MKE MWEMA AU MUME MWEMA YUKOJE?

Na Mtumishi Peter Mabula, hapa akiwa na mkewe Scholar Mabula siku ya harusi.
BWANA YESU atukuzwe.

Karibu ujifunze kitu cha kukusaidia.

Kama kuna wanaoteseka zaidi katika suala la kupata wenzi wao wa maisha basi wanawake ndio wahanga zaidi.

Uhanga wa wanawake mara nyingi unakuja kwa sababu wao ndio huchaguliwa na sio wao kuchagua.

Hata kama wakichagua ni katika kukubali tu maana kijana wa kiume ndio hujitokeza kwanza, Wanawake wana uhuru wa kukubali au kukataa lakini huyo wanayemkataa au kumkubali ndio huchagua kwanza na binti ni mpelekewa taarifa tu.
Ukiona binti kachaguliwa na kijana fulani ili aposwe na baadae waje wafunge ndoa takatifu ujue kuna sababu.
Sababu kadhaa za binti ndizo zitamfanya huyo kijana amchumbie huyo binti na sio mwingine. Kwa kijana huyo, sio mabinti wote wana hizo sifa kama za huyo aliyemfuata ndio maana hakuwafuata wao ila amemfuata huyo.

Mithali 19:14 '' Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA.'' 

 Ipo kazi kumpata mke mwema kama ilivyo kazi pia kumpata mume mwema.
Unajua maana ya mke/mwema?
Mke mwema hutoka kwa MUNGU, na kama hutoka kwa MUNGU basi huyo hutokana na MUNGU na sio akili zako.
Mke mwema au mume mwema ni yule mwenye sifa mbili.

   1. Ni Mcha MUNGU na mwemye hofu ya MUNGU.
  2.  Ni yule ambaye mnaendana kwenye ulimwengu wa roho. au kwa lugha nyingine niseme ni yule ambaye mko pair moja na wewe kwenye ulimwengu wa roho.
Ni kama kufuri moja ambalo lina funguo 2 tu.
Funguo hizi hutegemeana, na hufanya kazi moja kulifungua kufuri, ukileta ufunguo mwingine kufuri halitafunguka. Kufuri ni mfano wa ndoa ambapo kufuri hilo lina funguo zake tu 2 special za kulifungua. 
Kama ufunguo mmoja ukipatea maana yake mwanandoa mmoja akifariki basi master key anayo ROHO MTAKATIFU tu na sio mwingine yeyote. 
funguo hizo pair moja kwingine haziwezi kufungua na ukiupoteza ufunguo mmoja ujue hata ukiazima ufunguo mwingine hautaweza kulifungua kufuri hilo maana ufunguo huo mgeni sio pair yake.
Kuna watu hudhani mke/mume mwema ni lazima awe yule mpole na mtaratibu huku amejaa tabasamu masaa yote. Hiyo sio sababu ya kiroho na mke/mume mwema.
Mke mwema au mume mwema ni lazima awe na sifa hizo zote mbili yaani ucha MUNGU na kuendana na wewe kwenye ulimwengu wa roho.
Kuna wacha MUNGU wengi lakini sio wote mko pair na wewe katika ulimwengu wa roho.
Mke mwema au mume mwema huumbwa katika ulimwengu wa roho kabla ya kuja katika ulimwengu wa mwili

Mwanzo 1:27 '' Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa MUNGU alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. '' 

-Tukio la andiko hili la kuumbwa kwa Adamu na Eva linaonekana  kabla ya Adamu hajaletewa usingizi mzito ili ubavu wake uondolewe ili aumbwe Eva.
-Unaweza ukajiuliza kwanini katika uumbaji wa MUNGU wa siku 6 kabla ya siku ya saba ya kupumzika MUNGU baada ya kumaliza uumbaji lakini wakati huo Eva hakuwa ameumbwa?
Jibu ni kwamba ni kweli katika siku 6 za uumbaji wa MUNGU Eva alikuwa hajaumbwa katika ulimwengu wa mwili tu lakini katika ulimwengu wa roho Eva alikuwepo ndio maana andiko hapo juu linaonyesha Eva alikuwepo rohoni kabla ya kuja kutokea mwilini.
Ndivyo inavyotakiwa kwa kila Mwanamume  ahakikishe anaomba ili Eva wake ambaye yuko ulimwengu wa roho atokee ili wafungue ndoa.
Na ndivyo inavyotakiwa kwa kila Mwanamke ambaye hajaolewa aombe ili Adamu wake ambaye yuko katika ulimwengu wa roho atokee ili wafunge ndoa.
Kwenye kutokea kwa huyo ambaye yuko katika ulimwengu wa roho ndipo kuna kasheshe sana, nitafafanua muda mwingine maana wengi pia wamenasa huko.
Kuna binti mmoja alikuwa amepanga chumba katika nyumba kubwa ambayo wamepanga wapangaji wengi akiwemo kijana mmoja.
Binti siku moja akiomba kwa sauti kijana yule akasikia akiwa chumba cha pili na akagundua kabisa kwamba binti alikuwa anaomba MUNGU ili apewe mume mwema maana alimsikia akiomba. Kesho yake kijana akamfuata binti na kumweleza kwa hila  kwamba Ameonyeshwa kuwa yule binti ndiye atakuwa mke mwema wake. Binti alifurahi sana ila akasema atatoa jibu kesho yake. Usiku wa siku hiyo MUNGU alisema na yule binti kwa ndoto kwamba yule sio mume wake. Kesho yake akamwambia yule kijana kwamba sio kweli katika kile alichosema jana yake na ni kweli kijana akasema alivyotaka kufanya usanii.
Ndugu, uwe makini sana katika hatua za kupata mchumba.
Binti mmoja pia kwa sababu ya kuwakataa vijana, kuna kijana mmoja aliamua kufanya kituko ili ampate yule binti. yule binti alikuwa ameokoka na ni muombaji mzuri ila chumba alichokuwa amepanga hakikuwa na dari. kijana yule akanunua tochi kubwa sana  na kuichaji sana.
Kwa sababu alikuwa anajua masaa ya yule binti kuomba basi alinyata na kupanda kwenye dari ukutani ambako vyumba vyao vinapakana na chumba cha yule binti. yule kijana alipofanikiwa aliiwasha tochi kubwa ghafla na kujigeuza sauti akisema ''wewe binti yangu utaolewa na kijana fulani''
Yule binti kwa furaha akamshukuru MUNGU na kutoka hadi nje kwa furaha, wakati anatoka yule kijana akarudi chumbani kwake na baadae yule binti aliporudi chumbani kwake aliikuta tu koroboi yake ndogo inawaka na akajua kabisa ule ulikuwa ni ujumbe wa MUNGU maana aliuona hadi utukufu wa MUNGU kumbe tochi ya msela.
Ndugu, Ni muhimu sana kuwa makini sana na muombaji sana tena ukiwa mtu wa rohoni sana.

Mithali 31:10A '' Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? ''

Mke Mwema au mume mwema wako huwa mnakuwa mmeunganishwa katika ulimwengu wa roho na kuwa kitu kimoja kamili kisicho na dosari.
Wakati mwingine wewe unaweza ukawa jicho na yeye akawa mboni ya jicho maana yake ukiondoa kimoja tu kati ya hivyo basi ujue jicho halitaona.
Anaweza akaona mengi kwenye ulimwengu wa roho ya kwako maana wewe ni sehemu ya Mwili wake.
Mke/mume mwema atakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kukuvumilia hata pale ambapo ungeoa/olewa na asiye wa kwako asingevumilia kiasi hicho.
Mke/Mume mwema wako anaweza akakubebea mzigo katika ulimwengu wa roho kiasi kwamba ungeoa/olewa na asiye pair na wewe hakika asingeweza kuubeba mzigo huo.
Kuna watu wameoana na wanajiita mke mwema na mume mwema lakini kitendo cha mwanaume kufungwa gerezani tu mwaka mmoja na nusu, mwanamke huku nyumbani anasema siwezi kuvumilia muda wote huo, huyo hakuwa mke mwema wala hafanani kuwa mke mwema.
Unakuta wanandoa wanajiita mke mwema na mume mwema lakini kitendo cha kukosa tu mtoto inaanza vita na mmoja kati yao anaanza kulaumiwa na kusaliti ndoa  maana mwenzake hazai, huyo hakuwa mke mwema wala mume mwema maana hata hafanani.
Mke mwema au Mume mwema wako lazima mume na sifa za kuwa mwili mmoja katika ulimwengu wa roho.

Mwanzo 2:24 ''Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.'' 

-Hamuwezi kuwa mwili mmoja kisha mnapigana kila siku na matusi mengi kila dakika.
-Huwezi kuuchukia mwili wako ambao ni mke mwema wako au mume mwema wako.
Andiko la mwanzo kabisa hapo juu limesema kwamba ''Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA. ''
Kwanini Busara?
Ni Kwa sababu  '' Busara itakulinda;-Mithali 2:11A''
Kama mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA, basi busara ya huyo mke mwema au mume mwema itakulinda.
Mwenye busara hata kama yakitokea magumu katika ndoa yenu basi busara yake humtuma kufunga na kuomba ili magumu yaondoke.
Asiye na busara wakati wa magumu hutaka kutafuta msaada kwa waganga na kuleta laana badala ya baraka katika ndoa yetu.
Asiye na busara hata kama ataambiwa tu na mumewe kwamba ''mbona amezidisha chumvi katika mboga'' Yeye hubeba vyombo na nguo zake na kurudi kwao.
Asiye na busara kila siri ya ndoa lazima awapelekee marafiki zake saluni.
Asiye na busara  ni tofauti sana na mwenye Busara.
Mke Mwema ndio pia mweke Mwenye Busara maana mke Mwema hutoka kwa BWANA na mke mwenye Busara hutoka kwa BWANA kama maandiko yanavyosema.
Ni vizuri sana kumhitaji mke Mwema wako au mume mwema wako na huyo hupatikana kwa BWANA pekee.
Mithali 18:22 ''Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA. ''

Licha ya hayo yote tuliyojifunza lakini pia Jitahidi sana jina lako lisiwe kwenye chupa za soda tu bali Liandikwe kwenye kitabu cha uzima wa Milele .
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com


Hapa ni siku nafunga ndoa kule Mwanza 20 Sep 2014

Comments