JE! MALANGO YAKO YA KIROHO YANATUMIWA NA NANI NA KUPITISHA VITU GANI KUJA MAISHANI MWAKO?(3)

Na Mwl Samwel Kibiriti


 inaendeleaa.

BAADHI YA MALANGO YA KIROHO NA VITU VINAVYOPITA HAPO LANGONI.
4: Malango ya sifa.
Kuna lango la sifa la mtu au familia au ukoo au mji au ofisi au mkoa au nchi au eneo au kijiji n.k Na kazi ya lango hili la sifa kazi yake ni kupitisha roho ya sifa iwe Nzuri au mbaya ndani ya huo mji au familia au ukoo au kijiji au kwa mtu.

Wewe hujawahi kusikia mtu anasema fulani yuko na tabia mbaya au tabia nzuri? Au watu wakisema familia Fulani iko na tabia nzuri au tabia mbaya? Au wakisema kuwa kijiji Fulani watu wake wako na tabia nzuri au tabia mbaya?
Sasa hizo tabia watu wanazosema ni sifa ya mtu. Nataka ufahamu jambo hili kwamba shetani akitaka kuharibu sifa yako nzuri & tabia yako nzuri huwa anatafuta hilo lango lako la sifa kwenye ulimwengu wa roho na kupitisha sifa au tabia mbaya kwenye maisha yako.
Pia hivyo hivyo shetani akitaka kuharibu tabia au sifa nzuri ya familia yenu au ukoo wenu au kijiji chenu au mkoa au eneo au ofisi au shule huwa anashikilia malango ya sifa yao na kupitisha sifa mbaya.

Tusome Biblia katika ISAYA 60:18 Inasema "....Na Malango yako, Sifa". Kwahiyo ombea sana lango lako la sifa pia lifunike kwa Damu ya Yesu kila siku.
5. Malango yanayopitisha Laana:
Kwenye ulimwengu wa roho maadui zako wakitaka kuyalaani maisha yako au kazi yako au biashara yako au familia yenu au ukoo wenu huwa hiyo laana ya maneno wanaipitisha kwenye malango yenu.
Ukisoma ZABURI 69:12 Biblia inasema "Waketio langoni hunisema...." Hili neno hunisema maana yake hunilaani. Kwahiyo ukiona laana ya maneno inakutesa maishani mwako ujue kwamba hayo maneno ya laana yamepitishwa kwenye malango yako.
6. Malango yanayopitisha Vita:
Unapoona unapitia Vita kwenye maisha yako kutoka kwa maadui ujue kwamba hivyo vita vinapita langoni.
Ukisoma kitabu cha ISAYA 28:6 Inasema "Naye atakuwa nguvu kwao wageuzao nyuma vita langoni"

Kwahiyo kama Leo hii unapitia maisha ya vita kutoka kwa maadui zako ujue kwamba hivyo vita vinapita kwenye malango yako ya kiroho. Kwahiyo ukitaka unyamazishe hivyo vita unavyoviona maishani mwako na kupata ushindi Mkuu hakikisha unafanya maombi ya vita kupitia langoni acha kubaki kulia lia.
Funga malango yanayotumiwa na maadui zako kukuletea vita maishani mwako



BAADHI YA MALANGO YA KIROHO NA VITU VINAVYOPITA HAPO LANGONI:
Tunaendelea na somo letu nabado nakuonyesha aina tofauti tofauti za malango ya kiroho na vitu vinavyoweza kupita au kupitishwa hapo vizuri au vibaya na kuja maishani mwako, na kujikuta unateseka na kupata shida maishani mwako.
7. ( Malango yanayopitisha roho ya upinzani na uadui )
Unapoona MUNGU amekufungulia nlango maishani mwako au kazini au kwenye biashara au mafanikio au Elimu n.k na ukajikuta unakutana na upinzani mkubwa sana na kuona maadui wamekuinukia, ufahamu kwamba huo upinzani na uadui unapitia kwenye hilo lango MUNGU alilokufungulia.
Tusome katika 1WAKORINTHO 16:8-9 Inasema "Lakini nitakaa Efeso hata pentekoste; kwa maana nimefunguliwa Mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao"
Hapa tunamuona mtume Paulo akieleza kwamba MUNGU amemfungulia mlango mkubwa sana huko Efeso lakini wako wengi maadui wakumpinga.

Wewe hujawahi kuona mtu anafunguliwa na MUNGU mlango wa kuolewa au kuoa lakini anakutana na upinzani mkubwa sana mpaka anakata tamaa? Au mtu anafunguliwa mlango na MUNGU wa kupandishwa cheo kazini lakini anakutana na upinzani mkubwa sana mpaka anatamani kuachia hiyo nafasi? Au mwingine amefunguliwa mlango mkubwa wa kihuduma na anapigwa vita mpaka na wapendwa wenzake?
Ukishaona MUNGU Baba amekufungulia mlango mahali kutokana na kumuomba uelewe kwamba maadui watakuinukia na kupitia kwenye huo huo mlango MUNGU aliokufungulia kwahiyo jambo la kufanya pambana na kila adui atakayeutumia huo mlango MUNGU aliokufungulia wasipite hapo.
8. ( Malango ya Adui )
Uadui una Mlango ambao ni eneo ambalo adui anaupitisha huo uadui ili ukufikie.
MWANZO 22:17
Inasema ".....Na uzao wako utamiliki mlango wa Adui zako". Hapa tunaona kwamba maadui wako na mlango ambao MUNGU alitaka uzao wa Ibrahimu uumiliki kiroho, na kama uzao wa Ibrahimu wangeshindwa kuumiliki mlango wa maadui zao, ina maana kwamba maadui zao watawamiliki na kuwasumbua wao.

Unapoona maadui wanakusumbua kwenye maisha yako ufahamu kwamba haujaumiliki mlango wao wa kiroho na wao wanatumia hayo malango yako kukutesa kwenye kila eneo la maisha yako. Je wewe umemiliki malango ya maadui zako au wao wamemiliki malango yako?
9. ( kuna Malango ya chuki ).
MWANZO 24:60 Inasema "....Na wazao wako waurithi Mlango wa hao wawachukiao". Hapa utaona ni wazazi wa mke wa Isacka aitwaye Rebeka wakimwambia uzao wake waurithi mlango wa wale wawachukiao.
Unapoona watu wanakuchukia kwenye maisha yako ujue kwamba hiyo chuki inapitishwa kwenye malango yako ya kiroho. Wako watu wengi ambao nimekutana nao wakinieleza jinsi wanavyochukiwa na marafiki zao au makazini au na mke au mume wake, au unaweza kukuta mtoto anachukiwa na wazazi au kuchukiwa na majirani n.k
Ukiona hivyo kila mtu anakuchukia bila sababu za msingi ujue shetani anamiliki malango yako. Je wewe unachukiwa na nani?



BAADHI YA MALANGO YA KIROHO NA VITU VINAVYOPITA HAPO LANGONI:
Tunaendelea na somo letu rafiki yangu.
10. ( Lango la Haki )
Hili ni lango linalopitisha roho ya Haki au kumpatia mtu Haki anayopaswa kuipata. Nataka utambue kwamba shetani akilikamata lango lako la Haki atakuzuia usipate Haki zako pia atakunyanganya.
Soma ZABURI 118:19-20 Inasema "Nifungulieni malango ya haki........"
Leo hii tunao watu wengi sana ambao wamepokonywa vitu ambavyo ni Haki zao mfano: mashamba, Mali, miradhi kwa mjane, mishahara yao, mifungo, nyumba zao, n.k bila kuelewa nikwanini wamepokonywa Haki zao.
Nataka nikuulize kwamba je wewe kuna vitu gani ambavyo ni Haki yako na umepokonywa au kudhurumiwa?

Wengine wameenda mahakamani au kwenye vyombo vya sheria kudai Haki zao lakini mwisho wa siku wamekosa hizo Haki zao, ngoja nikusaidie rafiki yangu kama mahali unapoenda kudai Haki zako hilo lango la Haki limekamatwa na shetani ufahamu wazi kabisa kwamba shetani atazuia hizo Haki zako usizipate kabisa.
Jambo la kufanya unapodai Haki zako mahali popote pale hakikisha unashughulikia hilo lango la Haki mahali hapo unapoenda kudai Haki zako na kumuomba Bwana Yesu akamate hilo lango lako la Haki na akupatie Haki zako unazoshahili kuzipata, pia kama umenyanganywa Haki zako muombe Bwana Yesu akurudishie vitu ambavyo umepokonywa vilivyo Haki zako.
11: ( Malango ya Ukiwa )
Hili nalo ni lango ambalo shetani amelitumia kuwatesa sana watu wengi. Hili lango kazi yake ni kupitisha roho ya ukiwa kwenye maisha ya mtu au kupitisha roho ya ukiwa kwenye eneo, kijiji, mkoa hata taifa, na kuwafanya hao watu waishi maisha ya ukiwa hata kama hawataki kuishi katika hali hiyo.
Ukiwa ni nini?
Ukiwa ni ile hali ngumu ambayo mtu hupita nayo bila kuona njia ya yeye kufanikiwa hata akianzisha kitu kinaporomoka au kuharibika ili abaki kwenye hali ya ukiwa.

Tusome katika MAOMBOLEZO 1:4 Inasema "Njia za sayuni zaomboleza, kwa kuwa hakuna ajaye kwa sikukuu; Malango yake yote yamekuwa Ukiwa".
Nataka utambue kwamba shetani akifanikiwa kukamata lango lako la maisha na akapitisha roho ya ukiwa utateseka sana kwenye maisha yako kupitia hali ngumu kimaisha bila kuona njia ya wewe kufanikiwa nahata ukianzisha kitu kipya kitakufa ili ubakie kwenye maisha ya ukiwa hata kama hutaki hayo maisha.
Tunao watu wengi sana ambao hawaoni njia ya kufanikiwa kwenye maisha yao mpaka kufikia kukata tamaa ya kuishi, pia tuko na watu wengi sana ambao kila kitu wanachoanzisha huwa kinakufa badala ya kuendelea kukua hicho wanachoanzisha na kujikuta wanaishi maisha ya ukiwa.
Sikiliza unapoishi kwenye eneo ambalo malango yake yanapitisha roho ya ukiwa ujue wewe hutaweza kusonga mbele na utaona uharibifu kwenye maisha yako na kujikuta unaishi maisha ya ukiwa.
Pia ukiishi kwenye eneo hilo kitu chochote utakachoanzisha hakitakua au kuongezeka Bali kitakufa na kujikuta unaishi eneo hilo kwa ukiwa. Wewe angalia maisha ya watu waliopo hilo eneo kwamba wanaishi maisha ya furaha au maisha ya ukiwa?

Je wewe mahali hapo unapoishi na kufanyia kazi zako hilo lango halipitishi roho ya ukiwa au kuua vitu vinavyoanzishwa?
Usikose sehemu ijayo ya somo hili na kama utahitaji maombi au ushauri basi unaweza kunipata kwa mawasiliano haya:
Simu +255 765 867574.
KUMBUKA KUOKOKA NI LAZIMA ILI UINGIE MBINGUNI KWENYE UZIMA WA MILELE.
BARIKIWA SANA NA BWANA YESU

Comments