![]() |
Askofu Niwemugizi |
Wakati zikiwa zimesalia siku kadhaa kwa Tanzania kufanya uchaguzi mkuu,
baadhi ya makanisa nchini Tanzania yametoa ruhusa maalum kwa viongozi wa
kanisa kuendesha ibada zao Jumamosi Oktoba 24 badala ya Jumapili tarehe
25 ili kutoa nafasi kwa waumini wao kushiriki shughuli kubwa ya upigaji
kura.
Makamu wa rais wa Baraza la maaskofu katoliki Tanzania (TEC), Askofu
Severin Niwemugizi, amesema kuwa ibada haipaswi kuzuia haki ya kimsingi
na kikatiba ya waumini .
“Si utaratibu wa kawaida kwa sababu kama baraza hatujakaa, lakini kila
askofu anawajibika ndani ya jimbo lake, hivyo anaweza kutoa fursa hiyo.
“Hata mimi katika jimbo langu la Rulenge Ngara, nimetoa kibali hicho kwa makanisa yote,'' amenukuliwa akisema Askofu Severin.
Hadi sasa tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1961 imeongozwa na
marais wanne, wa kwanza akiwa baba wa taifa hilo Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, akafuatiwa na Al Haji Hassan Mwinyi, baadaye Benjamin
William Mkapa.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete anayeelekea kukamilisha muhula wake wa pili
atampisha rais wa tano kuchukua madaraka mwishoni mwa mwezi huu wa
Oktoba.
Comments