JE WEWE NI MTU SAHIHI?

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mkristo sahihi akifanya jambo sahihi katika muda sahihi na kwa njia sahihi ni lazima tu atapata matokeo sahihi.
Mkristo halisi ni yule aliyempokea YESU.
Yohana 1:12-13 ''Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake;
waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU''

Hiyo ni A ya Mkristo sahihi lakini B yake ni hii.
 '' Umtumaini BWANA ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.-Zaburi 37:3'' 
Mkristo halisi humtumaini na kumtegemea BWANA kwa maombi na imani.
Mkristo halisi huishi maisha ya uaminifu kwa MUNGU.
Lakini pia napenda ujue kwamba;
Usahihi wa mtu hauji kwa sababu ya elimu yake bali usahihi unakuja kwa mtu huyo kuongozwa na Neno la MUNGU.

''Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.-Zaburi 119:11''
Ndugu yangu nadhani sasa umekwisha kumjua mtu sahihi.
Je, wewe ni mtu sahihi?
Je, unaoshirikiana nao kila siku ni watu sahihi?
Katika wote unaoshirikiana nao naomba ujue kwamba sio wote ni sahihi na sio wote sio sahihi.
Kuna watu walipompokea YESU hakika walifanyika Wakristo sahihi tena wakristo halisi lakini usahihi wao ulianza kuondolewa na marafiki zao, uharisi wao ulianza kuondolewa na wale wa karibu yao  katika maisha.Biblia inatoa ushauri kwa mtu sahihi kuufuata kwamba 
''Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.-Zaburi 1:1-2'' 

Sheria ya BWANA inaitwa Biblia takatifu, hiyo ndio inatakiwa kumpenzeza huyu mtu sahihi kila siku.
Sheria ya BWANA ndio Neno la MUNGU ambalo lipo kutusaidia hivyo kama sisi ni watu sahihi hatutakiwi kuwa mbali na Neno la MUNGU maana kuishi maisha ya kumpendeza MUNGU ni lazima tulifuate na kulitii Neno la MUNGU siku zote.

Japokuwa kuna Wakristo wengi sahihi lakini wameshindwa kuujua muda wao sahihi wa kufanya jambo sahihi ili wapokee kitu sahihi kuoka kwa MUNGU.
Kaina na Habili walikuwa Wacha MUNGU sahihi lakini Habili aliitumia nafasi sahihi katika muda sahihi kufanya jambo sahihi ambalo lilimletea baraka sahihi.
Biblia inasema kwamba 
'' Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. -Mwazo 4:3-7'' 

-Hapa tunajifunza kwamba Habili alifanya jambo sahihi katika muda sahihi hibyo akapokea baraka sahihi kutoka kwa MUNGU.
-Hapa pia tunajifunza kwamba Kaini hakufanya jambo sahihi japokuwa jambo hilo lisilo sahihi alilifanya katika muda sahihi hivyo hakupokea baraka sahihi.
Wakristo wengi wa leo huwa hawafanyi jambo sahihi katika muda sahihi hata wakapokea baraka sahihi.
unaweza ukakuta Binti/Kijana sio sahihi kwa sababu ni mzinzi, lakini licha ya kutokuwa sahihi lakini utakuta anataka kupata baraka sahihi jambo ambalo haliwezekani.
Wengine ni Wakristo sahihi kabisa lakini muda sahihi umefika na ameudharau japokuwa jambo lake ni sahihi hivyo wakati yeye atataka jambo hilo sahihi muda hautakuwa sahihi hivyo atakosa kupata baraka sahihi.
Lakini pia kuna watu sahihi walivumilia katika usahihi wao hata muda sahihi wa baraka yao ukafika hivyo wakapokea baraka sahihi.
 
Muda sahihi kwa mtu sahihi ukifika hakuna anayeweza kumpinga.

Hesabu 23:8,20 ''Nimlaanije, yeye ambaye MUNGU  hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye BWANA hakumshutumu? Tazama, nimepewa amri kubariki, Yeye(MUNGU) amebariki, nami siwezi kulitangua.''
 
Muda sahihi hutolewa na MUNGU na sio mwanadamu.
Muda sahihi ni muda wa mema na sio mabaya.
Muda sahihi hubeba baraka na ushindi.

Changamoto kwa watu wengi huwa hawajui tu muda sahihi ndio maana hubaki vile walivyo.

Mhubiri 3:1,7 '' Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena;''
 
Sio kila muda ni sahihi na ndio maana kuna muda wa kuomba ambao ni tofauti na Muda wa kuacha kuomba maana jambo hilo umejibiwa.
Muda wa jangwani ni tofauti na Muda wa Misri.

 Muda wa Kaanani ni tofauti na Muda wa jangwani.
Inawezekana kabisa Jangwani ulikuwa unapewa chakula cha mbinguni(Mana) Lakini kaanani unatakiwa ulime na BWANA atabariki kazi za mikono yako kama ukimtii. Hiyo ndio tofauti ya muda sahihi  na pahali sahihi kwa muda huo sahihi uliopo wewe mtu sahihi.

Utu wako ni wa thamani sana na unatakiwa kutunzwa sana.
Hakuna anayeweza kuutunza utu wako ila ni wewe mwenyewe.
Kama hutaweza kuutunza utu wako utakuwa hujui thamani ya utu wako ambayo MUNGU amekupa.


Waefeso 5:3-5 ''Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa KRISTO na MUNGU.''
 
Utu wako unatunzwa kwa;
-Wewe kukataa kutumiwa na shetani.
-Unautunza utu wako kwa kutenda yanayompendeza MUNGU tu.
-Unautunza utu wako kwa wewe kutunza Wokovu wako ambao kwa huo utafurahi milele katika uzima wa milele ambao BWANA YESU amekuandalia.

Ukiudharau utu wako hata ukafanya dhambi, hiyo ni kwa hasara yako mwenyewe.

 MUNGU anakupenda sana ndio maana uko hai leo kwa neema yake, fanya matendo mema ili uwe rafiki wa MUNGU siku zote.
Kama umeokoka hakika wewe ni mtu sahihi ambaye kwa maombi yako sahihi utapokea baraka sahihi.

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

Comments