UKOMBOZI WAKO UNAPATIKANA KWA MAAMUZI YAKO MWENYEWE.

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
MUNGU ameachilia vitu fulani ambavyo kama tukivishika  vitatuvusha na kutupeleka sehemu nyingine nzuri.
Ndugu mmoja kabila mmasai aliambiwa ajitetee mahakamani, akakimbia baada ya kuambiwa ajitetee, na watu wa mahakama wakashindwa kumkimbiza maana badala ya kumkimbiza wakabaki wakicheka tu, lakini hiyo ndio ikawa pona yake yule ndugu mmasai. Yeye aliambiwa ajitetee kwa maneno yake yeye akajitetea kwa miguu yake lakini akapona maana alijitetea.

Warumi 10:9-11 ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.'' 

Neno la MUNGU linatupa jinsi ambavyo tunaweza kuokolewa na kuupata uzima wa milele bure, Lakini watu wa MUNGU wengi wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.

Hosea  4:6 ''Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya MUNGU wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.''

Binadamu wengi sana wanadhani hadi Malaika awahubiri ndipo wataona umuhimu wa kumpokea BWANA YESU na kujiponya raho zao na Nafsi zao.
Mmasai alipoambiwa ajitetee hakika alijitetea lakini  wanadamu wengi leo wakiambiwa wajitetee kwa kuzikimbia dhambi na kumkimbilia YESU watasena '' subiri kwanza, au watasema ''labda mwakani''
Hawana uhakika wa kuishi hiyo mwakani lakini hiyo mwakani ndio wameipangia mipango mingi kuliko leo yao.
=MUNGU amewasogezea karibu kabisa wanadamu uzima wa milele lakini kwa kukosa kwao maarifa wameukataa Wokovu wa MUNGU.
=MUNGU amewasogezea uzima wa milele karibu yao sana tena amewasogezea kwenye vinywa vyao kabisa lakini bado wanadamu kwa kukosa kwao maarifa ya MUNGU wameukataa Wokovu wa BWANA YESU ambao ni wa thamani kwao kuliko yote wanayoyahitaji maishani mwao.
=Wengine kwa kukosa maarifa wameshika madhehebu yao huku YESU  yuko pembeni wamemwacha.
=Wengine kwa kukosa maarifa wanafuata dini za wazazi wao japokuwa ni dini za shetani kabisa.

Neno la MUNGU katika Warumi 10:13 Linasema ''kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la BWANA ataokoka.''  Lakini kwa kukosa maarifa wanadamu wengi wanaukataa Wokovu huo wa BWANA YESU.
Kwa kukosa maarifa wanadamu wengi wanamkataa BWANA YESU mwenye uzima wao wa milele.
-Ukombozi utatokana na wewe mwenyewe.
-Ukombozi utapatikana  kwa maamuzi yako Mwenyewe.
-Ukombozi wako uko  katika KRISTO YESU pekee lakini wewe utaumiliki ukombozi huo kwa kuufuata huku ukidharau ya dunia na kuacha uovu wote.
Ndugu, Usikubali kuishi na mapepo maishani mwako huku ukijua kabisa kwamba mapepo ni mashetani ambayo yametumwa kwako ili kuhakikisha hufiki mbinguni. 
Kataa leo kutumiwa na shetani kama chombo chake cha kumburudisha.
 Watu wengi wamefungwa kwenye mambo mengi huku wakijua kabisa kuwa MUNGU anaweza kufanya muujiza katika hayo lakini kwa kukosa maarifa kwao hawamwendei MUNGU kwa maombi hata wakapokea baraka zao hizo.
Japokuwa MUNGU ''Amewapelekea watu wake ukombozi, Ameamuru agano lake liwe la milele, Jina lake ni takatifu la kuogopwa.-Zaburi 111:9'' Lakini wanadamu wengi wameukataa ukombozi wa MUNGU ambao pekee uko katika YESU KRISTO.
Kwa kukosa maarifa wanadamu wako tayari kumchagua shetani na kumkataa YESU.
Kwa kukosa maarifa wanadamu wengi wako tayari kumwabudu shetani hata kama wanajua kabisa kwamba anayestahili kuabudiwa ni MUNGU pekee, tena MUNGU huwa haabudiwi kwa mazoea  bali huabudiwa katika ROHO  na kweli.
Yohana 4:24 ''MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. '' 

Wanadamu wengi mimi naona huwa wanapenda zaidi ukumbusho na sio ukombozi wa roho zao.
Wanadamu wako tayari wakifa wakumbukwe kwamba walikuwa walevi wenye uwezo wa kumaliza kreti ya bia moja kwa siku.
Kuna ambao wako tayari wakumbukwe kwamba walikuwa viwembe na walitembea na mabinti/vijana wa mitaa mitatu yote.
Ni kumbukumbu mbaya na ni kumbukumbu ya waliokosa maarifa sahihi ya kiMUNGU.
Ni ukumbusho wataacha kwa sababu ya uovu wao uliopindukia lakini hiyo itawasaidia nini kwa habari ya uzima wa milele?
Bibi  mmoja kwenye Biblia jina lake Anna  alikuwa anaungojea ukombozi wa KRISTO na akauona na kumtukuza MUNGU.
Bibi huyu licha ya kuwa mjane kwa miaka 84 lakini aliendelea kuomba na kufunga maana ameichagua njia ya uzima.
Ukombozi ulipofika Biblia inasema kwamba Bibi
 ''Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru MUNGU, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.-Luka 2:38'' 

Je, wewe ndugu unayesoma ujumbe huu unataka kuacha historia gani duniani?
Je na wewe uko katika kundi la watakaoacha heshima bar huku wao wakielekea jehanamu?
Je unaacha heshima mtaani kwa kuwa ulikuwa mzinzi grade A.
Itakusaidia nini kupata  vitu vyote vya duniani kisha ukapata hasara ya milele.
Nakushauri leo okoka na anza kuishi maisha matatifu.
Uzima wa milele upo na jehanamu ipo pia lakini ashukuriwe MUNGU kwa kutuletea ukombozi wa roho zetu ambao uko katika KRISTO YESU pekee.
Ndugu ukombozi wako unapatikana kwa maamuzi yako mwenyewe leo ya kumpokea YESU KRISTO.
Yeye BWANA YESU anasema ''Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. -Mathayo 11:28''
Amua vyema leo itakusaidia.
 Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments