MATENDO YAKO YATAONYESHA KULE UTAKAKOKUWA SIKU YA MWISHO.

Na Mtumishi Peter M Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mara nyingi huwa natamani nifundishe Neno la kuwafariji watu, au kuwaimailisha kiroho, au kuwatia moyo.  lakini agizo la MUNGU ambalo lipo kwa sasa kwangu ni kuwaambia watu ukweli ili wakipenda kuchagua uzima basi uzima wa milele uwe wao.
Kwanini kunahubiriwa sasa habari za uzima wa milele?
Ni kwa sababu siku ya BWANA i karibu sana.
Isaya 13:9 ''Tazama, siku ya BWANA inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.'' 

Siku ya BWANA ndio siku ya mwisho, ndio siku ya hukumu, ndio siku ya kiama kama baadhi wanavyoita.
 Ni siku ya mahesabu na hakutakuwa na kutubu siku hiyo, maana muda wa kutubu kila mwanadamu amepewa atubu akiwa hai duniani, ndio maana injili kama hii inahubiri leo.
BWANA YESU atakuja siku hiyo na kuwahukumu wanadamu wote na wa dini zote.
Kama ulimtambua BWANA YESU kama mtu tu, siku hiyo ndio utamjua kwamba yeye ni MUNGU mwenyezi.
Ufunuo 1:7-8 '' Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema BWANA MUNGU, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.''

Siku hiyo kila mwanadamu aliyepata kuishi duniani atafufuka na kulipwa sawasawa na matendo yake ya kipindi anaishi, hakuna atakayekosekana hata mmoja.

Siku hiyo Ya Mwisho Watu Watabeba Mizigo Yao Ya Dhambi. Unajua Kwanini Watabeba Mizigo Yao? 
Ni Kwa Sababu Wameshindwa Kuitua Sasa Mizigo Hiyo. 
Sehemu Ya Kutua Ni Moja, Ni Kalvari. 
Unatua Mzigo Kwa Kumpokea BWANA YESU Na Kutubu Na Kuanza Kuishi Maisha Matakatifu Ya Wokovu. 
Matendo 3:19 '' Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA; '' 

Ndugu, Peleka Dhambi Zako Golgotha Na Utatoka Huru, Na Ishi Maisha Ya Wokovu Wa BWANA YESU, Siku Hiyo ya Mwisho Wewe Hutakuwa Na Mzigo Bali Utakuwa Unang'aa Kama Jua.
 Danieli 12:2-3 ''Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.''

 Wasiotubu Wakiwa Hai Duniani Siku Hiyo Watakuwa Kila Mtu Na Furushi Lake La Dhambi Zake Tayari Kwenda Nalo Jehanamu.
 Obadia 1:15 '' Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.''
 -Matendo Yako Yatakufuata kama hutatubu wakati huu ukiwa hai.
-Damu ya YESU KRISTO pekee ndio inayoweza kukufutia maovu yako yote, ya tangu unazaliwa hata sasa kama tu ukiamua kumpokea YESU leo, na kuanza kuishi maisha matakatifu kuanzia sasa.

 Leo Ni Siku Njema Ya Kujua Hili Na Naamini Hako Ka Mzigo Utakapeleka Kalvari Leo Baada Ya Kutubu Na Kumpokea BWANA YESU. 
Ni Tendo La Kiroho Hili Wala Halihitaji Kwenda Kimwili. 
Ndugu yeyote ambaye Inayemhusu hii naomba Awafuate Wachungaji Wamsaidie Maana Kazi Ya Wachungaji Ni Kuwapatanisha Wanadamu Na MUNGU Wao.

 Ndugu mmoja aliniambia kwamba yeye hana tatizo kubwa maana hafanyagi dhambi kubwa. 
nikamuuliza dhambi kubwa ni ipi?
akasema dhambi kubwa ni kama uzinzi, kutoa mimba, kuroga na uchawi. nikamwambia " Uko sahihi kabisa maana hizo ni dhambi kubwa na hazifai lakini pia naomba ujue kwamba dhambi zote ni kubwa Tena hazifai" akasema kivipi dhambi zote ni kubwa?
Nikamwambia

 " Kwa maana yeye aliyesema, usizini, pia alisema, usiue, Hivyo ukikosa katika moja umekosa katika yote(Yakobo 2:10-11)
Katika andiko hilo Biblia inasema  
'' Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote. Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria.   ''
 
Ndugu zangu, ni muhimu sana kuacha dhambi zote.
Ndugu huyu alijua dhambi ya uongo inayomsumbua ni ndogo, alijiona mtakatifu mbele ya watenda dhambi wengine kumbe hata yeye asipotubu hukumu ya MUNGU inamhusu sana.


Ndugu zangu, tusizipake rangi dhambi zetu Bali tuzitubie na kuziacha, kumbuka kuwa dhambi ni dhambi tu na haibadilikagi jina.
-aliyesema usiabudu sanamu ndiye Huyo aliyesema usiibe, ukikosa katika moja, umekosa katika yote.
-Aliyesema usipokee rushwa ndiye Huyo huyo aliyesema usiende Kwa waganga na wasoma nyota, ukikosa katika moja, umekosa katika yote.

Dhambi ni mbaya sana na kila mmoja anatakiwa aachane na dhambi zake.
Yuda kwa kumsaliti YESU aliambiwa ''Ni heri usingezaliwa'' (Marko 14:21)
Je waamini wanaomsaliti BWANA YESU leo unadhani ni neno gani linalowafaa linalowafaa Kuambiwa?
Tuko katika nyakati za mwisho.
hakuna haja ya kung'ang'ania dhambi bali dawa ni kutubu tu na kuokoka.
Najua sio wote wataokoka lakini naomba wewe unayesoma ujumbe huu okoka na anza kuishi maisha mataktifu ya Wokovu.

 Wakati mwingine cheo au madaraka ya MTU vinaweza kumpeleka jehanamu, mtu kama huyo akiambiwa atubu na kuokoka ataona anadhalilishwa kumbe kashadhalilishwa na shetani siku nyingi ndio maana jina lake halimo katika kitabu cha Uzima. Tukio la kuambiwa kutubu leo analolidharau ndilo linaloweza pekee kulirudisha jina lake kwenye kitabu cha Uzima cha YESU KRISTO.

Warumi 6:23 ''Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA  wetu.  ''
Ni saa ya kuokoka na kuishi maisha mataktifu halisi.
Dunia na mambo yake yote yatapita.
Dunia isikufanye utende dhambi bali ishinde dunia kwa kuishi maisha mataktifu.
 Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke.
Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo yangu ambayo sasa yanafika 400 mtandaoni.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula. 

0714252292.
 mabula1986@gmail.com

Comments