DHAMBI NA KUMBUKUMBU YA DHAMBI

Na Frank P Sethi

"Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu, asema Mungu wenu. Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa; kwa kuwa amepokea kwa mkono wa BWANA adhabu maradufu kwa dhambi zake zote" (Isaya 4:1,2).

Dhambi ni kitendo cha kukiuka au kuasi maagizo fulani mtu aliyopewa (na Mungu) au kutenda jambo pasipo imani.
Angalia hapa, "Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi" (1 Yohana 3:4) na "Lakini aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi" (Warumi 14:23).
Tafsiri hii ya dhambi inaweeza kuwa finyu bado, na sijawahi kukutana na tafsiri moja ya dhambi, ndio maana ikifika mahali pa kuhukumu dhambi inabaki kuwa makini sana. Mambo mengi sana tunayoyaita dhambi au ambayo tumeyahalalisha au kuyaona kuwa ya kawaida, yanaweza yakawa na mtazamo tofauti mbele za BWANA. Hukumu sio kazi yetu, ole wake ahukumuye wenzake.
Nikalitazama jambo hili na kuona mambo haya, dhambi inachukiza, naam, inatia hasira na inakera au hata kuleta kinyaa au mara nyingine kutia huruma au kuleta simanzi. Usisahau, ipo Damu ya Yesu ambayo haina mipaka ya matumizi, KILA aliyeomba MSAMAHA husamehewa na KUSAFISHWA na kuwa safi kabisa (Isaya 1:18,19). Sasa tazama, kwa Mungu huyu mtu aliyetubu huwa MWEUPE kama theluji, ila kwa wanadamu kuna KUMBUKUMBU la dhambi! 

Hakuna kitu kizuri kama kumtia moyo mtu aliyeanguka dhambini na kumwambia "dhambi zako zimesamehewa". Nikitizama maandiko naona BWANA akimwachilia mwanamke mzinzi ambaye kwa sheria za Kiyahudi alipaswa kupigwa mawe hadi kufa, Akasema, "asiye na dhambi awe wa kwanza kurusha jiwe." Hakuna aliyerusha! (Yohana 8:1-11). Kumbe, wale warushau MAWE kwa wenzao nao wana dhambi?! Ndio, "kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu" (Warumi 3:23).
Jambo la kujifunza, dhambi tuonazo maishani mwetu ni nyingi kuliko Mungu aonavyo kwa maana hata ile TULIYOITUBIA bado hurudi mawazoni na kuleta HATIA ya dhambi! Angalia, jifunze kujisamehe mwenyewe kama Mungu anavyokusamehe. Kama Mungu anakusamehe na KUSAHAU, nawe jifunze kutubu na KUFUTA kabisa hatia za dhambi zilizotubiwa. Jitie moyo hata kama hakuna akutiaye moyo, jiambie mwenyewe, "nimesamehewa, mimi ni kiumbe kipya".

Sasa angalia jambo hili, Bwana Yesu hakuja kusamehe tu, ila na kufuta HATI ya mashitaka! Hati ya mashitaka ni mchanganuo wa DHAMBI na UBAYA wake na inaelekeza HUKUMU kwa hizo dhambi. Ibisili ni MSHITAKI, na mzoefu wa kazi yake, bila shaka anajua KUELEZEA dhambi zako hadi ukijitazama unajiona HUFAI kabisa mbele za BABA! Usikubali, msamaha ni BURE kama UKITAKA. 

Huu ndio ujasiri tulionao, msamaha ni BURE! Kwa maana imeandikwa, "wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu" (Warumi 3:24-26)
Frank P. Seth

Comments