USIKUBALI KULA ZAKA BALI MTOLEE MUNGU WA MBINGUNI.

 
Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Nakukaribisha tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Fungu la kumi au zaka ni asimilia moja katika kumi ya kila mshahara wako, ni asilimia kumi katika kila asimilia mia moja ya faida ya biasahara yako.
Nimewahi kuulizwa maswali mengi sana kuhusu fungu la kumi, kupitia somo hili nitajibu maswali yote kuhusu fungu la kumi lakini muhimu zaidi kujua ni kwamba
''Ukila Fungu La Kumi(zaka) Tambua Kwamba Umekula Moto.''
 Ni Heri Upate Laki Moja Ukiwa Chini Ya Baraka Kuliko Kupata Milioni Moja Ukiambatana Na Laana Kwa Sababu Tu Ya Kuacha Kutoa Fungu La Kumi. 

Hagai 1:5-10 ''Basi sasa, BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.  Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka. BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema BWANA. Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha. Ni kwa sababu gani? Asema BWANA wa majeshi. Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake. Basi, kwa ajili yenu mbingu zimezuiliwa zisitoe umande, nayo nchi imezuiliwa isitoe matunda yake.''

Hili ni neno binafsi kwa ndugu anayejifunza somo hili.
Tangu Mwanzo kabisa wa uumbaji tunaona jinsi kutoa kulivyo muhimu sana.
Mapema kabisa kabla hata ya sheria za Musa kuwepo akina Kaini na Habili walikuwa watoaji japokuwa utoaji wao ulitofautiana.
Kama vile mwanadamu anavyopenda sana pesa na mali ndivyo hivyo hivyo MUNGU hupata kipimo kizuri zaidi cha kumfahamu mwanadamu anayempenda MUNGU kwa moyo wake wote, nguvu zake zote na akili zake zote.
Katika utoaji wetu wote tunatakiwa tufahamu kwamba MUNGU hataki mali zetu wala pesa zetu ila MUNGU kupitia pesa yetu na mali zetu huuona utii wetu ulio kamili.
Watu wengi hujinadi kwamba wana mtii MUNGU lakini MUNGU akitaka tu aone utii huo kupitia kuwataka wanadamu hao kutoa matoleo, MUNGU hauoni utii huo ambao wanadamu wanadai wanamtii.
 Hata makanisani kuna baadhi ya wachungaji hawafundishi masomo ya utoaji maana akifundisha tu wale watu ambao ni mbegu zilizopandwa katika mwamba na kwenye miiba (Luka 8:5-15) husema '' anataka hela za kusomeshea wanae''
Neno la MUNGU ni neno la MUNGU tu na hatuwezi kulibadili ili litutii sisi, ni heri kufundisha tu.
Kuna makanisa husambaratika baada ya ya mchungaji kuhubiri kuhusu utoaji.
 Kuna wachungaji wengine ili afundishe somo la utoaji inabidi amwite mchungaji mwingine ili ampe ujumbe huo afundishe.
Kanisa la leo wengi hawajui kwamba utoaji kwa mkristo ni jambo la lazima.
Kuna watu kabla hawajaokoka walikuwa wakitoa fungu la 40 kwa waganga wa kienyeji lakini wameokoka hao hao wamesahau kwamba walikuwa wanamtoleta mganga fungu la 40 na wakati huu neno la MUNGU likiwataka watoe fungu la 10 huanzisha maneno yasiyo na maana na machukizo.

Kumb 14:22 ''Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka.''

Kuna Dozi Nyingine Ni Chungu Sana Lakini Ukinywa Tu Unapona Haraka Sana. 
 Fungu La Kumi Ni Kama Dozi Chungu Sana Kwa Watu Wengi Lakini Ni Tiba Kuu Ya MUNGU Kukubariki.
-Ni Tiba Ya Kumfanya MUNGU Ajue Kwamba Unahitaji Baraka Zake.
-Ni Tiba Ya Kumfanya MUNGU Ailinde Biashara Yako Au Kazi Yako.
-Ni Tiba Ya MUNGU Kulinda Chanzo Cha Kipato Chako.
 Ukiiba Zaka Unaiba Baraka Zako Kutoka Kwa MUNGU, Ukiiba Zaka Unaingia Chini Ya Laana.

 Malaki 3:10-11 ''Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.
Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi.''.


Utoaji humfurahisha MUNGU maana hapo tunakuwa tunatii agizo lake.
ukitaka uufurahishe moyo wa MUNGU basi ishi maisha matakatifu na utoaji.
Katika kutoa zaka au sadaka naomba pia ujue kwamba '' Hatutoi  zaka kama kujipendekeza kwa MUNGU  ili atubariki, bali vyote ni vyake hata kama tunavimiliki sisi, lakini unyenyekevu wetu uko katika uaminifu wetu wa kumtolea MUNGU wetu.

Yohana 12:24 '' Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.'' 

Unamtolea MUNGU ni kama unatupa mbegu katika ardhi lakini mbegu hiyo huota na kukuletea mazao mengi.
Mojawapo ya mazao ambayo utayapata kutokana na utoaji wako wa sadaka na fungu la kumi ni;
      1.  Ulinzi wa MUNGU kwako na mali zako, maana MUNGU maeahidi kuilinda mali yako hivyo na wewe utalindwa maana haiwezekani kulinda mali huku mwenye mali akiwa halindwi.(Malaki 3:11,Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi. )

    2.  Utakuwa unaweka hazima mbinguni.
(Mathayo 6:20-21,bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi;kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako)

    3.  Sadaka yako itakuwa ukumbusho mbele za MUNGU.(Matendo 10:4,Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za MUNGU.)

    4.  Utakuwa unaonyesha utii kwa MUNGU.
(Warumi 2:8,na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu;)

    5.Utakuwa unaonyesha kwamba pesa yako inakutii na sio wewe kuitii pesa.
(1 Petro 2:13,Tiini kila kiamriwacho na watu, kwa ajili ya BWANA; ikiwa ni mfalme, kama mwenye cheo kikubwa;)

   6. Utakuwa unaonyesha kwamba wewe ni mwaminifu katika kidogo hivyo kwa kanuni ya Neno la MUNGU utakuwa mwaminifu pia katika kikubwa.
(Luka 16:10, Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia.)

7.  Utakuwa unaonyesha kwamba pesa yako unaitawala na sio pesa kukutawala.
(Warumi 6:12,Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake;)


Utoaji ni kanuni nzuri kwa Mkristo na kanisa kwa ujumla lakini wakati mwingine watumishi hukosea
Kuna madhaifu baadhi ya watumishi huyaonyesha kuhusu utoaji makanisani mwao.
Kuna makanisa wamewekewa kiwango cha mwisho cha chini cha utoaji, hiyo sio kibiblia.
Kuna watumishi wakipewa zaka na sadaka nyingi makanisani mwao wao ndio huongeza magari ya kifahari kutoka 1 na kufikia hata 10, hiyo sio nzuri na iko kimwili zaidi na hiyo haiitakii mema injili ya KRISTO ambayo inahubiriwa kila siku kwamba inatakiwa isonge mbele. Ni heri badala ya kuongeza magari ya kifahari, pesa hiyo ingeinunua viti na kuwapelekea makanisa ya vijijini, au ingenunua Biblia na kuwagawia wanafunzi mashuleni, au ingeunda timu hata 7 za watumishi vijana na kuwawezesha ili waipeleke injili kule BWANA atawapeleka.


Mtumishi Hakikisha Huduma Yako Haiendeshwi Kwa Sura Fulani Za Watu kwa sababu tu wao ni watoaji.
Kumbuka Kanisa La Kwanza La Mitume Lilianzia Ghorofani hivyo MUNGU ataliweka juu tu kanisa lako kama mkibaki katika kusudi lake, Tukiwategemea Watu Fulani Tu Kwenye Huduma Zetu MUNGU Atatuacha. 
Tumtegemee MUNGU Ili MUNGU Ainue Watu Kwa Ajili Ya Huduma Zetu Na Hapo Atatukuzwa MUNGU, Lakini Tukiwategemea Watu Basi Watatukuzwa Watu Hao.
Kumwamini MUNGU katika utoaji ni jambo la Muhimu sana.
 Ulimwengu Wa Roho Unaenda Kwa Matamshi, MUNGU Anaangalia Neno La Mtumishi Alilolitamka Ili Alidhibitishe. Kiwango Chako Cha Imani Ndio Kiwango Chako Cha Kupokea.
Kiwango chako cha imani katika utoaji wako ndio kiwango chako cha utii.
Zaburi 20:1-4 ''BWANA akujibu siku ya dhiki, Jina la MUNGU wa Yakobo likuinue. Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni. Azikumbuke SADAKA ZAKO ZOTE, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote.''

Ndugu, usipopenda kumtolea MUNGU wako aliyekuumba utamtolea nani?
Usipomtolea BWANA MUNGU ambaye wako ambaye yeye kwanza ndiye aliyeanza kutoa kwa kumtoa Mwanaye YESU KRISTO ili awe sadaka kwa ajili ya wewe kupata uzima, je kwanini usimtolee yeye.
Kuna jambo watu wengi huuliza sana kwamba je ni wapi pa kutoa fungu la kumi?
Jibu ni kwamba fungu la kumi unatoa mahali unapoabudu, mahali unapolishwa neno la MUNGU kila jumapili yaani kanisani kwako.
Kuna watu hutaka tu kutoa fungu la kumi kwa watumishi wengine au kwa yatima na wajane, jibu ni kwamba toa fungu la kumi kanisani na kisha andaa pesa au zawadi nzuri kwa ajili ya yatima na wajane na wahitaji na watumishi wengine ambao hukuombea na kukusaidia kiroho na wewe ukawiwa kutoa sadaka kwao, sio fungu la kumi bali toa nje na fungu la kumi. Wakati mwingine mtu anaweza akatoa fungu la kumi kanisani lakini kwa neema kabisa akatoa pesa nyingi zaidi kwa yatima na wahitaji, hiyo ni nzuri sana maana umetoa nje na fungu la kumi.

Kumb12:12-13 ''Nanyi mtafurahi mbele za BWANA, MUNGU wenu, ninyi, na wana wenu, na binti zenu, na watumishi wenu wanawaume na wanawake, na Mlawi aliyemo malangoni mwenu; kwa kuwa hana sehemu wala urithi kwenu. Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo;''


Ukipokea Kidogo Kutoka Kwa MUNGU Zaidi Ya Kile Ulichoomba Basi Tambua Kwamba Imani Yako Ni Ndogo Na Inaendana Ulichopokea.
Kama wewe sio mtoaji hakikisha unakuwa mtoaji kuanzia leo.

''Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.- 2 Wakorintho 9:6.''

 Ndugu yangu, panda kwa kumtolea MUNGU zaka na sadaka.
Panda kwa kuwapa watumishi wa MUNGU ili waipeleke mbele injili ya KRISTO maana hapo utakuwa umehubiri injili pamoja na wao.

 Ndugu panda neno la MUNGU kwa rafiki zako  
Wateule Hatuwezi Kusema Kwamba Tunajua Zaidi Ya Kile Biblia Imeandika.
Kuna watu wametumia mamilioni kwa waganga na bado hawakupona zaidi tu ya kudanganywa ili wawafanye zezeta wake zao/waume zao au ndugu zao kumbe shetani yuko kazini akicheza
timu zote mbili yaani akikuroga na wakati huo huo akijifanya dokta. ndugu zangu msaada kamili ni Kwa YESU tu.

Ni heri ukanunua hata Kinanda ili kusaidia tuipeleke mbele injili ya KRISTO.
 Ni heri ukanunua mic hata moja ili kutusaidia kuhubiri,
Ne heri ukanunua hata Gitaaa ili kutusaidia kuitenda kazi ya MUNGU. Apandacho Mtu Ndicho avunacho.
Nataka nitoe angalizo; Kuna baadhi ya watumishi ambao kwa sababu ya kunyimwa madhabahu wamezusha maneno mengi kwa wachungaji na sehemu kubwa ya kuwaaminisha watu ni kusema uongo juu ya Pesa ya kanisa.
Katika kila kanisa kuna timu ya uongozi na sio mchungaji pekee hivyo ni vizuri sana kila kitu kikawa wazi kwa viongozi ili kuondoa manung'uniko yasiyo na maana.
 Binafsi mimi Sitasahau Huruma Za BWANA YESU Maishani Mwangu. Alinishindia Hata Pale Ambapo Ufahamu Wangu Ulifika Mwisho.
 Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com


Comments