HARIBU MADHABAHU YA POMBE KATIKA UKOO WAKO.

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze neno la MUNGU.
Warumi 13:13-14 '' Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali mvaeni BWANA YESU KRISTO, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.'' 
-Watu wote tunatakiwa twenende kwa adabu; Sio kwa ulafi na ulevi, sio kwa ufisadi wala uasherati.
Mengi yamesemwa katika andiko hapo juu lakini mimi leo nazungumzia pombe. 
Pombe ni pando la adui ili kuhakikisha watu hawafiki uzima wa milele.
Pombe ni madhabahu ya shetani ambayo inauwezo wa kuiteka familia nzima au ukoo mzima.
Madhabahu hii ni hatari na kama ikiwakamata ukoo mzima mtajikuta mnaabudu tu katika madhehebu ambayo wanaruhusu pombe maana hata wao wanamilikiwa na madhabahu hiyo ya pombe. yaani hata leo unaweza ukafanya utafiti kwamba kuna baadhi ya koo utakuta ukoo mzima wanasali dhehebu fulani sio kwa sababu ni zuri ila ni kwa sababu hawawezi kuacha pombe ndio maana wako katika dhehebu hilo. Lakini katika Biblia sehemu nyingi tu imesema kwamba hakuna mbinguni ya mlevi hata mmoja.

Kama mlevi anataka mbingu basi aokoke na atubu kisha aanze kuishi maisha mataktifu na aache dhambi zake ikiwepo pombe anatakiwa aiache maana haina faida kwake hata moja bali pombe imejaa hasara tu.
Waefeso 5:18 ''Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;''.
Biblia haikuishia hapo tu kukataza pombe au mvinyo kwa lugha nyingine bali hapa tena Biblia inasema hivi 
''Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi.-1 Kor 6:9-10 ''
=Katika maandiko haya hapo juu walevi wanaitwa wadhalimu na imesemwa hapo kwamba wathalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU.
Walevi hawako katika msafara wa waenda mbinguni ndivyo Biblia imesema. sasa mafundisho ya kuruhusu pombe yanatoka wapi? Wakati Biblia imesema hakuna mbinguni ya walevi?
Ni matokeo ya madhabahu ya pombe kutawala hadi kwa baadhi ya viongozi wa kanisa ndio maana wanafundisha watu wanywe pombe, jambo ambalo halifai kufundishwa na mtumishi wa MUNGU aliye hai.

Pombe haina faida hata moja lakini ina madhara zaidi ya kumi.
Hebu ona katika andiko andiko hili ili uone jinsi pombe inavyoweza kumfanya mtu kuwa mtumwa.
Mithali 23:29-35 '' Ni nani apigaye, Yowe? Ni nani aliaye, Ole? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye mguno? Ni nani aliye na jeraha zisizo na sababu? Ni nani aliye na macho mekundu?
Ni wale wakaao sana kwenye mvinyo; Waendao kutafuta divai iliyochanganyika. Usiitazame mvinyo iwapo ni nyekundu; Iitiapo bilauri rangi yake, ishukapo taratibu; Mwisho wake huuma kama nyoka; Huchoma kama fira. Macho yako yataona mambo mageni; Na moyo wako utatoa yaliyopotoka. Naam, utakuwa kama alalaye katikati ya bahari; Au kama yeye asinziaye juu ya mlingoti. Utasema, Wamenichapa wala sikuumia; Wamenipiga wala sina habari; Nitaamka lini, nitazidi kuitafuta tena.'' 

-Kupitia maandiko hayo tu unaweza ukaona madhara zaidi ya 10 ya pombe.
Ni muhimu sana ndugu yangu kujitenga na pombe na ni muhimu sana kuomba maombi ya kuikomboa familia yako ili iepukane na ulevi.
-Unakuta katika ukoo kijana anataka kujinasua ili aache ulevi ambao umeleta umasikini kwake na kwa ukoo mzima lakini hawezi.
-Inawezekana kabisa dada umeolewa katika ukoo ambao unamilikiwa na madhabahuu ni ya kipepo na mme wako mwanzo hakuwa mlevi lakini miaka 2 baada ya ndoa anaanza tena kunywa maana ndio ukoo wao ulivyo, unamilikiwa na madhabahu ya pombe. unaweza ukamchukia mume wako kumbe madhabahu inayomtumikisha ndio inatakiwa kuharibiwa.
Haribu madhabahu ya pombe katika ukoo wenu.
-Unakuta mama analia kila siku maana wakilima shamba miezi 6 kisha wanavuma mazao , baba wa familia akienda tu kuuza mazao hayo anarudi baada ya siku 4 huku hana hata Shilingi mia. unajiuliza pesa hiyo familia imeitafuta kwa miezi 6 au zaidi lakini inakuja kutumiwa na baba wa familia tu kwa siku 4 kwa sababu ya pombe.
-Ndugu uliyeokoka hakikisha unaukomboa ukoo wako kwa maombi.
-Wewe ambaye umepata neema ya Wokovu wa BWANA YESU hakikisha unaomba ili ukoo wako wawe huru mbali na jini pombe linalowatesa.

BWANA YESU awape neema ya wokovu wake ndugu zako na familia yako.

Habakuki 2:15-16 '' Ole wake yeye ampaye jirani yake kileo, wewe utiaye sumu yako, na kumlevya pia, ili kuutazama uchi wao!Umejaa aibu badala ya utukufu; unywe nawe, uwe kama mtu asiyetahiriwa; kikombe cha mkono wa kuume wa BWANA kitageuzwa ukipokee, na aibu kuu itakuwa juu ya utukufu wako. ''

 Ndugu zangu nawasihini licha ya kuacha vileo unapaswa pia kutompa kileo mtu yeyote yule. haijalishi ni baba, ni mama au ni nani? Kwa kufanya hivyo unashiriki dhambi isiyo ya Kwako, kumbuka dhambi zote ni sawa na hukumu yake inajulikana.

Wewe ndugu uanyefanya dhambi ikiwepo ya ulevi naomba ujue kwamba;
Kujifurahisha katika dhambi kwa muda kidogo kisha ukaingia kwenye ziwa la moto haitakusaidia chochote.
Muda wa kugeuka ni leo, BWANA YESU anakungoja umpokee leo. najua una marafiki wengi wanaokushawishi katika mabaya lakini naomba ujue kwamba siku BWANA YESU akirudi utasimama peke yako kwenye hukumu, rafiki anayekuchochea leo ili umfuate siku hiyo hatakuwa msaada kwako hata mmoja.
Neno hili naomba liwe lako leo na umpokee YESU.


MUNGU BABA akupe macho ya kuona na kuelewa jambo hili nilisemalo leo.
Isaya 5:11 ''Ole wao waamkao asubuhi na mapema, wapate kufuata kileo; wakishinda sana hata usiku wa manane mpaka mvinyo imewaka kama moto ndani yao! ''
 Mambo ya dunia mengi yamewafanya wanadamu wamsahau MUNGU.
  Kazi  zimewafanya wanadamu wengi kumsahau MUNGU.
Japokuwa hakuna mwanadamu hata mmoja ambaye siku ya mwisho atajitetea Kwa ajili ya kazi yake serikalini au kwenye kampuni.
Kazi ya mtu ya sasa haitakuwa na msaada siku ile.
Sio kwamba kazi ni mbaya lakini kitendo cha kuthamini kazi zaidi ya MUNGU wako ambaye ndiye aliyekubariki hiyo kazi ni vibaya.

Na wengi wenu licha ya kuwa busy na kazi lakini mkitoka kazini hamwendi kanisani bali mnaenda bar kunywa pombe na kufanya starehe zingine.
Kila mtu ukimwambia aende kanisani atakuambia kazi imembana hivyo yuko busy lakini mtu huyo huyo hata siku moja hajawahi kukosa bar kwenye pombe.
Ndugu Ambaye umeokoka nakusihi sana kuomba sana kwa ajili ya familia yako na ukoo wako ili BWANA YESU awanasue kutoka kwenye dhambi ikiwepo pombe.
Usifurahie ndugu zako wakose muda wa kwenda kanisani lakini muda wa kwenda vilabuni wanao.
Ukitibu pepo pombe hakika utakuwa umepunguza mengi mabaya katika ukoo wako.
Chanzo kikuuu cha watu kufa na ukimwi wakati mwingine ni pombe maana baada ya kulewa ufahamu unaondoka na mtu huyu anaweza akafanya lolote au akafanyiwa lolote.
2 Kor 6:16-18 '' Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la MUNGU na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la MUNGU aliye hai; kama MUNGU alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa MUNGU wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa BABA kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, ''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments