YESU ALIKUWA NA LENGO LIPI KUMTEMBELEA ZAKAYO? (LUKA 19:1-10)

 
Na Apostle Mtalemwa Dionis

 (LUKA 19:1-10)
Zakayo alikuwa afisa mtoza ushuru kazi ambayo pia alikuwa akiifanya Mtume Mathayo kabla ya kuitwa na Yesu. Kazi hii kwa Tanzania ni sawa na ile kazi ya afisa wa TRA yaani TANZANIA REVENUE AUTHORITY.
Kazi hii ilimfanya Zakayo awe tajiri sana kama maandiko yasemavyo
"Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye alikuwa ni tajiri " (LUKA 19:2). Lakini utajiri huu aliupata kwa dhuluma na wizi kama tutakavyoona huko mbeleni. Kwa sababu hiyo basi, Yesu aliamua kumtembelea Zakayo kwa Lengo kuu moja la kumpelekea wokovu ili aachane na dhuluma na wizi aliokuwa akiwafanyia watu katika jamii yake.

Zakayo hakujivunia fahari ya kuona Yesu amemtembelea katika mji wake wala hakuona fahari kwakuwa Yesu alikula nyumbani kwake, vilevile hakuona fahari ya kuandika historia kwamba ameketi na Yesu meza moja lakini Zakayo alitumia mwanya huo kutubu maovu yake na pia alitumia mwanya huo kuwarudishia watu aliowaibia Mali na stahiki zao.
Imeandikwa;
"Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana,nusu ya Mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne." (LUKA 19:8)

Yesu muda wote alipokuwa katika mji ule akila na kunywa, Zakayo hakuona wokovu ukishuka ndani yake mpaka pale Zakayo alipotubu na kurudisha haki za raia alizozitwaa kwa hila, baada ya kufanya hayo ya muhimu ndipo Yesu aliposema "....Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwasababu huyu nae ni mwana wa Ibrahimu. Kwakuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea" (LUKA 19:9-10).
*ZINGATIA HAYA:
(a) Kama Zakayo asingetubu na kurudisha Mali na haki za wanajamii aliowadhulumu basi angebaki na faraja ya kutembelewa na Yesu na kuandika historia tu bila baraka halisi za Mungu.

(b) Kama Yesu angezubaishwa na karamu (sherehe) kubwa aliyoandaliwa na Zakayo basi asingefikisha lengo la wokovu na hivyo angebariki dhuluma na wizi wa Zakayo na kumfanya Zakayo azidi kuwaibia watu maradufu kwa kuwa hakukemewa juu ya uovu wake.
*Yesu anapokutembelea tumia mwanya huo kujipatanisha nae na si kufurahia uwepo wake bila mabadiliko.
*Mtumishi wa Mungu, Mungu anapokutuma kwa Zakayo agenda kuu iwe ni kumfanya atubu na awarejeshee haki wale aliowadhulumu na si vinginevyo, ukifanya hivyo utumwa wako unakuwa umefanikiwa.

Baraka za Yesu ziwe nasi sote, sasa na hata milele. Amina.

Comments