ONDOKA KWENYE UFALME WA GIZA NA NENDA KWENYE UFALME WA NURU.




BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Mtu mmoja siku moja aliniambia kwamba yeye anajitambua ndio maana anashabikia timu fulani. nikamwambia kwamba  hajitambui maana angekuwa anajitambua basi ungempokea YESU na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Labda na wewe ndugu ngoja nikuulize swali hili.
je wewe ndugu yangu unajitambua?
Kama umeokoka kweli kweli hakika unajitambua.

Kujitambua ambako ni muhimu, ni kule kujitambua kwamba wewe ni mwenye dhambi, na kwa sababu ya dhambi zako hakika huna sifa hata moja ya kuingia uzima wa milele.
Ukishajitambua na ukautambua msaada pekee wa kukufanya upate neema, basi hakika utaufuata msaada huo.
Msaada pekee ambao wanaojitambua wameufuata ni YESU KRISTO, ambaye ndiye pekee anayeweza kuwaokoka wanadamu kutoka dhambi na kuingia nuruni.
Mathayo 7:13-14 '' Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.''
-Mlango wa uzima wa milele ni YESU KRISTO.
Mlango huo ni mwembamba na sio wote wanaouona.
Wanaojitambua tu ndio wanaouona mlango huo.
Bila kupita katika mlango huo mwembamba hakuna uzima wa milele. 
Wanaojitambua hakika wameingia katika mlango huo mwembamba.
Mlango mwembamba ndio njia ya uzima wa milele.
Iko njia moja tu na njia hiyo ni YESU KRISTO.
Inaonekana ni njia nyembamba kwa sababu duniani wanadamu walio wengi wamekubariki kudanganywa na yule asi shetani. 
Lakini kwa wanaojitambua neno la MUNGU linasema,

 ''Na kila mwenye matumaini haya katika yeye(YESU) hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu. Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake.-2 Yohana 3:3-5'' 
BWANA YESU alidhihilishwa ili aziondoe dhambi, na tukio hilo hufanyika pale tunapompokea yeye na kutubu dhambi zetu.


Shetani Na Ufalme Wake Wanaitwa Giza. Ni Jina Lao Na Ndivyo Ilivyo. 
Wanadamu Hawatakiwi Wawe Wana Wa Giza Bali Wana Wa Nuru. Biblia Inasema Kwamba Waliookoka Si Wana Wa Giza, Bali Wa Nuru, hao ndio waliojitambua.
Waefeso 5:8 ''Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika BWANA; enendeni kama watoto wa nuru,'' 
-Kumbe tunatakiwa tuenende kama wana wa nuru na sio giza.
Wana wa nuru huishi maisha mataktifu.
Wana wa nuru hawanajifichi vichochoroni usiku kwenye maovu.
Wana wa nuru wanajitambua. Biblia inaendelea kusema juu yao waliookoka
  ''Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.-1 Thesanolike 5:5'' 
-Wana wa nuru humtukuza MUNGU na sio shetani.
Wana wa nuru hufanya mambo mema na matakatifu na sio dhambi na uovu.
Wana wa nuru hakika wanajitambua maana wako nuruni mwa YESU KRISTO.
Wana wa nuru hawawezi kufungwa nira moja na uovu maana hawawezi kufanya uovu.
Biblia inasema neno hilo.

 2 Kor 6:14 '' Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya KRISTO na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la MUNGU na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la MUNGU aliye hai; kama MUNGU alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa MUNGU wao, nao watakuwa watu wangu.'' 
-Waliookoka ni wana wa nuru tena ni hekalu la MUNGU. Hawa ndio wanaojitambua na wanatambua waishije katika dunia hii iliyojaa uovu na machukizo mengi.
Waliookoka hawako gizani bali wako nuruni.
Kuokoka ni kumpokea YESU kama BWANA na MWOKOZI wa maisha yako kisha unaanza kuishi maisha matakatifu ya wokovu.

 Giza Lina Maana Ya Ufalme Wa Shetani Lakini BWANA YESU Anaokoa Na Kuwatoa Watu Kutoka Gizani Kwa Shetani Na Kuwaweka Kwenye Nuru Yake Ya Ajabu. 
Wakolosai 1:13-17 ''Naye(YESU) alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa MUNGU asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye.''

 Maana Yake MUNGU Alituhamisha Sisi Wateule Wake Kutoka Eneo Moja Linaloitwa Giza Na Kutuingiza Katika Eneo Jingine Linaloitwa Nuru Yake MUNGU.
 Huko Ndipo Kuzaliwa Upya. 
Huko ndiko kujitambua kunakofaa kwa kila mwanadamu.
Tukio La Kuhamishwa Huku Hufanyika Kipindi Mwanadamu Anampokea YESU Kama BWANA Na Mwokozi Wake, Anatubu Na Kuanza Kuishi Maisha Matakatifu Sawasawa Na Neno La MUNGU. 
Sio Wote Wamehamishwa Ila Ni Wale Tu Wanaomtii MUNGU Aliye Hai. 
Kama Kuna Kitu Shetani Anakupinga wewe Basi Hataki Wewe Uhamishwe Kutoka Kwenye Familia Yake Na Kuingia Kwenye Familia Ya Watoto Wa MUNGU. 
Ndugu, Kama Hujaokoka Naomba Uokoke Leo  maana huko ndiko kuhamishwa kutoka utawala wa shetani na kuingia katika ufalme wa MUNGU kupitia YESU KRISTO.
Huko ndiko kujitambua.
Ndugu Uliyeokoka tayari, nakuomba Shikilia Taji Yako Asije Mtu Akaitwaa.
Baki ukijitambua siku zote kwa kuishi maisha mema na mataktifu kama neno la MUNGU linavyoagiza.
dhambi isikuharibie wokovu wako.
tunza utu wako na jifunze neno al MUNGU huku ukimtii MUNGU katika maisha yako yote.
 ''Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake;-Wakolosai 3:9''
Dunia na mambo yake yote yatapita.
Dunia isikufanye utende dhambi bali ishinde dunia kwa kuishi maisha mataktifu.
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke.
Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo yangu ambayo sasa yanafika 400 mtandaoni.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

0714252292.
mabula1986@gmail.com

Comments