VIWANGO VINNE(4) VYA NENO LA MUNGU KWA MKRISTO.

Na Mtumishi Peter Mabula.
 BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la kutuvusha na kutushindia.
Ujumbe huu MUNGU ameuhifadhi ndani yangu kwa mwaka mzima sasa lakini leo amenipa kibali nikuletee.
Kuna viwango vinne vya Neno la MUNGU kwa Mwamini, mkristo aliyeokoka.
Kila Mkristo aliyeokoka yuko katika kiwango kimojawapo kati ya viwango hivi vinne ninavyokuletea.
Kupitia ujumbe huu naomba ujipime umefikia kiwango gani.
Lakini unapojifunza ujumbe huu naomba ujue pia kwamba uwezekano wa kupanda kutoka kiwango kimoja kwenda kingine upo na upo leo kwa ajili yako.

Hivyo baada ya ujumbe huu utatakiwa ukue kiroho na kufikia kiwango cha juu. 


Zaburi 12:6 ''Maneno ya BWANA ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba.''

Neno la MUNGU ni maneno safi na Neno ni jipya kila siku.
Unajua Neno la MUNGU kwa nini ni jipya kila siku?
Ni kwa sababu Neno kila siku ni kama Pesa mpya inayoanza kutumika.
Wakati Serikali inapotoa Noti mpya naamini kila mtu anatamani kuwa na noti mpya na sio zile za zamani. sasa Neno kila siku ni jipya na Biblia imesema hapo juu kwamba Neno la MUNGU ni kama pesa mpya iliyojaribiwa kalibuni tu tena Pesa hiyo imesafishwa mara saba ndipo ikaanza kutumika, ndivyo neno la MUNGU lilivyo siku zote.
=Ukiona umeanza kulichoka Neno la MUNGU tambua kwamba wewe umeanza pia kuichoka mbingu.
=Kupitia Neno la MUNGU tunamjua MUNGU na mpango wake kwetu.
=Kupitia Neno la MUNGU kila mtu anajua ameandaliwa kitu gani baada ya kuondoka duniani.

VIWANGO VINNE VYA NENO LA MUNGU KWA MWAMINI NI;

   1. Kiwango cha maziwa.
Kiwango cha maziwa ni kiwango cha neno la MUNGU ambaco mtu anakipokea baada tu ya kumpokea YESU kama BWANA na MWOKOZI wake.

1 Petro 2:2 ''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;''

Mama anapozaa mtoto humwesha maziwa tu kwa miezi 6 maana mtoto huyo kwa muda huo anakuwa hawezi kukipokea chakula kingine. 
 Kiroho mtu anapookoka maana yake amezaliwa upya kiroho.
amezaliwa na MUNGU kiroho na anaanza kuitwa mtoto wa MUNGU(Yohana 1:12-13).
Mtu anapozaliwa kiroho anakuwa ni kama mtoto mchanga kiroho maana mambo mengi anakuwa hajayajua bado. Huyu anahitaji kunywa maziwa maana chakula bado anakuwa hakiwezi.
Lakini kuwa kanisani miaka 5 au 20 au 30 haiwezi kukufanya kuvuka kiwango cha maziwa kama hukui kiroho.

=Kukua kiroho huwa ni juhudi binafsi za Mwamini.

Mtu ambaye yuko katika kiwango cha maziwa  anatakiwa awe na wasimamizi wazuri wa kumsaidia na kumwendeleza  kukua kiroho.
Maziwa ni matamu na rahisi kunywa.
Ndio maana kuna baadhi ya makanisa wana madarasa ya kuukulia wokovu ambapo madarasa hayo yanakuwa na walimu wanaowafundisha waamini wapya mafundisho ya kuukulia wokovu.
Mtu wa kiwango cha maziwa chakula kigumu anakuwa bado hakiwezi.

=Kiwango hiki huambatana na imani haba kwa baadhi ya watu.

Mfano;
Kama mchungaji atatangaza maombi ya siku 21 ya kufunga mara zote watakaolalamika au hata kuhama kanisa  ni wale wa kiwango cha maziwa,  hata kama watu hao wana miaka 12 kwenye wokovu.
Mtu wa kiwango cha maziwa ni rahisi shetani kumdanganya maana huyu ndugu anakuwa hajui mambo mengi ya MUNGU.
Mwenye kiwango cha maziwa ni mtoto kiroho au ni mchanga kiroho.
 Mtu kama huyo huwezi kumfundisha mambo magumu maana yanaweza kumkimbiza kanisani kabisa japokuwa hayo magumu ndio muhimu zaidi kwake.
Kama wachungaji wangekuwa wanatangaza kila wiki kile watakachofundisha wiki inayofuata hakika wenye kiwango cha maziwa wangepata taabu sana hata kukimbia kanisa. 
Mfano mchungaji atangae kwamba ''Wiki ijayo nafundisha juu ya fungu la kumi maana ni laana kutokutoa fungu la kumi'' 
Wenye kiwango cha maziwa hata kama wako katika kaisna kwa miaka 2 itawasumbua sana.

Mfano Mchungaji aseme ''Wiki ijayo nitafundisha juu ya kusimama imara kwenye dhoruba kama Stephano, maana Stephano alipigwa mawe hadi kufa lakini alivumilia'

Ujumbe kama huo kwa muumini ambaye yuko kiwango cha maziwa utampa maswali mengi. mfano atawaza kumbe kuna kuuawa, kumbe kuna magumu hivi katika imani hii. hayo atayawaza kwa sababu yeye ni mchanga kiroho na anatakiwa aimalishwe kwanza kwa mafundisho ya kuukulia Wokovu.

=Juhudi ya Mwamini katika maombi, utakatifu, kumtii MUNGU  na kujifunza Neno Kanisani ndivyo vitamuondoa haraka kutoka kwenye kiwango cha maziwa hata akahitaji chakula kingine cha kumletea nguvu zaidi mwilini mwake.

 Kuna watu hata miezi 3 tu inamtosha kabisa kuhama kutoka kiwango cha maziwa na kuingia kiwango kingine maana kwa muda huo atakuwa kila ibada anahudhuria na kujifunza neno la MUNGU na kulishika na kulitii Neno hilo, atakuwa mwanamaombi na atakuwa akimtumikia MUNGU.

Kuna Wakristo kwa sababu ya kupuuzia kile wanachofundishwa kanisani wamebaki kwenye kiwango cha maziwa tu miaka yote.
Ni watoto wachanga kiroho hata yakija magumu kidogo tu kanisani watakimbia maana ni wachanga kiroho.

Siku moja kuna ndugu mmoja kutoka dini nyingine nje na Ukristo. Yule ndugu alipookoka tu aliniuliza nimwambie YESU ni nani?
Kwa sababu ameokoka muda huo huo nilimwambia kwamba Biblia inasema katika Yohana 3:31 kwamba aliyetoka mbinguni yaani BWANA YESU yu juu ya yote, hivyo YESU anaokoa na kuponya.
Ndugu huyu alifurahi na kusema hakika imani yenu Wakristo ni ya kweli. Baada ya kuukulia wokovu na kulijua Neno vizuri na kukionja kipawa cha ROHO, ndugu huyu haikumsumbua kujua kwamba YESU ni Mwana wa MUNGU, Haikumsumbua kujua kwamba ina maana gani kusemwa kwamba YESU ni Mwana wa MUNGU, Haikumsumbua kusemwa kwamba YESU KRISTO ni MUNGU mkuu(Tito 2:13). 
Ndugu huyo hata sasa ni mtumishi mzuri wa MUNGU lakini kama ningempa chakula kigumu siku ya kwanza tangu aachane na dini yake na kuokoka hakika angerudi tu kwenye dini na kukosa uzima wa BWANA YESU.
Watumishi wa MUNGU wanatakiwa kuelewa kiwango cha neno cha wanaowapelekea neno.

   2. Kiwango cha Nyama au kiwango cha Chakula cha kawaida.

Yohana 6:27 '' Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na BABA, yaani, MUNGU.'' 

Neno la MUNGU ni chakula cha uzima  ila kuna viwango vya chakula hiki kwa mwamini.
 
Wenye kiwango hili ni wale ambao wamekuwa kidogo kiroho lakini shetani ana uwezo wa kuwayumbisha. Mtu wa kiwango hiki anaweza kuwa anajua mambo mengi kidogo ya ki MUNGU bila kuyatendea kazi. 

Waamini wengi sana wako katika kiwango cha nyama.

Mtu kama huyu anaweza akafanya baadhi ya  vitu kanisani hata baadhi ya huduma lakini akiambiwa 
mfano;wiki ijayo tutakuwa na ibada ya changizo kwa ajili ya kujenga kanisa anaweza asije kanisani siku hiyo na kwenda kuabudu kwingine akidhani anafanya jambo jema kumbe sio.
Mtu kama huyo akiambiwa ijumaa ijayo vijana wote wa kanisani tutatekwenda kwenye mkesha kigamboni anaweza hata akatoa udhuru wa uongo kwa sababu tu hataki kwenda.

=Kiwango  hiki huambatana na mazoelea ya ibada.

Mtu wa kundi hili hufanya vitu kwa kujisikia na kusingizia hadi apate amani moyoni ndipo atende jambo hilo la kiMUNGU kumbe ni upungufu wake wa kiwango cha neno ndani yake.

Mtu wa kiwango hiki anaweza hata akachagua vitu vya kushika huku vingine ambavyo ni muhimu akiviaacha.
Mtu kama huyo anakuwa anajua neno kwa sehemu lakini hataki neno limuongoze wala kumuendeza katika njia zake.

Kuna watu wanajua kabisa kwamba viburi ni dhambi lakini wanawafanyia kiburi hata baba zao wa kiroho.
Ingawa anajua kabisa kwamba fungu la kumi ni lazima lakini mtu wa kundi hili anaweza akatoa mwezi huu kisha mwezi ujao akapotezea, ni mbaya na anatakiwa atamani kukua zaidi maana uwezekano wa kuingia kiwango bora zaidi upo wazi kwa kila mwamini.

   3. Kiwango cha nyama ngumu au chakula kigumu.
Kiwango hiki ni kiwango cha watu ambao wameshakua kiroho lakini kuna vitu vichache wanavihitaji ili kukamilika ipasavyo.
Mtu wa kundi hili ni ni yule ambaye ameshakuwa kiufahamu  wa Neno la MUNGU na ana uelewa wa kutosha.
Mtu huyu anakuwa anafahamu haki zake zote  lakini hajaanza kushirikiana na haki zake hizo.

Waebrani 5:12-14 '' Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya MUNGU; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.''

Mtu wa kundi hili anaweza kuwa anajua mambo mengi sana ya kiMUNGU. 
Anaweza akakariri kichwani hata mistari 50 ya Neno la MUNGU lakini hajui jinsi ya kushirikiana na maandiko hayo ili apokee hitaji lake.
Anaweza akajua na kukariri maandiko mengi lakini hajui kutumia Neno hilo  ili kufunga na kuharibu nguvu za giza.

Kiwango hiki ni kizuri kiasi lakini mara nyingi watu wa kiwango hiki hawajui maarifa sahihi na jinsi ya kufanya ili kushirikiana na neno la MUNGU hata kuingia katika baraka yao.

=Kiwango hiki wakati mwingine huambatana na kiburi cha uzima na kujiona bora kuliko wengine.

     4. Kiwango cha Asali.
Kiwango cha mwisho cha Neno la MUNGU kwa mwamini kinaitwa kiwango cha asali.
Ni kiwango adimu sana na inawezekana kabisa ni wachache walio nacho kiwango hiki.
Kila Mkristo anatakiwa kukifikia kiwango hiki.

=Kiwango hiki huambatana na imani timilifu na utakatifu halisi. 

Wa kwanza kutembea katika kiwango hiki ni BWANA YESU mwenyewe alipokuwa duniani.

Isaya 7:14-15 ''  Kwa hiyo BWANA mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli. Siagi na asali atakula, wakati ajuapo kuyakataa mabaya na kuyachagua mema. ''

Ukiwa katika viwango vitatu vya kwanza kuna vitu vya kiMUNGU unaweza kuvikosa maana sio saizi yako.
Kiwango hiko cha asali ni kiwango ambacho mhusika anaweza kupokea vitu vikubwa na anaweza kuvumilia katika yote kwa ajili ya BWANA YESU.

Ufunuo 10:9 ''Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.'' 

Katika maono mtume Yohana anakifikia kiwango cha asali na ndio maana alipewa kujua hata mambo ya siku za mwisho hata akatuandikia sisi.

=Kwa kadri unavyokula Neno la MUNGU kwa kujifunza ndivyo unaweza kukua hata kufikia kiwango cha asali.

Mtu wa kiwango hiki hata akiambiwa utakufa wiki hii  maana kuna maono yameonekana hivyo yeye ataomba na kumuuliza ROHO MTAKATIFU na ROHO atasema jambo hilo sio kweli  na ndugu huyu atasonga mbele maana yuko katika kiwango kikubwa kiimani na kiufahamu wa Neno la MUNGU.

Mfano mtu wa kiwango cha maziwa akiambiwa atakufa wiki hii kwa maono  yeye atakimbilia msaada kwa mganga wa kienyeji.
akiambiwa mtu wa kiwango cha nyama anaweza hata kukimbilia polisi kushitaki.

Ni muhimu kupanda na sio kushuka kiviwango.

Ezekieli 3:1-3 '' Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli. Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo. Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali. '' 

Kwa njia ya maono Ezekieli naye anakifikia kiwango hiki.
Asali hakika ni tamu na Neno la MUNGU kwa watu ambao wako kiwango cha asali ni tamu sana kwao jakupua kwa walio viwango vya chini wataona Neno hilo kama chungu na gumu.

=Mtu akiwa katika kiwango hiki anaweza akapewa  vitu vingi na MUNGU vya kihuduma na maono pia.

Mithali 24:13-14 ''Mwanangu, ule asali, kwa maana ni njema, Na sega la asali lililo tamu ulionjapo. Basi utaijua hekima kuwa tamu kwa nafsi yako; Ikiwa umekwisha kuiona; Ndipo itakapofuata thawabu; Wala tumaini lako halitabatilika.''

Natamani niendelee lakini kwa leo naishia hapo.

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

 

Comments