MCHUNGAJI ALIVYONUSURIKA KUUAWA

Kwa YESU yote yanawezekana.

Katika Kijiji fulani mkoani Kilimanjaro, ulifanyika mkutano wa Injili. Miongoni mwa watu waliookoka ni kijana mmoja wa kiislamu. Kutokana na uamuzi huo wa Kumkataa shetani na kumkiri Yesu, alifukuzwa Nyumbani, akawa anaishi kwa Mchungaji.

Hazikupita siku nyingi, kijana akiwa kwa Mchungaji alianza kuumwa, wakampeleka hospitali, lakini kadiri siku zilivyoenda ndivyo hali ilivyozidi kuwa mbaya.

Wazazi wake walijulishwa, lakini walisema mgonjwa hawamtambui, wanamtaka mtoto wao akiwa mzima, wala hawakwenda hospitali kumuona.
Kanisa lilijitahidi kuomba lakini matumaini hayakuonekana, hatimaye kijana akakata roho!

Wazazi walipopelekewa taarifa ya msiba, walisema wanachohitaji ni kumuona mtoto wao akiwa hai, na wakati huo wanadini wakajulishana, wakakusanyika na kuanzisha vurugu wakidai aliyekufa ameuliwa na Mchungaji.

Kwa wakati huo maiti iliondolewa Mochwali, ikaletwa Nyumbani kwa Mchungaji. Vijana washika dini waliizingira nyumba ya Mchungaji wakiwa na mawe, mapanga na marungu kwa lengo la kumuua Mchungaji.

Alipoona hatari ya kuuawa, Mchungaji akakumbuka, kumbe, Jina la YESU lipo si kwa kukemea mapepo tu, akakumbuka kumbe likitajwa hata wafu hufufuka! (Math 10:8) Ndipo akaomba maiti iletwe chumbani kwake.

Mchungaji akiwa chumbani peke yake na maiti, akaliitia Jina la YESU. Haikupita muda, akaona maiti anapiga chafya! Kuona hivyo, Mchungaji akamhimidi BWANA, akamwita jina, kijana kaitika! Akamshika mkono, akamwinua na kumpeleka mbele ya umati, Kisha akaanza kuhubiri.

Kwa muujiza huo, watu wengi walimpokea Yesu siku hiyo. Miongoni mwa waliookoka siku hiyo, inasemekana ELINGALAMI MUNISI, alikuwa ni mmoja wao. Huyo ni mwandishi wa vitabu, Mchungaji na Mkurugenzi wa Idara ya Uanafunzi na Maandiko katika Kanisa T.A.G.

FUNDISHO:
*Mtumaini BWANA, wala usizitegemee akili zako mwenyewe. Angalia Neno linasemaje, na si akili zako zinakupa tafsiri gani juu ya kile unachokiona.

* Viwete, vipofu, viziwi, mabubu na wanaokufa wengine wanapatwa na hayo kwa ajili ya Utukufu wa Mungu. (Yohana 9:3) Wakati umefika, ukisema Yesu yu Hai, basi na tuzione kazi zake.
UBARIKIWE.

Comments