HERI MWISHO KULIKO MWANZO

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Kama kawaida nakukaribisha tujifunze neno hai la MUNGU.
Leo ni siku nzuri sana katika zile siku nzuri ambazo MUNGU ametupa tuziishi.
Leo tutajifunza jambo la muhimu sana kwa kila mtu.

Kama Kuna Mwanzo Basi Hata Mwisho Upo. 
Mwisho Huwa Ni Muhimu Zaidi Kuliko Mwanzo. 

Mathayo 10:22 '' Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.'' 

BWANA YESU Haangalii Ulianzaje Ila Anaangalia Umemalizaje.
Mwisho ni wa muhimu sana kuliko mwanzo.
Ni Muhimu sana kuanza vizuri na kumaliza vizuri zaidi.
Tunapoongelea umuhimu wa mwisho sio kwamba tunaudharau mwanzo, bali mwisho ndio unaoamua ni wapi pa kwenda kwa kila mtu baada ya kuondoka duniani.
Biblia iko makini sana ikiizungumzia siku ya mwisho.
Ni watu wengi sana wamewahi kumpokea BWANA YESU na kuokoka kabisa, lakini baadae upepo wa dunia ulipowakumba walimsahau Mwamba wa wokovu wao. Hawa walidharau neno la BWANA linalosema '' MWENYE KUVUMILIA HATA MWISHO, NDIYE ATAKAYEOKOKA'' 
Japokua BWANA YESU kupitia watumishi wake aliwaambia watu hawa warudi lakini wengi walishupaza shingo zao.
Mwisho ni muhimu sana kwa kila mtu.
Mzee mmoja siku moja alikuwa ananisimulia jinsi alivyokuwa anamtumikia MUNGU katika ujana wake, alikuwa anazungumzia mambo ya kiutumishi yanayovutia sana. Lakini wakati huo alipokuwa ananisimulia alikuwa mlevi na anavuta sigara  na maisha yake yalikuwa tofauti kabisa na wokovu, alikuwa amebakiza historia tu nzuri lakini yeye alikuwa haiishi historia hiyo ya wokovu.
Watu wengi leo pia wanaweza kujisifu kwa sababu ya utumishi wao kipindi cha nyuma, lakini kama kwa sasa wanaishi maisha ya dhambi kujisifu kwako hakuna maana hata moja. Kuna watu walisaidia watu mbalimbali wakampokea YESU lakini hao hao washuhudiaji kwa sasa wamemkataa YESU na kuichagua dhambi.
Mwisho ni muhimu sana kama unamaliza salama ukiwa na wokovu wako na Uzima wako wa milele ulio katika BWANA YESU tu.
Biblia inatuonya wale tuliookoka kwamba 

''Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa MUNGU, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele.-Warumi 6:22''
 
 Je Unamaliza Na YESU Au Unamaliza Na Shetani?. 
Kuna watu kwa sasa wamebakiza tu story kwamba zamani walikuwa wanakwaya wazuri au waimbaji wazuri, lakini kwa sasa wamejichanganya na dunia na kumwacha BWANA YESU. Wanatembea kwa historia yao ya nyuma badala ya kutembea na utakatifu wa sasa.
Kuna watu hujisifu tu kwamba miaka 17 iliyopita walikuwa wakiombea watu na mapepo yanawatoka, lakini kwa sasa wamemwacha BWANA YESU na kuufuata ulimwengu.
 ni mbaya sana.
Ndugu zangu, Neno hili limekuja kwetu uli tutengeneze njia zetu.
Kuna ndugu ameishi miaka 60 ya dhambi lakini akiambia kwamba basi aokoke na kuishi angalau miaka chini ya 20 ya utakatifu hataki.
Unakuta mtu ameua watu wengi na mwingine ametoa mimba nyingi  na mwingine amefanya kila aina ya dhambi kwa miaka mingi lakini akiambiwa aokoke anaona kama kuokoka ni kujila kumbe ndio kuitafuta kesho yenye uzima wa milele.
Mwisho ni muhimu sana ndugu yangu.
 Wale wanaovumilia hata sasa na hata mwisho Biblia inawaambia kwamba
 ''ambaye atawathibitisha hata mwisho, ili msilaumiwe siku ile ya BWANA wetu YESU KRISTO. MUNGU ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, YESU KRISTO BWANA  wetu. Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la BWANA wetu YESU KRISTO, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja.-1 Kor 1:8-10''

Kuna Watu Walikuwa Kwenye Wokovu Kwa Miaka Mingi Walitumika Katika Maombi, Kwaya Na Huduma Zingine Lakini Baadae Walichoka Kuendelea Na Wokovu.
Walidhani Ni Kawaida Tu Kumbe Ilikuwa Kujiangamiza Maana Baadae Walikufa Na Kupata Hasara. 
Ndugu Unamalizaje? 
Ndugu, Makwazo yapo lakini je makwazo ndiyo yakuondoe kwenye wokovu wa BWANA YESU?
Ndugu, kuzushiwa kupo na kuonewa kupo lakini je hivyo ndivyo vikuondoe katika wokovu wa BWANA YESU?
Kunenewa uongo na kutengwa kupo tu lakini hivyo ndivyo vikuondoe katika Wokovu wa BWANA YESU?
Manabiii wa uongo ni wengi na wao humkataa YESU na wokovu wake, je hao ndio wakuondoe katika Wokovu wa BWANA YESU?
Hila nyingi kwa ajili yako zipo tu, lakini je hizo ndizo zisababishe uwe na mwisho mbaya wakati ulianza na mwanzo mzuri?
BWANA YESU mwenyewe mwenye uzima wetu anatuonya kama ifuatavyo
''Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka-Mathayo 24:10-13'' 

MUNGU Haangalii Kwamba Wewe Umeshawahi Kukemea Mapepo Na Watu Wakafunguliwa.
MUNGU Haangalii Kwamba Ulikuwa Mwimbaji Na Umewahi Kutoa Dvd 5 Lakini BWANA Anaangalia Unamalizaje. 
Heri Mwisho Kuliko Mwanzo Kama Huo Mwisho Unafika Ukiwa Na KRISTO Katika Wokovu Wake Na Utakatifu Wake.
 Ndugu, Je Unamalizaje? 
Shika Uzima Wa BWANA YESU Bila Kumuachia Shetani Hata Sekunde 5. 
Luka 21:19 ''Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.'' 
Ndugu, hakikisha unakua na subira,
Kuwa na subira ni kuvumilia hata iweje.
Vumilia yote ndugu bila kumwacha YESU.
 BWANA YESU Yu Karibu Kuja.
Kuna wadada baada ya kukosa wachumba kanisani  wameamua kutafuta wanaume wa bora liende na kuacha wokovu wa BWANA YESU ulio wa thamani sana.
Kuna wakaka baada ya kukataliwa tu na wachumba mabinti wa kanisani waliookoka wameamua kwenda duniani kutafuta wapagani, ni hatari sana.
Wanaojitambua siku zote wana jua hakuna kitu cha kuwatenga na BWANA YESU.
Warumi 8:35-39 '' Ni nani atakayetutenga na upendo wa KRISTO? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa MUNGU ulio katika KRISTO YESU BWANA wetu. ''

 Ndugu Yangu, Kuna Kesho Na Hiyo Kesho Inatengenezwa Leo. Kesho Inaweza Kuwa Uzima Wa Milele Au Jehanamu Vyote Hivyo Unavitengeza Leo. 
Nakushauri Kesho Itengeneze Leo Kwa Kuokoka Na Kuanza Maisha Ya Wokovu Matakatifu. 
YESU KRISTO Anaokoa, Ukimpokea Leo Unaokoka.
Baada ya kuokoka hakikisha unamaliza salama ukiwa na utakatifu wa BWANA.
Heri mwisho kuliko mwanzo.
Mhubiri 7:8 '' Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi.'' 
 Jitahidi sana jina lako lisiwe kwenye chupa za soda tu bali Liandikwe kwenye kitabu cha uzima wa Milele .
 Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Karibu ku-like page yangu ya www.Facebook.com/petermichaelmabula.

Comments