SIKU YA LEO NI MUHIMU SANA KAMA TU UKIITUMIA KWA BWANA YESU.


BWANA YESU atukuzwendugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Siku Ya Leo Ni Siku Muhimu Sana Kwako. 
Siku Ya Leo Ni Siku Ya Kipekee Sana Kwako Kama Utaitumia Kwa BWANA YESU. 
Mathayo 11:28 '' Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.'' 
-Watu wengi wana mizigo mingi sana lakini siku zote wanataka kupumzishwa mizigo hiyo isipokuwa mzigo mmoja yaani dhambi.
-Unakuta binti anataka apumzishwe mzigo wa kutokuolewa lakini hataki kupumzishwa mzigo wa dhambi.
-Unakuta mama kila siku anataka maombezi ili mzigo wa ugumba utoke kwake lakini huyohuyo hataki kupumzishwa mzigo wa dhambi zake. ukimwambia njoo kanisani utubu atakuambia nitajitahidi mwakani lakini ukimwambia njoo kanisani  nikuombee ili utasa utoke atataka kuja dakika  hiyo hiyo kanisani.
-Unakuta kijana yuko tayari leo kupumzishwa mzigo wa kuteswa na wachawi usiku, lakini mzigo wa dhambi atakuambia atafanya hivyo mwezi ujao.
-Unakuta baba anataka apumzishwe ugonjwa wa ukimwi alioupata akizini nje ya ndoa, lakini bado licha ya  kuwa na ugonjwa huo bado hataki kupumzishwa mzigo wa dhambi.
Zamani mimi nilipokuwa mdogo nilikuwa najua kwamba wengi wa wanaoenda mbinguni ni wazee na wagonjwa wa ukimwi.
Nilijua kwamba kama mtu amefikisha umri wa miaka 75 na kuendelea basi huyo angeishi maisha matakatifu maana anajua hawezi kuishi miaka 100, nilidhani umri ungemsaidia kutubu maana alijua ana muda mchache zaidi wa kuishi kuliko kijana wa miaka 20.  kumbe nilikosea sana maana leo wazee wengi sana hawamtaki YESU japokuwa wanautaka uzima wake wa milele. Nilijua kwamba kama mtu atajikuta ana ukimwi basi huyo lazima aende mbinguni maana ataishi maisha matakatifu akijua kwamba hana miaka mingi ya kuishi ukilinganisha na watu ambao ni wazima, kumbe nilijidanganya sana maana leo kuna wagonjwa wengi wa ukimwi wanashinda bar na gesti huku wakijua kabisa hawana muda mrefu wa kuishi ukilinganisha na walio wazima. nilikuwa nawaza tu zamani lakini hivyo bado sio sababu ya kuwasababishia watu wakaingia uzima wa milele. 
Jambo kubwa zaidi ambalo BWANA YESU anataka kuwapumzisha wanadamu ni kuwaondolea dhambi zao kama tu wakitubu. anawaondolea jehanamu kama tu wakitubu na kuanza kuishi maisha mataktifu.
Leo yako imebeba yote mawili, imebeba uzima wa milele na imebeba ziwa la moto kama bado huhitaji kupumzishwa mzigo wako wa dhambi.

Yawezekana Wachawi Wanakupangia Mambo Mabaya Sana Lakini Kitendo cha Wewe Cha Leo Cha Kumfuata YESU Kitawafanya Wakuogope Na Kukukimbia Maana Utakuwa Huingiliki. 
Yohana 8:36 '' Basi Mwana(YESU) akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. ''

Leo Yako Ni Muhimu Sana Kama Utaitumia Kwa BWANA YESU. Haijalishi Ulitenda Dhambi Nzito Kiasi Gani Lakini Ukiitumia Leo Yako Kumpokea YESU Na Kutubu Itakufanya Uwe Wa Uzimani Na Sio Motoni.
 Isaya 55:6-9 '' Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa.  Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.''

 Leo Yako Ni Ya Muhimu Sana. Itumie Leo Yako Kujulikana Mbinguni Mara Baada Ya Kumpokea YESU Na Jina Lako Kuandikwa Kwenye Kitabu Cha Uzima. 
Luka 15:10 ''Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.'' 

Neema Ingalipo Na Neema Hiyo Inatutaka Tumpokee BWANA YESU Kisha Kuanza Kuishi Maisha Ya Wokovu. 
Yuda 1:3 ''Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu.'' 
-Imani Ya Uzima Ipo Moja Tu Nayo Yatutaka Tumpokee YESU Kama BWANA Na Mkombozi Wa Maisha Yetu Kisha Tuishi Maisha Ya Wokovu Matakatifu Huku Tukilingojea Kwa Imani Kuu Tumaini La Uzima Wa BWANA YESU KRISTO. 
Leo Yako Imebeba Ushindi Kama Ukiamua Kuhusika Na Huo Ushindi.
 Leo Imebeba Uzima Wa Milele Kama Ukimpokea YESU.

Kumb 11:26-28 ''Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya BWANA, MUNGU wenu, niwaagizayo leo; na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya BWANA, MUNGU wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua.''
-Leo yako usitangulize miujiza bali tanguliza kumpokea YESU na kuzaliwa mara ya pili.
-Leo yako usitangulize miujiza bali tanguliza  Kuokoka na kufanyika mtoto wa MUNGU ambaye anasubiri uzima wa milele.
 Usitangulize ishara na miujiza ila tanguliza
kwanza kuhakikisha jina lako limeandikwa
mbinguni kwenye kitabu cha uzima cha Mwana
kondoo YESU KRISTO. Ndipo hayo mengine
yafuate.

Mathayo 6:33 ''Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.''

 Wakati mwingine cheo au madaraka ya MTU vinaweza kumpeleka jehanamu, mtu kama huyo akiambiwa atubu na kuokoka ataona anadhalilishwa kumbe kashadhalilishwa na shetani siku nyingi ndio maana jina lake halimo katika kitabu cha Uzima. 
Tukio la kuambiwa kutubu leo analolidharau ndilo linaloweza pekee kulirudisha jina lake kwenye kitabu cha Uzima cha YESU KRISTO.
Mithali 27:1 ''Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja.''
Leo yako itumie kwenda kwa mkombozi ambaye ni BWANA YESU pekee.
1 Yohana 4:14-19 ''Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa BABA amemtuma MWANA kuwa MWOKOZI wa ulimwengu. Kila akiriye ya kuwa YESU ni Mwana wa MUNGU, MUNGU hukaa ndani yake, naye ndani ya MUNGU. Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo MUNGU kwetu sisi, na kuliamini. MUNGU ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya MUNGU, na MUNGU hukaa ndani yake.
 Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, kama yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu. Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo.
Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza.  '' 

- Kwa sababu ukombozi upo basi na Mkombozi yupo.
Na siku zote Ukombozi hutoka kwa Mkombozi.
Bila Mkombozi basi hakuna ukombozi.


Wengi leo wanataka riziki tu kutoka kwa MUNGU lakini hawataki uzima wake wa milele leo.
Mathayo 6:11 '' Utupe leo riziki yetu. ''
-Wengi leo wanataka riziki tu na sio toba.
-Wengi leo wanataka kubarikiwa tu na sio kuambiwa kutubu.
Ni sawa kabisa kuomba riziki kwa MUNGU lakini kabla ya riziki MUNGU anataka kwanza uokoke na uanze kuishi maisha mataktifu.
 Hakuna mkombozi mwingine ila YESU KRISTO.

Leo yako ndio muhimu sana kuitumia kuamua hatima ya maisha yako. 
 ''Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA wetu.-Warumi 6:23''
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi
tutajifunza tena siku nyingine. na kama
hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea
ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika
jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza
kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani.
MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki
upotelee motoni anataka uende uzimani aliko
KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments