JINSI YA KUMSHAURI NA KUMSAIDIA MTOTO ALIYEFIWA NA MZAZI/WAZAZI ,COUNSELING TRAINING!



Na Mchungaji Peter Mitimingi

1. Watoto Wasizuiwe Kuomboleza
Wakati msiba wa mzazi au wazazi wa mtoto, baadhi ya ndugu na marafiki wa karibu hujaribu kuwazuia watoto wasikabiliane na ukweli halisi wa tukio la msiba wa mzazi/wazazi wao kwa lengo la kuwafanya watoto hao wasijisikie vibaya wala kujisikia huzuni.

2. Watoto Wapate Nafasi ya Kuhuzunika na Kuwalilia Marehemu.
Ifahamike kwamba watoto pia wanahitaji wapate nafasi ya kulia, kuhuzunika na kuomboleza kwajili ya kifo cha mzazi/wazazi katika njia bora ambayo haitawaletea matatizo makubwa zaidi.

3. Watoto Wasaidiwe Kuelewa Undani wa Kifo cha Mzazi Wao.
Ili watoto waweze kuelewa kwa undani uhalisi na maana ya kifo,
wanapaswa kusaidiwa kuelewa mambo yafuatayo:
Waweza kujitofautisha wao na watu wengine.
Waweze kutofautisha walio hai na waliokufa.
Watofautishe wazo na uhalisia.
Waweze kutofautisha
o Wakati uliopita.
o Wakati uliopo.
o Wakati ujao.

4. Mtoto Asaidiwe Kuelewa Kwamba Marehemu Hatamuona Tena.
Kwamba mtoto anafahamu au hafahamu, ni lazima asaidiwe kufahamu kuhusu kifo na kwamba mtu anapokufa anakuwa ameondoka katika dunia hii na kwamba hatuta muona tena.

5. Mtoto Apewe Nafasi ya Kuelezea Hisia zake na Kuuliza Maswali Yake.
Mtoto apewe nafasi ya kuelezea hisia zake na kuuliza maswali yake yote aliyo nayo na wahusika wajaribu kumjibu mtoto maswali hayo kwa hekima na sio kumdanganya kwani wakati ukifika na akagundua kuwa alidanganywa ataumia sana na anaweza kujikuta akipata huzuni iliyopitiliza isiyo ya kawaida yaani (complicated grief).

6. Watoto Wasidanganywe Kwa Lengo la Kuwatuliza au Kuwasahaulisha.
Baadhi ya wahusika ili kumtuliza mtoto na kumfanya asijisikie vibaya, humdanganya mtoto na kumwambia mzazi wako amekwenda mbali sana na kumficha na taarifa yoyote ihusuyo ukweli halisi juu ya kufariki kwa mzazi wake.

7. Mtoto Asiposaidiwa Kuelewa Atamtarajia Kumuona Mzazi Tena.
Mtoto kama hatasaidiwa kuelewa vizuri kile kinachoendelea kwamba mzazi wake amefariki anaweza akaendelea kukua akitegemea kwamba kuna siku atakuja kumuona mzazi wake tena na kuhisi tu kwamba huenda kwa sasa amesafiri na kuna siku atarudi tena.

8. Watoto Wahusishwe Katika Msiba na Mazishi ya Mzazi Wao.
Baadhi ya wanasaikolojia wa watoto (child psychologist) na wataalamu wengine wanashauri kwamba hata watoto wadogo wa marehemu pale panapokuwa na uwezekano basi waweze kuhusika katika ibada ya mazishi na ikiwezekana kama kuna utaratibu wa kuaga mwili mwa marehemu kwa mara ya mwisho basi na wao waweze kupewa hiyo nafasi kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia sana kuondoa maumivu ya ndani na kuifanya safari yao ya makuzi kuwa bora zidi.



BAADHI YA MADHARA YANAYOWAKABIRI WATOTO AMBAO WALIOFIWA NA WAZAZI WAO NA HAWAKUPATA NAFASI YA KUOMBOLEZA IPASAVYO
COUNSELING TRAINING!

MADHARA YA KIHISIA (EMOTIONAL EFFECTS)
1. Wanakuwa na hofu sana.
2. Kama ni watoto wadogo mara kwa mara watakuwa wanajikunyata kwa wazazi wao.
3. Wanaweza kuwa waoga sana kwa watu wasio wafahamu au wasio wazoea.
4. Wanakuwa na uwoga katika maeneo ya giza.
5. Kila wakati wanakuwa na hofu kwamba kuna jambo baya linaweza kutokea wakati wowote.
6. Wanakuwa na hofu kwenda shuleni.
7. Wanakuwa na hasira sana na wachokozi kwa wenzao.
8. Watoto wadogo watakuwa wakipigana na watoto wenzao mara kwa mara.
9. Watoto wakubwa na hali ya uasi na ukaidi dhidi ya wazazi wao na walimu wao.
10. Wanapoteza shauku ya kuishi.

MADHARA YA MWILI (PHYSICAL EFFECTS)
1. Mtililiko wa kuongea una athirika (They are speech may be affected). Wanaweza kuwa na hali ya kigugumizi au kushindwa kuongea kabisa.
2. Wanaweza kukabiliwa na hali ya kupoteza hamu ya kula.(under eating)
3. Wanaweza kuwa na hali ya kula sana kuliko kawaida. (Over eating)
4. Wanaweza kulalamikia maumivu ya kichwa mara kwa mara.
5. Kuumwa na tumbo mara kwa mara.
6. Kuwashwa washwa sehemu mbalimbali katika mwili.
7. Wanaweza kushambuliwa na magonjwa ya kifua.

MADHARA YA KITABIA (BEHAVIORAL EFFECTS)
1. Wanaweza kuanza kufanya tabia ambazo walikuwa nazo wakati walipokuwa watoto wadogo zamani. Kwa mfano mtoto anaweza kuanza kurudia tabia ya kukojoa kitandani kama zamani au kuanza kunyonya vidole kama zamani.
2. Kuota ndoto za mang’amu ng’amu.
3. Kuota ndoto za vitisho
4. Baadhi ya watoto wanaweza kuwa wanagalagala (screaming) usiku wakiwa usingizini bila hata kushtuka kutoka usingizini.
5. Wanaweza kupenda kuigiza mambo ya michezo ya kivita mara kwa mara.
6. Kulia na kuwa na huzuni mara kwa mara.
7. Wanapoteza umakini katika vitu mbalimbali kwamfano kupoteza kiatu, nguo, toys, vitu vya kuchezea n.k
8. Kushindwa kufanya vizuri kimasomo darasani.
9. Watoto wakubwa wakubwa wanaweza kuanza tabia ya kunywa pombe na uvutaji wa sigara, bangi na hata madawa ya kulevya katika umri mdogo.
10. Wanaweza kujiingiza katika mambo ya mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo.

Comments