KARAMA YAKO UNAITUMIA VIZURI AU VIBAYA?

Na Mtumishi Peter Mabula.
BWANA YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo tunajifunza kuhusu Karama.
Neno ''Karama'' maana yake ni kipawa anachojaliwa mtu kupewa kutoka kwa MUNGU ili kipawa hicho akitumie kwa mema na sio mabaya.
Neno ''Kipawa'' maana yake ni uwezo aliozaliwa nao mtu ambao humfanya mtu huyo kufanya jambo fulani vizuri.
Kila mtu amejaliwa kuwa na karama fulani kutoka kwa MUNGU lakini mipango ya MUNGU ni kwamba kila karama alizotupa lazima zitumike kwa mema tu.

Yohana 4;10 '' YESU akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya MUNGU, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai.'' 

Karama za rohoni huwa hazifanyi kazi kwa mtu ambaye hajaokoka, ila mtu huyo akiokoka basi na karama njema zinafufuka ndani yake.
BWANA YESU hapo juu amesema kwamba ''Kama ungaliijua karama ya MUNGU, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai''
YESU ana maji yaliyo hai yaitwayo WOKOVU. Tukiyanywa maji hayo tutampendeza MUNGU. 
Ndani ya Wokovu kuna karama mbalimbali ambazo MUNGU huzidhihilisha ndani ya wateule wake waliouchagua wokovu wake.

Kuna tofauti karti ya karama na huduma. 
=Karama ni ujuzi unaopewa na MUNGU.  
=Huduma ni kazi unayopewa na MUNGU.
Kuna tofauti kati ya karama na huduma lakini vyote viwili vinategemeana sana.


1 Kor 14:1 ''Ufuateni upendo, na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu.'' 

Kuna karama nyingi watu wamepewa na MUNGU lakini ni watu wachache tu wanaozitumia karama zao katika kusudi la MUNGU.
Leo kuna waimbaji wengi wa nyimbo za kidunia na kazi yao ni kumtukuza shetani na dhambi.
wengi wa waimbaji hao ukiwauliza walijigundua lini kwamba wana vipaji vya uimbaji watakuambia kwamba uimbaji wao walianzia kanisani, walipojiona wana vipaji waliondoka kanisani na kwenda duniani kumtukuza shetani.
Hawa wana karama lakini karama zao wanazitumia kwa shetani na sio kwa MUNGU.
Nimewahi kusoma historia ya uimbaji wa baadhi ya waimbaji maarufu sana duniani wanaomwimbia shetani, na katika historia hiyo karibia wote wanaeleza kwamba walianza uimbaji kanisani kisha walipogundua kwamba wana vipaji waliondoka kanisani na kuanza kuimba nyimbo za kidunia, walichobakiza tu ni kusema ''Nilikuwa mwanakwaya mzuri kanisani enzi naanza uimbaji''.
Kwa sasa wanazitumia karama zao vibaya sana maana wamekuwa lango la kuwapeleka watu kuzimu.
Kuna watu wana karama za kusikilizwa na watu lakini badala ya kuhubiri injili wao karama zao wamelekeza kwa shetani.
Kuna watu wana karama za uandishi lakini badala ya kuzitumia kwa MUNGU wao wanazitumia kwa shetani. Kuna vitabu vingi leo mitaani ni vya kuchochea ngono na pombe na machukizo mengi, vimeandikwa na wenye karama lakini karama zao wanazitumia kwa shetani na sio kwa MUNGU.
Kuna mtu mmoja aliwahi kuniuliza swali hili.
''Kwanini MUNGU hawaondolei karama alizowapa hawa wanamziki wa kidunia?''
 "Mbona MUNGU awewaachia sauti zao nzuri bila kuwaondolea japokua Wanaimba kwa kusifia dhambi tu?"

Nikamjibu.
Biblia inasema kwamba karama za MUNGU hazina majuto hivyo MUNGU amewaachia karama zao lakini iko jehanamu kwa ajili ya watenda dhambi na huko ndiko watu watajuta kuzaliwa, watajuta kumwimbia shetani.
Ndugu, hata shetani alipofukuzwa mbinguni hakuondolewa nguvu zake ila licha ya kuwa na nguvu fulani kwa sasa lakini anaingoja hukumu ya kutisha.


 ''Kwa sababu karama za MUNGU hazina majuto, wala mwito wake.-Warumi 11:29'' 

Kama MUNGU amekupa Baadhi ya karama fulani hata kama utaitumia vibaya MUNGU hatakuondolea lakini ukumbuke kwamba hukumu ya kutisha iko mbele yako kama hutatubu na kuokoka kwa upya.

Malaki 4:1 ''Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema BWANA wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi. ''

Nimesema kwamba kama MUNGU amekupa baadhi ya karama hata kama utazitumia kwa mabaya MUNGU hatakuondolea karama hizo ila kuna hukumu kwa waovu siku ya mwisho.
 Lakini kuna baadhi ya karama kama utazitumia kwa mabaya zitaondoa maana karama hizo zinasimamiwa na ROHO MTAKATIFU, hivyo kutenda kwako dhambi kutamuondoa ROHO wa MUNGU ndani yako na akiondoka ROHO wa MUNGU na karama zake zitaondoka kwako.
Mfano wewe umepewa karama ya unabii na matendo ya miujiza, kama ukimwacha YESU hakika karama yako hiyo pia itaondoka kwako. Ndio maana kuna baadhi ya watumishi walimtumikia MUNGU kwa muda mrefu lakini baadae kwa tamaa zao wakajitenga na KRISTO na MUNGU akaondoa karama zake zote kwao, na wao kwa sababu ya kutaka kujionyesha kwa watu kwamba bado MUNGU anawatumia wanaamua kwenda kwa waganga au kuzimu na kupewa karama za shetani ambazo zinafungamana na ulimwengu wa roho wa giza. ndio maana ni muhimu sana kujua kwamba sio kila anayeombea watu wakapona ni mtumishi wa MUNGU, kama yuko kinyume na KRISTO hakika huyo ni mtumishi wa shetani na sio wa MUNGU.
 
 Kuna watu wana karama ila wanazitumia kwa shetani badala ya kuzitumia kwa MUNGU, mfano waimbaji WA nyimbo za kidunia.

Kuna watu wana Huduma ndani yao ila hawajui wafanyeje.

Kila aliyeokolewa na BWANA YESU anayo karama ndani yake.
Kama hujui karama yako basi omba MUNGU akujulishe au muulize mchungaji wako ili akusaidie kujua karama yako.
Ni vizuri sana ukatumika kwa MUNGU kupitia karama yako hiyo ambayo MUNGU amekupa ili uitumie katika kumtukuza yeye.
Kila mtu ana karama yake japokuwa wengine MUNGU amewapa karama zaidi ya moja ili wamtumikie BWANA YESU.

1 Kor 7:7 ''Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa MUNGU, huyu hivi, na huyu hivi. ''

Lakini pia ni muhimu kukumbuka kwamba  karama za MUNGU hazina majuto ukiitumia karama yako vibaya ni kwa uangamivu wako mwenyewe.


=Ushauri wangu nakuomba uitumie vyema karama yako. 


2 Timotheo 1:6-10 ''Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya MUNGU, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana MUNGU hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa BWANA wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya MUNGU; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika KRISTO YESU tangu milele, na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu KRISTO YESU; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili;''
 
=Itumie kwa MUNGU na sio kwa shetani.

Mmea ukikua huonekana kwa umbo lake, na Imani ya mkristo ikikua huonekana kwa matunda yake mema, moja ya matunda mema ni karama kuanza kufanya kazi. Mimi sijui wewe ndugu una karama gani lakini nakushauri kwamba karama yako hiyo itumie kwa BWANA YESU tu.
Matunda ya mkristo mwenye imani ni kile kinachozaliwa kutokana kukua kwa imani yake.
Matunda ya mkristo ni kazi inayoleta faida katika ufalme wa MUNGU. 

Karama yako pia inaweza kuleta faida katika ufalme wa MUNGU na kwako pia mwenye karama.
Warumi 1:11 '' Kwa maana ninatamani sana kuwaona, nipate kuwapa karama ya rohoni, ili mfanywe imara;''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichako chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments