UTATHIBITIKA KATIKA HAKI, UTAKUWA MBALI NA KUONEWA



BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tuimalishane kiroho na ki-ufahamu na  ili tuinuke kiimani na ki mitazamo.
Mwanzoni mwa wiki hii nikiwa katika maombi ya kufunga na kuomba, sauti hii iliongea ndani yangu kwa nguvu ''UTATHIBITIKA KATIKA HAKI, UTAKUWA MBALI NA KUONEWA''.
Ghafla nilichangamka sana na kuanza kuomba kwa spidi huku nikitumia andiko hilo ambalo liko kwenye Biblia, lakini wakati wa maombi hata sikujua liko katika kitabu gani ila nilichojua ni kulitamka tu, maana ndio lilikuwa Neno langu kutoka kwa BWANA YESU, kwa ajili ya mahitaji yangu ambayo nilikuwa nayaombea.
Sio kwamba andiko hilo ni special kwa ajili yangu tu bali ni special kwa ajili wa wateule wa MUNGU wote.
Hakika kama kanisa tunatakiwa tuthibitike katika haki na tuwe mbali na kuonewa, lakini haya hayatakuja kama tu tutakuwa tumelala au tumegeuka wanasiasa kanisani.
Katika kile ambacho nilikuwa namwita MUNGU kwacho siku hiyo hakika niliamini Neno la ufunuo lilivyosema.
  BWANA YESU anasema
 ''Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.-Yohana 15:7''
-Kumbe kwanza tunatakiwa tukae ndani ya YESU.
Kukaa ndani ya YESU ni kulitii Neno lake, kutembea katika neno lake na kuishi maisha matakatifu.
Kukaa ndani ya YESU ni kumtii ROHO MTAKATIFU maana ROHO humshuhudia YESU KRISTO ndani yetu.
-Lazima maneno ya YESU yakae ndani yetu. 
maneno ya YESU sio kwamba tunakariri bali tuyaishi maana ni neno hai la MUNGU.
-Kumbe pia ni lazima tuombe, kama huombi hata kama uko ndani ya YESU bado hutathibitika katika haki na wala hutakuwa mbali na kuonewa.
Kumbe hata kama neno la KRISTO liko ndani yako lakini kama hukai katika KRISTO bado wewe kupokea itakuwa ni ngumu.
MUNGU aliye hai anasema 
'' Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia.-Isaya 65:24''
Siku ya maombi yangu. 
Kabla ya kuanza maombi hayo nilikuwa katika hali ya unyonge mkubwa sana, nilianza maombi taratibu huku nikisikiliza Rohoni nitaelekezwa kuombea nini. Sikuwa nimeandika maombi ila niliona nibadilishe mfumo wa maombi, badala ya kuandika maombi kwenye karatasi siku hiyo niliamua kutokuandika ila kuombea kila kile ambacho ROHO wa MUNGU atakileta moyoni mwangu.
Roho yangu ilikuwa ina maumivu makali sana, nilimuhitaji BWANA YESU na nguvu zake.
Nilihitaji kibali cha kimbingu kwa ajili ya maisha yangu, nilihitaji  ushindi wa ghafla kutoka kwa MFALME wa mbinguni.
Niliomba  kwa imani rohoni  huku nikiamini kwamba MUNGU aliyewasikia kanisa zamani wakiomba kwa ajili ya Mtume Petro atolewe gerezani na akatolewa baada ya maombi yao, nilitamani na mimi MUNGU huyo anisikie na kunijibu sawasawa na maombi yangu. 
Nilitamani MUNGU aliyemsikia Danieli akiomba  kwenye shimo la simba anisikie na mimi na kunijibu.
Nilitamani MUNGU aliyemsikia Yona akiomba huku akiwa tumboni wa nyangumi, basi anisikie na mimi na kunijibu.
Nilikuwa na uchungu mwingi sana lakini Ghafla ikasikika kwa nguvu sauti ikisema '''UTATHIBITIKA KATIKA HAKI, UTAKUWA MBALI NA KUONEWA '' 
.Niliendelea na maombi na baadae mimi na mke wangu tukaanza kulitafuta andiko hilo ambalo tunalifahamu lakini kwa muda wa maombi hatukujua liko kitabu gani.
Haikuchukua muda tukaliona andiko hilo.
Isaya 54:14 '' Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.''

Roho yangu ilifurahi sana kukutana ana andiko hilo.
Niliomba na kupata amani ya ajabu sana.
Niliona ushindi mkuu kupitia andiko hilo. Imani yangu iliongezeka sana.
Neno la MUNGU na ufunuo ni muhimu sana.
Neno la MUNGU la ufunuo huja likitokea katika Neno la MUNGU(Biblia) lakini kwa njia sahihi iliyo na kibali cha ROHO wa MUNGU.
Andiko moja kwenye Biblia linaweza kutumika katika funuo hata 7 katika watumishi tofauti na inategemea MUNGU anataka alitumieje Neno lake.
Mfano andiko la Marko 9:23 '' YESU akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.''
-Anaweza kufunuliwa mtu ambaye anatakiwa aombe kwa imani ndipo atapewa anachoomba.
-Andiko hilo anaweza akafunuliwa mtu ambaye ingawa anaumwa sana lakini lazima atambue kwamba kupona inawezekana kama huyo ndugu ataomba katika jina la YESU KRISTO au atayafuata maombezi yaliko.
-Andiko kama hilo anaweza akafunuliwa binti ambaye anatamani kufunga ndoa, wakati katika ukoo wake wote hakuna hata mmoja aliyewahi kufunga ndoa takatifu, bali hutoroshwa tu. binti huyu akiomba kwa imani kama neno la MUNGU litakavyo hakika anaweza kuifikia hatima yake njema.
-Andiko hilo anaweza akafunuliwa dada ambaye amefukuzwa nyumbani kwao kwa sababu ya kumpokea YESU, hivyo kupitia Neno hilo la MUNGU, dada yule anatakiwa aombe na atambue kwamba inawezekana kabisa wazazi wake kuja na kumbembeleza kurudi nyumbani maana Maombi yake MUNGU ameyajibu. 
Hiyo ni mifano tu katika maelfu ya funuo ambazo MUNGU anaweza akawapa wateule wake ili kuwasaidia jinsi ya kufanya ili wapokee. 
Kumbe kuthibitika katika haki na kuwa mbali na kuonewa inawezekana tu kama tuna imani thabiti.
Neno la MUNGU  limebeba ushindi wako.
Sio kwamba andiko hilo tu ndio muhimu bali Biblia nzima imebeba maandiko ya ushindi kwetu.
Ajabu ni kwamba MUNGU anakuwa analiangalia Neno lake ili alitimize.
Yeremia 1:12 '' Ndipo BWANA akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize.'' 
-Biblia imejaa maandiko mengi ambayo ni neno la MUNGU ambalo MUNGU anataka alitimize katika maisha yako.
sio maandiko yote lazima yatimie kwako lakini kama ROHO MTAKATIFU yuko ndani yako nakuhakikisha kwamba liko tu Neno ambalo atakupa wewe na ukitembea katika utakatifu autakao MUNGU hakika litatimia katika maisha yako. Kama ukiwa na ROHO MTAKATIFU lazima tu yako maandiko sana atakupa ili kuwa ushindi kwako ikitegemea na mahitaji yako.
Wengi sana hajaokoka hivyo ROHO MTAKATIFU hayuko kwako, na kutokuwa kwao na ROHO MTAKATIFU hakika ni hasara kwao.
Yohana 14:15-18 ''Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba BABA, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye ROHO wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu.''
-ROHO MTAKATIFU ndiye msimamizi wa wokovu wetu.
ROHO MTAKATIFU ni muhimusana katika maisha ya Mkristo.
Ukiona  kanisa wanamkataa ROHO MTAKATIFU huko hama na nenda katika kanisa wanaoamini ROHO MTAKATIFU, Maana tutashindaje ya dunia kama ROHO wa MUNGU hatakuwa pamoja na sisi?
Mambo mengi ya kidunia kibinadamu tunaweza kuyaona hayana madhara na sisi lakini kama tutamsikiliza ROHO wa MUNGU tutaona anatukataza maana yeye analijua jambo mwisho kabla ya mwanzo. sisi tunaona mwanzo tu lakini mwisho hatuujui lakini ROHO MTAKATIFU huona mwisho kabla ya mwanzo ndio maana sehemu nyingi Biblia inatushauri tuenende kwa ROHO na tuongozwe na ROHO.
Kumbe unaweza kuwa na ROHO MTAKATIFU lakini usitake akuongoze na ndio maana mambo yako mengi yana kwama.
Unaweza ukawa na ROHO MTAKATIFU lakini siku zote hutaki kuenenda kwa ROHO na ndio maana unakwama.
Warumi 8:14 ''Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO  wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''
-Kumbe ni mihumi kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.
Katika kuongozwa na ROHO MTAKATIFU anaweza akakupa hata neno la ufunuo ili kukusaidia. 
-Kumbe utathibitika katika haki na utakuwa mbali na kuonewa kama tu ukiongozwa na ROHO MTAKATIFU huku ukijua kuumiliki ulimwengu wa roho.

Kuna mtumishi wa MUNGU mmoja ambaye ROHO wa MUNGU alimpa andiko la Waefeso 1:17 '' MUNGU wa BWANA wetu YESU KRISTO, BABA wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; '' 
-Andiko hili kwako linaweza kuwa la kawaida tu lakini kwa mtumishi yule andiko hili ni zaidi ya andiko bali ni neno la ufunuo kwa ajili ya huduma yake.
Kila akipanda madhabahuni alikuwa anaomba MUNGU ampe Roho ya hekima na Roho ya ufunuo katika kumjua MUNGU na Neno lake ndipo anaanza kuhubiri. 
Kama hajasema MUNGU nipe Roho ya hekima na ufunuo katika kukujua wewe na neno lako hahubiri siku hiyo. aliamini katika ufunuo huo na hakika ukisikiliza mahubiri yake ungesema hahubiri mwanadamu bali anahubiri Malaika wa MUNGU aliyevaa sura ya mwanadamu, alikuwa anahubiri kwa sauti ya kawaida tu lakini kile anachokisema cha kwenye Biblia kinaweza kukufanya useme ''naokoka upya leo '' kila akihubiri.
Mtumishi yule alikuwa anaomba kwanza ROHO wa MUNGU amhubiri yeye ndipo na yeye akawahubiri watu, ndio maana ya kuomba kwanza apate ufunuo wa kumjua MUNGU na Neno lake ndipo atasema kitu sahihi ambacho alitakiwa kusema
Sio kila kitu sahihi ni sahihi kukisema katika kila eneo, kumbe tunamhitaji sana ROHO MTAKATIFU ili atupe kibali cha yale ambayo tunatakiwa kuyasema.
Somo hili ningekuwa nafundisha kwa njia ya sauti ninekuambia ilipe kichwa cha somo wewe mwenyewe lakini kwa sababu ya blog na website ndio maana nimeandika kichwa cha somo ambacho kinahusu ka ufunuo nilikopewa mimi japokuwa somo ni pana zaidi. 
Niseme tu MUNGU akubariki sana na nakuomba uombe bila kukoma maana ndivyo Biblia inatuagiza katika 
1 Thesalonike 5:17  kwamba ''ombeni bila kukoma;''
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo yangu ambayo sasa yanafika 400 mtandaoni.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

Comments