidogo,bali dhambi ni kungangana kuitumikia miungu na kuendelea kutembea katika sheria ya mapokeo ya dini fulani ambayo hata wewe mwenyewe hujui maana ya hayo mapokeo. Mtu wa namna hii,ni vigumu kabisa kuisikia sauti ya Bwana Mungu wake na hata akisikia bado atazani ni pepo. 
Kwa mfano wa Ibrahimu jifunze mpendwa,utoke mahali ambapo kuna miungu au ibada ya miungu mfano ibada za sanamu,mfano kuwa chini ya sheria mahali ambapo hata Roho mtakatifu hayupo hapo. Haijalishi baba na mama yako wanaabudu wapi,bali angalia sana wewe unaabudu kitu gani,na wapi? Siku hii ya leo nahitaji nifanye maombi na wewe mpendwa katika Kristo Yesu.
Waweza sasa kunipigia kwa namba yangu hii 0655111149.
Mchungaji Gasper Madumla.
Beroya bible fellowship church ( Kimara baruti,Dar TZ )
UBARIKIWE.

Comments