ROHO MATAKATIFU KATIKA MAOMBI YAKO NI MUHIMU SANA.

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze lakini kabla ya ujumbe leo nataka tuombe.

Tuombe;

''Tunakushukuru MUNGU BABA Kwa Kuwa Wewe U Mwema, Na Kwa Maana Fadhili Zako Ni Za Milele. Ikawa Asubuhi Na Ikawa Jioni Bado Tunaishi Kwa Kulindwa Na Wewe. 
U MUNGU Milele Na Utabaki Kuwa MUNGU, Unaitwa NIKO AMBAYE UKO Na Ndio Maana Hata Kufika Leo Umekuwako Ukitulinda. 
Hatuna Cha Kukulipa Ambacho Kinalingana Na Upendo Wako. Wakati Maadui Zetu Wakiumiza Vichwa Ili Watudhuru, Malaika Wako BWANA Uliowatuma Wanaumiza Vichwa Kwamba Wawapige Wapi Maadui Zetu.
 Tunakushukuru BWANA Kwa Uzima Na Ushindi Uliotupa. 
Najua BWANA Wewe Unayajua Mawazo Yetu, Tena Unasikia Maombi Yetu, Unatazama Neno Lako Na Hakika Unatujibu Maombi Yetu. 
Tunapenda Kukuabudu Kila Dakika Maana Wewe Ndio MUNGU. BWANA MUNGU Asante Kwa Silaha Ulizotupa, Umetupa Neno Lako Na ROHO Wako, Umetupa Damu Ya YESU Na Jina La YESU Ndio Ndio Silaha Ambayo Adui Zetu Huziogopa. Tumeshinda Kwa Wewe BWANA Na Tutashinda Tena Na Tena Kwa Wewe JEHOVAH BWANA, Jina Lako Libarikiwe Milele. Ni Kwa YESU KRISTO Na Kwa Jina La YESU KRISTO Aliye Hai Milele timeomba. 
Amen Amen''

Baada ya maombi naomba tujifunze neno hili.
Maombi kwa mkristo ni jambo la kudumu.
Maombi ni maisha.
 Kuomba Maombi Katika ROHO MTAKATIFU Ni Muhimu Sana. 

 Waefeso 6:18 ''kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika ROHO, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;''

Ngoja nikupe ushuhuda huu mfupi.
Kuna Wakati Nilikuwa Na Mzigo Wa Kuwaombea Watu Fulani Wengi Ili MUNGU Awasaidie, Walinisihi Sana Niwaombee Na Rohoni Niliambiwa Kuwaombea.
 Jambo Hilo Halikuwa La Siku Moja, Na Niliomba Huku Na Mimi Nikiwa Katika Wakati Mgumu Sana Maana Huduma Yangu Mtandaoni Ilikuwa Inapigwa Vita Kuliko Kawaida Pia Kwenye Ulimwengu Wa Roho Niliona Mashambulizi Makubwa Dhidi Yangu Kwa Sababu Ya Neno La MUNGU.
 Nilitamani Kuombea Huduma Yangu Hiyo Lakini Rohoni Niliona Tu Agizo La Kuwaombea Wale Ndugu Waliokuwa Kwenye Matatizo Makubwa Sana Wakati Huo. 
Nilichojifunza Ni Hiki Kwenye Maombi Fuata Maamuzi Ya ROHO MTAKATIFU Maana Wakati Mimi Nawaombea Wale Ndugu Kuna Mama Mmoja Mwanza Aliona Hatari Iliyokuwa Inanikabili Aliagizwa Na ROHO Kufunga Siku 5 Ili Kuniombea. Hapa Unaona Umuhimu Wa ROHO Kwenye Maombi Maana Nilipokuwa Nawabebea Mzigo Wengine Ndipo Na Mimi Nilibebewa Zaidi Mizigo Yangu.

Ndugu Zangu Ombea Unalosukumwa Kuliombea Maana Hilo Ndilo Muhimu sana Kwako Kwa Wakati Huo.
Inawezekana kabisa umefunga ili uombee kupata mchumba lakini ulipoanza tu kuomba ukawa  unasikia msukumo wa kumuombea tu mtumishi fulani wa MUNGU, ambaye hata humjui na hata kama unamujua lakini hujui kama yuko katika wakati mgumu. lakini kwa MUNGU hakuna kazi ya hasara.
 inawezekana kabisa kitendo cha wewe kumuombea mtumishi wa MUNGU ndio kinatoa jibu la hitaji lako. Mtumishi yule wa MUNGU baada ya kuvuka katika jaribu alilokuwa nalo kwa sababu ya maombi yako yaliyomvusha iko siku ROHO wa MUNGU ambaye ni yeye yule kwako na kwa mtumishi yule anaweza akamtumia mtumishi yule kukutabiria jambo la baraka yako ya ndoa ambayo hata kama wangekupinga wachawi 60 bado utashinda maana ROHO wa MUNGU yuko kazini.

1 Kor 12:6-11 ''Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU  ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa ROHO kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa ROHO apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo ROHO yeye yule; mwingine imani katika ROHO yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika ROHO yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.'' 

Ni muhimu sana kuongozwa na ROHO MTAKATIFU maana yeye anaweza kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja.
Katika maombi pia ni muhimu sana kuomba katika ROHO maana kile ROHO atakuambia uombee ndicho muhimu zaidi kwako kwa wakati huo.
Wako watu walikuwa wana mahitaji yao mazuri tu lakini walipoanza kuomba ROHO alisema nao kwamba wawaombee watu fulani ambao ni maadui zao, ni ngumu wewe mwenye adui zako harafu uambiwe uombee adui zako, kibinadamu ni kama haina faida lakini jambo hilo ndilo muhimu zaidi kwako kuliombea kwa wakati huo maana ROHO wa MUNGU analiona jambo mwisho kabla ya mwanzo. Inawezekana wewe hupokei kwa sababu ya chuki uliyonayo moyoni mwako dhidi ya watu fulani lakini kwa kuambiwa uwaombee hao  unaowachukia itakufanya uweze kuwasamehe kisha ndipo utapokea baraka yako unayoiombea kila siku.
 Kwa Mkristo aliyeokoka ni lazima aenende kwa ROHO, Ni lazima amtii ROHO wa MUNGU siku zote na Biblia inasema hivi 
'' Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.-Wagalatia 5:25''

 Jambo la kujua ni hili;
 =Alipo MUNGU Na YESU Yuko Hapo Hapo.
=Alipo YESU Na ROHO MTAKATIFU Yuko Hapo Hapo 
= Alipo ROHO MTAKATIFU Na Damu Ya YESU Ipo Hapo Hapo. 
=Alipo MUNGU BABA Na MUNGU MWANA pia ROHO MTAKATIFU Wapo Hapo Hapo. 
Ni muhimu sana pia kuijua hii tahadhari inayotolewa na Biblia kwamba  ''Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya ROHO wa MUNGU; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.   -1 Kor 2:14 ''

Je, wewe ni mwanadamu wa tabia ya mwili au rohoni?
Mwanadamu wa tabia ya mwilini hawezi kupokea maagizo ya ROHO MTAKATIFU wala hawezi kuyaelewa wakati mwingine maana maagizo ya ROHO wa MUNGU hutambulikana kwa jinsi ya Rohoni na sio mwilini.
Tamani kuomba katika ROHO MTAKATIFU.
Omba ROHO akujaze ufahamu wa kiMUNGU na akujaze nguvu zake.
Hakikisha unakuwa mtu wa Rohoni na sio mwilini maana mambo ya MUNGU ambayo unayahitaji hupatikana Rohoni na sio mwilini.
Kama wewe ni mtu wa mwilini kisha unataka baraka za rohoni basi itakusumbua sana maana inabidi uwe mtu wa rohoni ndipo utapokea vya rohoni.
1 Kor 2:11 '' Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya MUNGU hakuna ayafahamuye ila ROHO wa MUNGU.'' 

 =Mambo ya MUNGU ayafahamuye ila ROHO  wa MUNGU. 
Kwa maneno mengine ina maana ya kuwa, ikiwa tunahitaji kuyafahamu mambo ya MUNGU inatubidi tujifunze kushirikiana na ROHO MTAKATIFU.
Naamini hakika kuanzia sasa utakuwa mtu wa rohoni na sio mtu wa mwilini.
Mtu wa rohoni ni mwana maombi na hujiunga na kundi la maombi kanisani.
Mtu wa rohoni hujifunza Neno la MUNGU na kuliishi.
Mtu wa rohoni ni mwaminifu kwa MUNGU.
Mtu wa Rohoni maisha yake amemkabidhi BWANA YESU na anatembea katika utakatifu wa kweli.
 ' Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.-Wagalatia 5:25''
Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili. 
 

Comments