KATIKATI YA KILELE NA KILELE

Na Frank P. Seth

"Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi" (Zaburi 121:1,2).
Katika maisha hakuna namna utaweza kuwa KILELENI bila michakato ya maumiuvu ya KUPANDA ili kufikia kilele fulani. Hii naiita "njia za haki" (Zaburi 23:3), ukitaka kupanda kwa LIFTI au kwa HILA inawezekana pia, ila kuna gharama zake, mojawapo ya gharama ni KULA ILA KUKONDA NAFSI, yaani unapata kila kitu kama utakavyo ili unakuwa na HUZUNI moyoni hata kama watu wataona umefanikiwa kuwa kileleni. Paulo anasema, "Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali" (2Tim 2:5) na BWANA sema, "Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?" (Mathayo 16:26).
Maisha ya mwanadamu yoyote ni kama wimbi la kupanda na kushuka, au njia yenye vilima-vilima vingi. Ni dhahiri kwamba kuna wakati unavuka mahali unajisikia raha na unamshukuru Mungu kwa hatua hiyo ya kuinuliwa, ila ukitazama kwa mbali utagundua kuna KILIMA kingine mbele yako, na mara nyingine kinaweza kuwa KIREFU kuliko ulichoko sasa.
Tazama jambo hili, ili upande kilima kingine ni lazima USHUKE kilima ulichopo na utembee KUPANDA kilima kingine. Kadri unapanda juu, utagundua UNAONA mambo ambayo ulikuwa huoni kwenye KILELE cha kilima ulichopita. Ghafla! unajikuta upo kileleni tena na unajisikia amani na furaha na unaanza kumshukuru Mungu tena kwa mafanikio hayo. Natazama, kumbe! kuna kilele kingine mbele yako kirefu zaidi cha kupanda!
Nataka kuzungumzia hapo katikati ya kilima na kilima, yaani BONDENI. Ukiangalia Zaburi ya 23 utaona Daudi akiita baadhi ya mambonde ya namna hii "bonde la uvuli wa mauti". Uvuli maana yake, kukingwa na MWANGA, unajikuta uko mahali kama huoni mbele, maisha yamefunikwa na unaona kama hatua zako zimekamatwa. Kila ukifanyacho hukioni, ila giza. Kumbuka, kila mtu anapita BONDENI kwa wakati tofauti ili kupanda KILELE fulani. Ukikata tamaa, huo uvuli wa mauti utakumeza na kufia biondeni. Kataa kufia mabondeni.
Hebu piga picha kwamba uko bondeni sasa, katikati ya kilima na kilima. Angalia, jua likichomoza, utagundua unachelewa kuona mwanga kwa maana kilima fulani kinakuzuia (kinakuwekea uvuli), na mara! Jua litokezapo, japo kwa kuchelewa, kabla hujalifaidi na kuona mambo yako vyema, kumbe! kilima kingine kimelizuia jua wakati wa kuzama kwake, mwanga unaondoka mapema. Giza linaendelea kutanda. Hapo ni bondeni, kati ya kilele na kilele.
Sasa chunga jambo hili, kuna makundi mawili ya watu: Kundi la kwanza wataanza kumlaumu kila MTU aliyeko juu kwamba haleti msaada huku chini bondeni wakati wewe unaangamia. Kundi la pili ni wale ambao wakiinua macho wanona VILELE ila wanajua msaada wao unatoka kwa MUNGU. Badala ya kumlaumu mtu, wanang'ang'ana na Mungu wao (Zab 121). Mara nyingi hawa watu wa kundi la kwanza hufia bondeni au hujikuta wakipanda kwa "njia zisizo halali" huku wakijifariji kwa maneno kama, "kila mtu anafanya hivi", au "bila kuwa na refarii mjini hutoki", au "dunia hii bila hela mambo hayaendi", nk.
Angalia jambo jingine, Bwana akiwa Mchungaji wako, hutapungukiwa na kitu, yeye hukupa malisho (kukufundisha), kukuhuisha (kukupa uhai maana unajikuta katika hali za kufani) na kukuongoza, ila KATIKA NJIA ZA HAKI kwa ajili ya jina lake, ndipo BONDENI huwa ni mahali pa USHUHUDA na sio pa AIBU kwa sababu japo uko na WATESI wengi, mbele yao UTAKULA na wao wataona unavyovukilia KILELE kingine.
"BWANA ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa BWANA milele" (Zaburi 23:1-6).
Frank P. Seth

Comments