LAANA ZA WACHAWI


Na:     AMOS  KOMBA (RP)
& DR. GODSON ISSA ZACHARIA (SNP)
Utangulizi: Kuna laana nyingi zimeandikwa katika Biblia. Mathalani, miongoni mwa hizo laana ni kama vile:-
1.      Laana za wazazi (kwa asiyemtii baba na mama), 
2.      Laana ya wanadamu,
3.      Laana zitokanazo na dhambi,
4.      Laana ya kutokulipa fungu la kumi
5.      Laana ya wachawi.
Je, Laana ni kitu gani? Laana ni jambo/tukio baya linalokusudiwa na mtu mmoja ili limpate mtu mwingine kwa minajili ya kuharibu maisha yake. Laana ni maneno yanayotamkwa na mtu ili kumpata mwingine. Mfano katika Biblia, Nuhu alipokuwa mkulima wa ardhi, alikunywa mvinyo na akalewa, akaanguka njiani na akabaki uchi, na mwanae mdogo akaenda kuwaeleza ndugu zake mambo hayo. Hata hivyo wanae wengine walichukua nguo wakarudi kinyumenyume wakamvisha nguo baba yao. Nuhu  alipozinduka akamlaani Kanaani (mjukuu wake /mtoto wa mwanae aliyeuona uchi wake).
Wachawi nao wanao uwezo wa kutamka laana katika maisha yetu. Lengo la laana mara zote ni kusababisha mtu afe, au awe maskini, awe mgonjwa n.k. Nyakati  nyingine wachawi hutamka laana siyo mtu afe, bali kumtesa kwa magonjwa. Kumbuka kuwa maneno ni  roho. Imeandikwa YOHANA 6:63bmaneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.  Mchawi akitamka maneno katika ulimwengu wa roho, anaziachilia roho. Atamkapo  ugonjwa,  yale maneno hugeuka kuwa roho la ugonjwa alioutamka na kufanya kile kilichokusudiwa kitokee.

Wachawi hutekeleza laana zao hizi katika madhabahu za kichawi. Mchawi ni mwanadamu. Akiwa peke yake hawezi kukulaani. Anachokifanya ni  kuzitumia roho za kichawi ndani mwake katika kufanya laana hiyo. Mchawi huyu huenda katika kikao  cha wachawi kwa ajili  ya kupeleka hoja / mashtaka dhidi ya mtu  aliyekusudiwa. Msingi wa yote haya ni “wivu”.
Imeandikwa katika HESABU 22:1-3.. [Kisha wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi tambarare za Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu ya Yeriko. 2 Na Balaki mwana wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli wamewatendea Waamori. 3 Moabu akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu akafadhaika kwa sababu ya wana wa Israeli.]… Tatizo la Moabu hapa ni kuona wana wa Israeli wakiwa wengi na yale matendo waliyowatendea Waamori. Inawezekana hata wewe una ndoa nzuri, wapo wengine wanafadhaika kwa sababu hiyo. Inawezekana unajifungua watoto wengi wazuri, na papo hapo wapo wengine wanafadhaika kwa sababu hiyo.
Imeandikwa katika HESABU 22:4 ...[Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile.]… Katika ulimwengu wa roho, kuna kamera za kumulika maendeleo ya watu wengine. Uwoga wa wachawi ni kuona watu wakiwa wengi kwa sababu vitu vyao vitarambwa kama ngo’mbe arambavyo majani. Kumbe ni vizuri kukusanyika sehemu ya pamoja kanisani ili kuweza kuomba pamoja na kuramba vitu vya wachawi kwa Jina la Yesu.
Imeandikwa katika HESABU 22:5-6…[Basi Balaki akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama,kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi. 6 Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.]… Hapa Balaki aliona wingi  wa wana wa Israeli na kujua hakika akipigana nao watamshinda. Kumbe mtu mwenye nguvu huwezi  kumshinda kirahisi, bali wachawi  wanachoweza kufanya ni kumlaani wemnye nguvu‼!.

UKIRI
Mashetani wote wa laana majini, wote wa laana, leo naipiga laana zenu kwa Damu ya Yesu. Wasimamizi wa laana kwenye maisha yangu, leo nawaondoa kwa Jina la  Yesu. Imeandikwa neno la Bwana ni moto,  na mimi leo nageuka na kuwa  moto kwa jina la  Yesu. Amen

Imeandikwa katika HESABU 22:7-12...[Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki. 8 Akawaambia, Kaeni hapa usiku huu, nami nitawaletea jawabu kama Bwana atakavyoniambia; wakuu wa Moabu wakakaa na Balaamu. 9 Mungu akamjia Balaamu, akasema, Ni watu gani hawa ulio nao pamoja nawe? 10 Balaamu akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema, 11 Tazama, kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza. 12 Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa..]… Mtu mwenye laana hawezi kufanikiwa. Hata hivyo, sisi tuliookoka tunao  uwezo wa kubadili laana zao na kufanyika baraka kwetu kwa Jina  la Yesu.
UKIRI
Kila kilichotoka kwenye mikono yangu halafu kikanifunga nakataa kwa Jina la Yesu.  maneno yoyoyte yaliyotamkwa leo nayafuta kwa Jina  la Yesu. Ninauteka ulimwengu wa roho, ulimwengu uliojaa laana nauteka kwa Jina la Yesu. Amen


Imeandikwa katika ISAYA 54:17…[Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.]…Kila anayelaani anao ulimi. Leo tunaenda kuhukumu ndimi za kina mama na kina baba zilizoinuka kinyume nasi kwa Jina la Yesu. Kila laana za wachawi zinazohusu taifa la Tanzania, leo tunaziondoa kwa Damu ya Yesu.

Maombi yetu leo yatalenga maeneo makuu matatu:

1.      Maombi ya kutoka kwenye laana. Ili ufanikiwe ondoa laana kwanza. Ukiondoa laana ujue matunda ya laana hayatamea tena.
2.      Kuyaondoa Mashetani yanayosimamia laana.  Yapo mashetani yanafanya kazi kwa njia mbili: Yakiwa nje ya mwili  wako au yakiwa ndani ya  mwili wako.
3.      Kuzishinda damu /sadaka za laana zote. Leo tutanyamazisha damu  zingine zote kwa kutumia Damu  ya mjumbe wa Agano Jipya (Yesu Kristo).

Hata hivyo kama haujaokoka siyo rahisi kuweza kuzitoa laana. Utakapookoka utapata faida za aina mbili: Yesu ambaye ana vitu vyote ataingia ndani mwako na kisha atakupa vyote unavyohitaji. Faida ya pili ni kuwa na nguvu ya kuwashinda wachawi na laana zao.

Comments