UJANA WAKO UNAUTUMIA KWA NANI?

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU apewe sifa ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Maisha ya utotoni hadi ujana yanahitaji mjenzi mzuri ili kijana huyo ampeneze MUNGU.
 kila mtoto au kijana kila anachofundishwa kina mchango katika maisha yake. Kama anafundishwa vitu vibaya hivyo hivyo vitakuwa na mchango mbaya katika maisha yake.
Kama anafundishwa vitu vizuri basi hakika vitakuwa na mchango mzuri katika maisha yake.
Hakuna vitu vizuri zaidi ya Neno la MUNGU, hofu ya MUNGU kuambatanisha maisha yake na YESU KRISTO.

Je, wewe ujana wako unautumia kwa nani?
Je, ujana wako unautumia kwa MUNGU au kwa shetani?
Hakuna faida hata moja kama ujana wako utautumia kwa shetani.
Kumbuka dhambi wakati mwingine inaweza kuleta kifo cha mapema.
Wana wa Israeli walifia jangwani isipokuwa wawili tu ambao walitoka Misri hadi Kaanani. ukifuatilia vifo vyao vilisababishwa na dhambi zao.  waliotoka Misri wote walifia njiani isipokuwa watu wawili tu, hivyo Waisraeli waliofika Kaanani wakitokea Misri ni watoto na wajukuu tu wa wale waliotoka Misri, ila hao wajukuu ndio walioungana na Yoshua na Kalebu ambao katika Taifa zima ndio waliotoka Misri na kufika Kaanani. Ndio maana kuna kitabu kinaitwa Kumbukumbu la Torati ambacho ni marudio ya Torati nzima ambapo wakati huu wale waliofundishwa torati mwanzo walikuwa wamekufa kwa sababu ya dhambi zao na uasi, hivyo kumbukumbu la Torati Musa alikuwa anawasomea wale ambao walikuwa watoto wadogo au hawajazaliwa kipindi baba zao walikopokuwa wanafundishwa, ndio maana kitabu kikaitwa kumbukumbu la torati. kumbe dhambi inaweza kuleta vifo vya mapema wakati mwingine.
Kuutumia ujana wako kwa shetani ni hatari sana.
Je unautumia ujana wako kwa nani?

Zaburi 119:9,11 '' Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako. Moyoni mwangu nimeliweka neno lako(MUNGU), Nisije nikakutenda dhambi.'' 

 Kuna vitu humjenga kijana na kumbomoa kijana.
Kuna vijana huiga mambo na kudhani kwamba huo ni utaratibu tu wa maisha, na kwa sababu kuna watu wanaishi hivyo na yeye anaona kuwa ana haki tu ya kuishi hivyo.
Ndugu yangu, jambo muhimu kulijua ni kwamba ni vizuri sana kuishi kama neno la MUNGU linavyotaka na sio kama nafsi yako inavyotaka.

Je, Unautumia ujana wako kwa nani?

1 Yohana 2:15-17 '' Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele. ''

 Ni vizuri sana kuweka msingi wa maamuzi yako kipindi cha ujana.
Umri wa ujana ni umri wa kuweka msingi wa maisha ya baadae ili huo msingi ukufikishe kwenye hatima njema. Msingi imara na ambao haujawahi kushindwa ni neno la MUNGU hivyo ni muhimu sana kulitii Neno la MUNGU maana huo ndio msingi imara na wa kudumu.

Je, Unautumia ujana wako kwa nani?

Zaburi 119:105 '' Neno lako(MUNGU) ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.''

 Maamuzi yako ya sasa mshirikishe MUNGU ili hata maamuzi ya baadae upate tena ujasiri wa kumshirikisha MUNGU.
Kama kwa sasa unadhani unaweza hata hutaki kumshirikisha MUNGU hiyo itakusumbua baadae pale ambapo utakuwa umekwama na unamhitaji MUNGU tu akusaidie.

Je unautumia ujana wako kwa nani?

Mhubiri 12:1 '' Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.''

 Umri wa ujana ndio umri wa kufanya maamuzi ya hatima ya kijana huyo baadae.
Ukiamua kujishughulisha na dhambi itakusumbua sana baadae, na muhimu kujua ni kwamba watenda dhambi hawataingi uzima wa milele, hivyo ni heri sana kufanya maamuzi mazuri wakati wa ujana kwa kumpokea YESU na kuanza kuishi maisha matakatifu.

Je, unautumia ujana wako kwa nani?
Yohana 3:36 ''Amwaminiye Mwana(YESU) yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya MUNGU inamkalia.''

Kuna baadhi ya vijana misingi yao ya ucha MUNGU wameiharibu.
Kuna baadhi ya vijana hawakupata neema ya kujifunza Neno la MUNGU na kulitii hivyo wamevulunda katika mambo mengi.
Lakini neema ya MUNGU bado inawahitaji ili watengeneze njia zao.
 Je, ni lini utaacha kuutumia ujana wako kwa shetani na kumkabidhi BWANA YESU maisha yako?
Isaya 55:7 '' Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa. ''

 Kijana,Misingi yako ikiharibika tafanya nini(Zaburi 11:3).
Inawezekana kabisa msingi wako uliuweka kwa watu fulani, je wakiondoka hao utafanya nini?

Inawezekana unaishi kwa kuwategemea wazazi tu, je wakiondoka utafanya nini?
Ni muhimu sana kuweka msingi wako katika Neno la MUNGU.
Ni muhimu sana kuweka msingi wako kwa BWANA YESU, maana wanadamu hukoma lakini BWANA ni wa milele.

Kuna vijana pia wamepitia malezi mabaya na kujikuta wana tabia mbaya sana.
Ni hatari sana na kama uko wa namna hiyo naomba umpokee YESU na kubadilisha mfumo wako wa maisha.
Je, unautumia ujana wako kwa nani?

2 Timotheo 2:22-23'' Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao BWANA kwa moyo safi. Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi.   ''

 Kuna maadili mema na maadili mabaya.
Sio wote wana maadili mema na pia sio wote wana maadili mabaya.
Ukiwa na maadili mema ni kwa faida yako mwenyewe na ukiwa na maadili mabaya ni kwa hasara yako mwenyewe.
Ukiwa duniani unaweza kuwadanganya sana wanadamu lakini mbingu zinakujua wewe kwa undani kabisa hivyo ni bora tu ukawa mcha MUNGU asiye na michanganyo

Yeremia 2:19 ''Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha BWANA, MUNGU wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema BWANA, BWANA wa majeshi.''
Je, unautumia ujana wako kwa nani?
 Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke.
Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa
wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

Comments