WATU WENGINE HUONA NINI KWAKO?



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Kwa upendo mwingi sana nakukaribisha tujifunze Neno hai la MUNGU. Nakuomba usome hadi mwisho wa somo.
Leo nakuzungumzia wewe na sio mtu mwingine.
Maisha ya mtu yeyote ni barua inayosomwa na watu wanaomzunguka.

Maisha ya Mkristo Aliyeokoka ni barua iliyoandikwa  kwa wino mwingi sana na kwa maandishi makubwa sana kiasi kwamba barua hiyo inasomeka kwa urahisi sana, na husomwa hata kama iko mbali.

Sio watu wote ni barua njema.
Sio watu wote wanaishi maisha sahihi ya wokovu.
Ukiishi maisha bandia ya wokovu utaonekana tu, na ukiishi maisha safi ya wokovu utaonekana tu.

3 Yohana 1:3-6 ''Maana nalifurahi mno walipokuja ndugu na kuishuhudia kweli yako, kama uendavyo katika kweli. Sina furaha iliyo kuu kuliko hii, kusikia ya kwamba watoto wangu wanakwenda katika kweli. Mpenzi, kazi ile ni ya uaminifu uwatendeayo hao ndugu na hao wageni nao,  waliokushuhudia upendo wako mbele ya kanisa; utafanya vizuri ukiwasafirisha kama ipasavyo kwa MUNGU.''

Huu ni ushuhuda wa mtu aliyeishi maisha matakatifu hata kuwa ushuhuda mzuri mbele ya kanisa na mbele ya jamii inayomzunguka.
Katika maandiko hayo; anayezungumzwa ni Gayo, mtu ambaye Mtume Yohana alikuwa amemhubiria Neno la MUNGU.
Gayo baada ya kuhubiriwa akaokoka na kuanza kuishi maisha matakatifu. Baada ya Mtume Yohana kumaliza kumhubiri Gayo aliondoka eneo hilo na kuendelea na kuhubiri katika maeneo mengine ambayo MUNGU alimpeleka.

Baada ya muda mwingi kupita Mtume Yohana alikuwa mbali akiendelea na huduma kama kawaida ndipo alipoupata ushuhuda mzuri wa Gayo.
Gayo wa leo ni wewe na mimi; Tulihubiriwa habari njema za ufalme wa MUNGU na tukaokoka, hivyo ni lazima sana kuishi maisha mataktifu siku zote.

Gayo ni mfano halisi wa Wakristo wote wanavyotakiwa kuwa katika maisha yao ya kila siku.
Wakristo wote wanatakiwa kuishi maisha matakatifu siku zote.

MUNGU hataki tuishi maisha bandia, bali anataka tuishi maisha matakatifu daima.
Je, Watu wengine huona nini kwako?

Je wanauona utakatifu halisi?

 Je wanauona utu wema?

Je wanaiona tabia njema?

Je, Wanaona thamani halisi ya Wokovu wako ambao ni wa thamani sana?

Kuna watu hujiita wameokoka lakini ukiwatazama kwa muda mchache tu utagundua kabisa kwamba vinvywa vyao havijawahi kuokoka hata dakika moja, maana ni matusi kila siku na uongo daima.
Je, Bwana YESU anaiona tofauti halisi kati yako wewe uliyempokea na watu wa mataifa?

Bwana YESU anasema juu yetu tuliompokea 
''Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.   -Mathayo 5:20''

Haki yetu tuliookoka ni lazima iizidi haki ya mafalisayo. 
-Haki ya mafalisayo inaweza kuwaruhusu kuchukua mawe na kumpiga mtenda dhambi mmoja, japokuwa katika uhalisia, wao ndio wenye dhambi zaidi ya huyo wanayetaka kumuua kwa kumpiga mawe.

Je, sisi tuwe kama mafalisayo?
Hapana, haki yetu lazima iizidi haki ya mafalisayo ndipo tutaingia uzima wa milele.

-Mafalisayo wanaweza wakasema ''Kunywa pombe lakini usilewe''
Lakini haki yetu sisi waliookoka inasema Tusiguse kitu kilicho kichafu, 2 Kor 6:17-18 ''Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa BABA kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,''

=Kama kugusa tu kitu kichafu tunakatazwa je kunywa si ni zaidi?

Kitu kichafu ambacho Biblia inakataza ni kile ambacho kinaweza kumnajisi mtu au kuharibu kiroho chake au kumfanya awe mpagani hata kama kanisani anaenda.
Uasherati ni kitu kichafu, pombe ni kitu kichafu, dhambi ni kitu kichafu na uovu na kila namna ni kitu kichafu hivyo hatutakiwi kugusa kabisa, na hiyo ndiyo haki yetu ambayo iko tofauti na haki ya mafalisayo.
Haki yetu ni lazima iizidi haki ya mafalisayo.

Mfalisayo wanaweza wakashika sabato tu lakini hao hao ndio wanaompiga Stefano kwa mawe ambaye yeye Stefano ana haki zaidi kuliko wao, Biblia inayathibitisha hayo katika Kitabu cha matendo ya mitume kwamba waandishi na mafalisayo ndio waliofanya njama za kumuua Stephano.

Haki yao inawatuma  Kumuua Stephano lakini haki ya Stefano haimruhusu kuua wala kuchukia watu wala kulipiza kisasi.
Haki ya Stefano ndio haki wa wateule wa Bwana YESU. 
Je, watu wengine wanaona nini kwako?

Je, Wanaona utu wema au uuaji?

Je, wanaona kumcha MUNGU au tu wanaona ukiwashauri watoe mimba?

Kuna watu hawanywi pombe lakini huiuza na kujiona wao ni watakatifu.
Haki yao inawaruhusu kuuza pombe lakini hiyo ni haki feki na sio haki ya waenda mbinguni.

Kuna watu huona kumiliki bar ni jambo dogo lakini ndugu yangu hiyo bar kwa sababu ya pombe unazouza imegeuka kuwa kiwanda cha kuzalisha dhambi. Kufanya hivyo unamsaidia shetani kuwaharibu wanadamu. Wanaolewa pombe kupitia bar yako na wanaochuna mabuzi kupitia hapo wote hawampendezi MUNGU.

Kuna watu hawaendi kwa waganga lakini huwashauri watu wengine kwenda kwa waganga na wao kujiona ni watakatifu kumbe hiyo ni dhambi.
''Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.-Mithali 28:13''

Je watu wanaona nini kwako?
Je, wanaona dhambi au utakatifu?
Matendo mema ya Ruthu yalimpa kibali cha baraka ya ndoa?

 Ruthu 2:8-13 ''Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. Macho yako na yaelekee konde walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikuguse? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikilia watu usiowajua tangu hapo. BWANAakujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, MUNGU wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake. Ndipo aliposema, bwana wangu, na nipate kibali machoni pako; kwa sababu wewe umeniburudisha moyo, na kumwambia mema mjakazi wako, ingawa mimi si kama mmojawapo wa wajakazi wako.'' 

Baada ya matendo mema ya Ruthu kuwa ushuhuda mzuri mbele ya jamii alibarikiwa kupata mme mwema na kuwa miongoni mwa wanawake mashujaa katika Taifa la Israeli  japokuwa yeye hakuwa mwisraeli ila aliolewa tu na Mwisraeili.

Ruthu 4:13-15 ''Basi Boazi akamtwaa Ruthuu, naye akawa mke wake; naye akaingia kwake, na BWANA akamjalia kuchukua mimba, naye akazaa mtoto wa kiume. Nao wale wanawake wakamwambia Naomi, Na ahimidiwe BWANA, asiyekuacha leo hali huna wa jamaa aliye karibu; jina lake huyu na liwe kuu katika Israeli. Naye atakurejezea uhai wako, na kukuangalia katika uzee wako; kwa maana mkweo, ambaye akupenda, naye anakufaa kuliko watoto saba, ndiye aliyemzaa.''

Kwa sababu ya matendo mema ya Ruthu, alionekana anafaa kuliko watoto saba.
Watoto saba ni watu saba, sasa kama unafanya matendo mema harafu watu wanakufananisha thamani yako na watu saba hakika wewe ni mbarikiwa.
Huyu Alikuwa ni binti tu ambaye mume wake alifariki mwanzoni kabisa mwa ndoa yao, lakini aliendelea kutenda mema na kujiheshimu hadi kwa kupitia matendo mema yake akaja kupata mume, na akaja kuwa mama wa wafalme wakuu kabisa katika taifa.

Je, Wewe binti unayetaka kuolewa, watu wanaona nini kwako?

Je, wewe kijana unayetaka mchumba, watu wanaona nini kwako?

Kungekuwa na ndoa za mkataba basi kuna watu wangesema '' Ngoja nimuoe huyu binti kwa muda tu maana hafanani kabisa kuwa mwenzi wa maisha kwa sababu ya matendo yake''
Lakini haiwezekani hivyo kwa watoto wa MUNGU, hivyo unaweza kabisa ukakaa muda mrefu bila kupata mchumba kwa sababu tu ya mfumo mbaya wa maisha yako.
Watu wanatakiwa waone kwako maisha halisi matakatiifu ya Wokovu na sio kuona umbea tu na uropokaji usio na maana.

 ''Lakini msingi wa MUNGU ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, BWANA awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la BWANA na auache uovu.-2 Timotheo 2:19''

 -Ukiendelea kulitaja jina la Bwana YESU huku ukiendelea na uovu wako, wewe hutakuwa mwaminifu mbele za MUNGU na mbele za wanadamu. Huko ni kujidanganya mwenyewe na dhambi zako.

BWANA anataka ayaone maisha matakatifu kwako.
Watu wanatakiwa waone matendo mema kwako na utakatifu halisi.

Je watu huona nini kwako?

Kama watu wengine wanaona maisha yako matakatifu, na wewe mwenyewe unashuhudiwa ndani yako kwamba unatembea katika haki ya KRISTO siku zote, mimi nakushauri endelea hivyo hivyo ukimtii MUNGU na Neno lake(Biblia)
Kama watu wanaona kwako mabaya basi acha kuyatenda mabaya hayo na ishi maisha mema kuanzia sasa ukiwa umeokoka.
1 Petro 2:12 '' Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze MUNGU siku ya kujiliwa.''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com

Comments