KWANINI WEWE HUSHUHUDII WENGINE ILI WAJE KWA YESU?

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze neno la Muhimu sana.
Moja ya kazi muhimu ambayo kila mkristo amepewa na MUNGU ni kushuhudia kwa wengine habari njema za ufalme wa MUNGU.
Biblia inawaita wakristo waliookoka kwamba jina lao ni ''Watangaza fadhili za BWANA''
Zaburi 103:17 ''Bali fadhili za BWANA zina wamchao Tangu milele hata milele, Na haki yake ina wana wa wana;'' 

=Una neema wewe maana umempokea BWANA YESU na hakika umeokoka, lakini kuokoka kwako kuna maana kwamba uepukane na dhambi na pia kuokoka kwako ni ili uwasaidie na ndugu zako kuokoka. Ndio maana Biblia inakuita wewe ni mtangaza fadhili za BWANA YESU.
Biblia haikuishia hapo bali inasema ''Mwimbieni BWANA, libarikini jina lake, Tangazeni wokovu wake siku kwa siku. Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, Na watu wote habari za maajabu yake. Kwa kuwa BWANA ni mkuu mwenye kusifiwa sana. Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote. Maana miungu yote ya watu si kitu, Lakini BWANA ndiye aliyezifanya mbingu. Heshima na adhama ziko mbele zake, Nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake. Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu, Mpeni BWANA utukufu na nguvu. Mpeni BWANA utukufu wa jina lake, Leteni sadaka mkaziingie nyua zake. Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu, Tetemekeni mbele zake, nchi yote.   -Zaburi 96:2-9''

=Inawezekana kabisa ndugu hujui jambo hili lakini naomba ujue kwamba BWANA YESU amekupa jukumu la wewe kuwa shahidi wake kwa watu wengine.
Mathayo 28:19-20 ''Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la BABA, na MWANA, na ROHO MTAKATIFU; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.''

=Inawezekana kabisa hujui uanzie wapi kushuhudia.
=Inawezekana kabisa unawaza labda kama ukipata neema ya kwenda chuo cha Biblia ndipo utaanza kushuhudia wengine habari za ufalme wa MUNGU. Lakini ulishawahi kujiuliza swali hili kwamba ''Kama kila siku watu wanakufa, je hadi umalize chuo ndipo ushuhudie, je watakuwa wamekufa watu wangapi ambao ulitakiwa wewe uwashuhudie kabla hawajafariki?''
Jibu ni wengi sana. Lakini BWANA YESU anatuambia mimi na wewe leo kwamba
 '' Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.-Marko 16:15''

MUNGU mwenyewe ndiye aliyeanza kushuhudia na akatupa kielelezo sisi wateule wake.
MUNGU aliandaa njia ya wokovu moja tu kwa wanadamu wote na njia hiyo ni YESU KRISTO pekee hivyo MUNGU mwenyewe akawa wa kwanza kushuhudia njia ya wokovu aliyoiandaa mwenyewe.

1 Yohana 5:9b ''Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa MUNGU  ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa MUNGU ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe.''
 
Dada mmoja aliyekuwa mgonjwa sana kule Zanzibar alishuhudiwa kila siku kwamba aokoke na BWANA YESU atampa uzima wa milele, Dada yule alikuwa katika kukubali kuokoka lakini ndugu zake wakamkemea na kumshauri kwamba asikubali kuwa mkristo. Yule dada aliwasikiliza ndugu zake na jioni moja vijana wenzangu ambao tulikuwa tunashuhudia pamoja walimtembelea na kumwambia habari za kuokoka, akakataa na kuanza kumsanifu BWANA YESU. Kwa sababu ziku zake za kuishi zilikuwa mwishoni kabisa na alikuwa mgonjwa mahututi hivyo aliikataa neema ya KRISTO maana BWANA YESU alitaka kumwokoa hata katika mazingira yale, Dada alikataa lakini baada ya hapo haikupitia hata wiki moja yule dada akafariki lakini wakati anafariki alianza kulia kwa nguvu sana huku akimtaja BWANA YESU, Yule Dada katika mazingira ya roho yake kuachana na Mwili ni kama alimuona BWANA YESU maana alianza kulia na kumwita YESU amsaidie, aliona anakoelekea siku hivyo alimhitaji BWANA YESU maana hapo ndipo alipojua kwamba nje na KRISTO YESU hakuna uzima wa milele. alikufa akiita YESUUUUUUUUUUUUU.
Mimi na wewe hatuwezi kujua baada ya hapo lakini napenda kukuambia kwamba kama Watu tuliookoka tunalo jukumu Kubwa sana la kuwashirikisha wengine upendo wa MUNGU wa wokovu.
Inawezekana kabisa hujui utaanzaje kushuhudia lakini lakini mimi najua ukiamua unaweza sana hata kama umeokoka jana tu.
Ngoja nikupe ushuhuda huu mwingine.
Kwa muda wa miaka mitatu na nusu sasa nimeandika masomo mtandaoni zaidi ya 400, Katika masomo hayo sikuacha hata siku moja kumwambia mtu kwamba anatakiwa aokoke. Kijana mmoja ambaye ni Mkristo anaishi mkoa wa mbali sana kutoka hapa Dar es salamm alijiona hawezi kushuhudiwa wengine japokua alitamani sana kushuhudia, na ndani yake kulikuwa na agazo la kuwashuhudia wengine.  Alichokifanya kijana yule ni kuingia katika blog yangu na Ku-copy baadhi ya masomo yangu Kisha kuya-Print Kwenye karatasi nyingi na kuingia mitaani kuwagawia watu aliokutana nao bila kuwaeleza mambo mengi maana alijiona hajui, Kwa njia hiyo aliwashuhudiwa wengi na hadi anakuja kunipa ushuhuda huo alikuwa amewashuhudia watu wengi sana.
Hiyo ni njia mojawapo tu ya kushuhudia, yeye alitumia gharama kidogo lakini ujumbe niliokuwa  nimeuandika ndio ulioshuhudia maana ulikuwa ni ujumbe mkali wa kuonya na kuwataka watu waokoke.
Ndugu yangu kama huyo kijana alitumia ujumbe wangu kushuhudia na akapata kondoo wengi je mfano kwa njia hiyo tu ya yule ndugu kama watu 500 wakifanya hivyo itakuwaje? maana mitandaoni kuna masomo mengi sana ya watumishi mbalimbali wa kweli wanaofundisha Wokovu kila siku hivyo kama watu watakuwa wanatumia jumbe hizo kuwasaidia na wengine unadhani injili haitawafikia watu wengi zaidi?
Kwa MUNGU hakuna kazi ya hasara, wewe ukishuhudia haijalishi umetumia ujumbe wa nani lakini Thawabu yako iko mbinguni na MUNGU atakulipa. Wewe utakuwa mtu mwenye faida zaidi katika ufalme wa MUNGU.
Wewe utakuwa mtumishi wa MUNGU.
Kuna njia nyingi sana za kushuhudia hata kama hujui uanzeje.
=Mfano kama kuna mkutano wa injili mahali fulani na wewe ukamwalika mtu mmoja mwende naye kwenye mkutano huo na yeye akaenda akalipokea Neno la MUNGU basi hakika hapo umeshuhudia.
=Kama kuna kipindi fulani kwenye redio ambako injili halisi inahubiriwa kisha wewe ukamwalika mtu kusikiliza kipindi hicho cha mahubiri, hakika hapo umeshuhudia.
=Kama wewe utajiwekea malengo kwamba kila mwaka lazima uhakikishe unapeleka watu 5 kanisani hakika utaweza maana MUNGU atasimamia maono yako hayo kwa utukufu wake.
Kila Mteule wa BWANA YESU anatakiwa ashuhudie injili kwa watu wengine.
 1 Petro 4:10-11 ''kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za MUNGU. Mtu akisema, na aseme kama mausia ya MUNGU; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na MUNGU; ili MUNGU atukuzwe katika mambo yote kwa YESU KRISTO. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina.''
 
=Hata kama utashuhudia harafu hakuna aliyeokoka wewe usijali maana hapo umepanda mbegu na mbegu yako hiyo ipo siku itaota tu.
Wewe ni Wakili wa BWANA YESU maana yake unamwakilisha BWANA YESU katika kuwakusanya kondoo wake, fanya kazi hiyo ya uwakili kwa uaminifu na utapewa taji mbinguni.
1 Kor 4:1-2 ''Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments