JE! JINA LAKO NI SAULI AU PAULO?

Na Frank P. Seth.

"Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua. Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu; nitakufunga mshipi ijapokuwa hukunijua" (Isaya 45:4,5)
Liko fumbo juu ya nchi, nalo ni JINA lako la SASA na la BAADAE. Je! wewe ni SAULI au PAULO? Yamkini unajua jina lako la sasa, Je! Unajua jina lako la MWISHO?
Jina LINACHAGULIWA na mhusika kwa MATENDO yake mwenyewe. Ni kweli mtu hupewa jina, ila SIFA ya mtu ndio jina lake HALISI kuliko alivyoitwa. Maana jina linaleta picha ya mtu kulingana na TABIA (SURA au MWONEKANO au TABIA) ya mtu aliyetajwa.
Nitarudia tena, jina la mtu hujenga picha fulani (nzuri au mbaya) mara litajwapo. Kwa hiyo ukionacho JINA fulani likitajwa ndilo jina HALISI la mhusika. Ndio maana tunafundishwa, "ni heri KUCHAGUA jina jema kuliko mali nyingi..." (Mithali 22:1) maana yake, JINA lako sio shida, ila watu wanaona PICHA gani jina lako likitajwa? Na, kumbe! Unawaweza KUCHAGUA jina lako mwenyewe? Ndipo utajua tofauti ya jina SAULI na PAULO, japo mtu ni yule yule.
Ndipo ukimtazama SAULI, japo ni mtu yule yule, jina lake likitajwa, watu wanaona muuaji, mtesi wa kanisa, mtu wa hatari, nk. Punde, alipoitwa PAULO, japo ni mtu yule yule, sasa akitajwa watu wanaona mtume, tena hirimu wa mitume wengine, mhubiri wa Injili ya Kristo, kiongozi na mwalimu wa njia za haki, nk., ambaye hata sasa wengi tunajifunza miguuni pake! Je! Si yule yule ila majina tofauti (kutokana na alichoamini na kutenda)?
Sasa angalia jambo hili, Wakati Anania anamwona SAULI, Bwana anamwona PAULO! "Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana. Bwana akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba; naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena. Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako. Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu" (Matendo ya Mitume 9:10-16). Matendo/Habari za Sauli zilitengeneza jina lake kuwa baya...ila Bwana anona "chombo kiteule.."
Kumbuka siku zote, wewe UMEITWA (kwa jina lako la MWISHO) tangu hujatunga mimba tumboni mwa mama yako. Haijalishi sasahivi unaitwa nani. Umeumbiwa KUSUDI la Mungu maishani mwako (sawa na jina lako la mwisho). Jina lako la sasa sio jambo la kutizama sana, liwe baya au zuri, Je! Unajua jina lako la MWISHO?
Angalia tena, wakati mitume wamejifungia kwa hofu ya kuuwawa na SAULI (Mdo. 8), maana Stefano ameshauawa tayari wakiona, sasa katika kuomba kwao, yamkini ili Sauli AFE, ndipo Bwana anajibu maombi yao kwa KUGEUZA jina Sauli kuwa PAULO, kitu ambacho mitume hawakutarajia sana (Mdo. 9:10-16).
Tunajifunza nini basi? Imekupasa kuomba na kutafuta JINA lako ili uwe katika kusudi uliloitiwa na kuenenda katika hilo. Tena, MAJINA ya watu uyajuayo sasa yasikusumbue kwa maana " Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu" (Mathayo 21:31b), japo kwa sasa majina yao ni mabaya, kumbe Mungu anaona WATEULE wake!
Amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu, AMEN.
Frank P. Seth.

Comments